August 15, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mwigamba ampisha Zitto

Spread the love

ALIYEKUWA katibu mkuu wa chama cha ACT- Wazalendo, Samson Mwigamba, hatimaye amefika safari yake. Ameng’olewa katika “kiti chake cha utukufu,” anaandika Pendo Omary.

Anna Mghwira, mwenyekiti wa chama hicho taifa, amewaambia waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, kuwa Mwigamba ameondoka katika nafasi hiyo kwa kuwa ameomba kwenda masomoni.

Mghwira anasema, Mwigamba amepanga kujiunga na Chuo Kikuu cha Kenyata, tawi la Arusha. Amepanga kuanza masomo yake, Mei mwaka huu.

Anasema, kikao cha kamati ya uongozi cha chama hicho, kilichofanyika kwa dharura katika hoteli ya Kebby’s, kimeridhia Mwigamba la kuachia ngazi.

Kung’atuka kwa Mwigamba kumekuja miezi mitano baada ya taarifa kuvuja kuwa ndani ya ACT, kunafukuta mgogoro unaohatarisha uhai wa chama.

Mgogoro wa sasa, ni kati ya kiongozi mkuu wa chama, Zitto Zuberi Kabwe kwa upande mmoja na Mwigamba na Mghwira kwa upande mwingine.

Zitto anadaiwa kumpindua Mwigamba, baada ya kubaini cheo cha kiongozi mkuu wa chama, hakina nguvu kiutendaji.

Mkakati unaelezwa kuwa iwapo Zitto atafanikiwa kuwa katibu mkuu, nafasi yake ya “ukuu wa chama” atapewa Mghwira.

Hadi sasa haijawekwa wazi nafasi ya uenyekiti wa chama anaandaliwa nani; lakini taarifa za uhakika zinasema Zitto amenukuliwa akisema Mghwira amekuwa maarufu kuliko yeye na kuwa na nguvu kiutendaji kuliko kiongozi mkuu.

Mkakati wa kumg’oa Mwigamba katika chama, ulianza katikati ya Septemba mwaka jana.

Huu ni mgogoro wa pili kukikumba ACT- Wazalendo. Mgogo wa kwanza ulikuwa kati ya waanzishi wa chama – Kadawi Lucas Limbu, aliyekuwa mwenyekiti; Leopold Mahona na Grayson Nyakarungu – dhidi ya waliowaita “wavamizi” – Prof. Prof. Kitila Mkumbo, Mwigamba na Shaban Mambo.

Prof. Kitila, Mwigamba na Mambo, walitangazwa kufukuzwa katika chama hicho, 19 Machi 2014. Walituhumiwa kwa “usaliti, kuanzisha chama ndani ya chama na uchonganishi.”

Hata hivyo, katika mahojiano yake na MwanaHALISI, Jumamosi iliyopita, Mwigamba anakana madai kuwa amejiuzulu nafasi hiyo kwa shinikizo la viongozi wenzake.

Anasema, “sijajiuzulu kwa shinikizo kutoka kwa yeyote. Nimejiuzulu kwa kuwa nimepata nafasi ya kwenda masomoni. Nilikuwa na ndoto ya kujiendeleza sina budi kutimiza ndoto yangu.

“Siwezi kuwa katibu mkuu, wakati muda mwingi nitakuwa nje ya ofisi. Nafasi hii inahitaji muda kwa kuwa katibu mkuu ndiye msimamizi wa shughuli za kila siku za chama. Hauwezi kusimamia chama wakati uko masomoni.”

Alipoulizwa kwa nini asichukue likizo ili baada ya kumaliza masomo yake aweze kurejea katika nafasi yake, Mwigamba alisema, “sikuona umuhimu huo.”

Alipoelezwa mbona kuna watu wengi walioko masomoni wakiwamo wabunge, lakini hawajiuzulu nafasi zao, Mwigamba alisema, “hao ni wao. Mimi nimeamua kujiuzulu.”

Alipoelezwa kuwa gazeti hili linazo taarifa kutoka ndani ya ACT- Wazalendo, kwamba kujiuzulu kwake kumetokana na madai ya kutoiva pamoja na Zitto na baadhi ya wanaoitwa “wafuasi wake,” Mwigamba alisisitiza, “siyo kweli. Haya ninayokueleza, ndiyo kayaandike.”

Anasema, “…kama ingekuwa ni kweli, nisingejificha. Ndani ya ACT hakuna wafuasi wa Zitto wala wa Mwigamba wala wa Mghwira wala wa Kitila. Wote ni wanachama, wafuasi na wapenzi wa chama.”

