April 13, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Mwijage ‘aibuka’ na parachichi bungeni

Kilimo cha parachichi

Spread the love

CHARLES Mwijage, waziri wa zamani wa Viwanda na Mbunge wa Kaskazini (CCM), ameitaka serikali kueleza mpango wake katika kuwezesha wakulima wa zao la parachichi mkoani Kagera. Anaripoti Danson Kaijage, Dodoma … (endelea).

Amehoji, kwa kuwa zao hilo lina mahitaji ya kitaalam katika kulima mpaka kuvuna, kwanini serikali isiwapatie mafunzo maalum wataalam angalau wawili katika kila Wilaya za Mkoa wa Kagera ili waweze kuwaongoza wananchi wanaolima zao hilo?.

Leo tarehe 14 Aprili 2020, Wizara ya Kilimo imejibu swali hilo kwamba, zao la parachichi ni moja kati ya mazao ya asili ya matunda yanayozalishwa Kagera.

Imeeleza, wakulima wengi wamehamasika kuzalisha zao hilo kutokana na kuwepo kwa soko la kimataifa la parachichi hususan aina za HASS na FUERTE.

“Katika kuhakikisha kuwa wakulima wa parachichi mkoani Kagera wanapata miche bora, Wizara ya Kilimo kupitia Kituo cha Utafiti wa Kilimo cha TARI- Maruku, imeendelea kuzalisha na kusambaza miche bora ya parachichi katika Halmashauri za Mkoa wa Kagera.

“Katika msimu wa 2018/19, Kituo cha Utafiti Maruku kilizalisha na kusambaza miche 4,000 ya zao la parachichi kwa wakulima wa Halmashauri za Karagwe, Misenyi na Muleba” imeeleza wizara.

Aidha, imeeleza katika msimu wa 2019/20, kituo cha TARI Maruku kitazalisha miche ya parachichi 10,000 itakayosambazwa na kuuzwa kwa wakulima wa Kagera kwa bei nafuu.

“Wizara kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya za Mkoa wa Kagera, imeendelea kutoa elimu kuhusu uzalishaji wa miche bora ya zao la parachichi kupitia maonesho ya Nanenane msimu wa mwaka 2019/2020, na maafisa ugani wanne (4) kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Misenyi, walipatiwa elimu ya uzalishaji wa miche bora ya parachichi.

“Vilevile, wakulima zaidi ya 300 walipatiwa elimu ya uzalishaji wa zao la parachichi kupitia maonesho ya wiki ya uwekezaji mkoani Kagera yaliyofanyika Agosti, 2019.

“Wizara kupitia TARI Maruku kwa kushirikiana na Halmashauri za Wilaya za Mkoa wa Kagera zimeandaa mpango wa mafunzo kwa wataalam wa kilimo katika Halmashauri za Mkoa wa Kagera kuhusu mbinu bora za uzalishaji wa zao la parachichi ili waweze kutoa elimu hiyo kwa wakulima wa zao la parachichi,” wizara imeeleza.

error: Content is protected !!