August 19, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mwigulu atwikwa mzigo wa maiti

Mto Ruvu ambapo maiti sita zilipatikana zikiwa zinaelea. Picha ndogo kushoto ni Mwigulu Nchemba, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi na kulia ni Boniventure Mushongi, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani

Spread the love

MWIGULU Nchemba, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi na Boniventure Mushongi, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani wamedaiwa kuwajua watu waliohusika na mauaji ya watu saba ambao maiti zao ziliokotwa zikiwa kwenye viroba na kuzikwa eneo la Mto Ruvu, anaandika Josephat Isango.

Akizungumza na MwanaHALISI Online, Henry Kilewo, Katibu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Mkoa wa Dar es Salaam amesema, Mwigulu na Mushongi wanapaswa kusimamishwa na mamlaka husika ili kupisha uchunguzi wa suala hilo.

“Tumeipokea vema kauli ya Waziri Mkuu, Majaliwa Kasim ila mauaji haya watu wanaopaswa kuanza kuhojiwa ni Mwigulu na Mushongi ambao wameuthibitishia ulimwengu kuwa, maiti hizo zilikuwa za wahamiaji haramu,’ amesema Kilewo na kuongeza;

“Waziri anapotoa taarifa anakuwa amepokea kutoka kwa RPC, RPC anapokea kutoka kwa askari walio chini yake, kwa kuwa maiti haziwezi kuzungumza, maelezo ya Mwigulu na RPC yanaonesha kuwa, huenda watu hao walihojiwa na kubainika kuwa ni wahamiaji haramu kabla ya kuuawa kikatili na kuzikwa haraka.”

Amesema kuwa, kumekuwa na uharaka wa Mwigulu na Kamanda Mushongi kutolea tamko sakata hilo na kwamba, ni wahamiaji haramu bila kutaja ni wa nchi gani na kwanini hawakufanyiwa uchunguzi.

“Haraka hiyo ilikuwa inaficha nini? hatuwezi kuwa kimya kubaki na viongozi wa aina hii wasio na utu, wasioheshimu haki za binadamu, na uchunguzi wa haraka ulioagizwa na Waziri Mkuu, ufanyike lakini Mwigulu na Mushongi wapishe uchunguzi huu,” amesema Kilewo.

Kauli ya Kilewo inakuja siku moja baada ya kauli ya serikali iliyotolewa na Mwigulu kuhusu miili iliyopatikana ndani ya viroba na kuzikwa haraka bila kufanyiwa uchunguzi wa kina.

Mwigulu alitoa kauli hiyo jana Jumatatu katika kipindi cha Tuongee kinachorushwa na Kituo cha Star Televisheni huku Mushongi akinukuliwa na gazeti la Nipashe akikubaliana na maelezo hayo kuwa, miili iikuwa ya wahamiaji haramu.

Tarehe 08 Desemba, 2016 iliokotwa miili ya watu Kijiji cha Mtoni, Wilaya ya Bagamoyo. Maiti hizo zilizikwa haraka na Jeshi la Polisi bila kuacha vielelezo kama nguo za marehemu wala vipimo vyao vya vinasaba (DNA) ili kutoa nafasi kwa watu waliopotelewa na ndugu zao kwenda kuhakiki.

error: Content is protected !!