Hata hivyo, Mwigamba anakili kuwa ndani ya ACT – Wazalendo, kuna vijana wengi watata ambao wasipoangaliwa kwa jicho la nyongeza, wanaweza kukiingiza chama katika migogoro. Hakufafanua.

Miongoni mwa anaowaja, ni pamoja na Habib Mchange, Ludovick Joseph na Gwanchele na kwamba wengine walikuwa wasaidi wake.

Alipoulizwa ikiwa kujiuzulu kwake hakuwezi kukidhoofisha chama hicho, Mwigamba anasema, “chama kina wanachama zaidi ya 1,000 (elfu moja). Wote hawa wanauwezo wa kuwa katibu mkuu na bado kikasonga mbele.”

“Hiki ni chama kikubwa sana. Chama cha namna hii hakiwezi kuyumba kwa kuondoka mtu mmoja. Hapa kilipofika ACT, hata wote sisi, mimi Zitto na Kitila tukiondoka, chama bado kitakuwa imara.”

Alipoulizwa amejifunza nini kuwa kwake katibu mkuu wa ACT, Mwigamba anasema, amejifunza huhitaji kuwa na mamilioni ya shilingi kubadilisha nchi.

“Nimejifunza wananchi wana kiu ya mabadiliko. Tulipoanzisha chama tukakiita cha mabadiliko na uwazi na kutangaza kurejesha misingi iliyoliasisi taifa letu, ikiwa ni pamoja na uzalendo kwa taifa na kutofanya siasa za matusi bali kueleza sera, mara moja wananchi walikipokea,” anaeleza.

Anasema, “ndiyo maana kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka jana kila chama kikazungumzia mabadiliko. Kila chama kikazungumzia uzalendo na uwajibikaji. Wagombea wakaeleza sera badala ya matusi. Uchaguzi ukawa na ushindani mkali kupita chaguzi zote.”

Alipoulizwa anaionaje Chadema, chama ambacho yeye alikuwa mwenyekiti wake mkoani Arusha, Mwigamba anasema, “…kimepoteza mwelekeo na mvuto wake ule uliokuwapo wakati sisi tukiwa wanachama.”

“Baada ya uchaguzi mkuu wa 25 Oktoba 2015, naiona Chadema kama chama kilichopotenza mvuto wake. Ni kweli kuwa watu walikichagua Chadema, lakini kutokana na udhaifu wao wa ndani, wameshindwa kura walizopata.

“Wabunge waliopatikana, pamoja na kuonekana kuwa wengi, hawaendani na hadhi ya chama. Idadi yao hailingani na nguvu ya chama na ukubwa wake. Yote haya yametokana na kiongozi mkuu wa chama kuishiwa mbinu za kuongoza chama,” anaeleza.

Alipoelezwa yawezekana anaeleza hayo kwa kuwa alifukuzwa ndani ya chama hicho, Mwigamba anasema, “hapana. Nayasema haya kwa kuwa napenda mageuzi.”

Anasema, “yale mambo yalikuzwa mno. Nimekuwa na mahusiano mazuri na viongozi wa Chadema. Nikienda pale makao makuu yao, kuna watu wananikumbatia. Hivyo haya ninayoeleza, hayana uhusiano wowote na kufukuzwa kwangu huko. Nayaeleza haya kwa kuwa naona Chadema hii siyo ile.”

Alipoulizwa kuwa ni kweli yeye na wenzake, Zitto Kabwe na Prof. Kitila, walitaka kufanya mapinduzi ya uongozi ndani ya chama hicho na kwa nini mkakati huo ulivuja, Mwigamba alisema, “hizi siyo hoja tena kwa sasa.”

Amesema, “…hatukupanga mapinduzi; bali tulitaka kumstaafisha kwa njia ya kura Mbowe mwenyekiti aliyeishiwa mbinu za kuongoza chama. Amekifanya chama kidumae huku akitudanganya kwamba tunaingia madarakani.”

Ndani ya Chadema, Mwigamba alituhumiwa kupanga mapinduzi kinyume cha taratibu, katiba na kanuni za chama hicho.

Akatuhumiwa kusambaza kilichoitwa, “waraka wa mabadiliko” uliodaiwa kusheheni matusi dhidi ya viongozi wakuu wa chama akiwamo Mbowe.

Makala hii imechapishwa katika gazeti la MwanaHALISI toleo la 336 la tarehe 25 Mei, 2016

error: Content is protected !!