December 5, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mwenzake Mdee adai Chadema iliwapa mashtaka mapya

Wakili wa Chadema, wakiongozwa na Peter Kibatala (katikati) wakiwa mahakamani

Spread the love

 

MBUNGE Viti Maalum, Nusrat Hanje, amedai Chama Cha Chadema, kiliwafanyia umafia katika mchakato wa kuwavua uanachama. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Akihojiwa maswali ya ufafanuzi na Wakili wake, Aliko Mwamanenge, leo Ijumaa, katika Mahakama Kuu, Masjala Kuu ya Dar es Salaam, Nusrat amedai miongoni mwa malalamiko yao mahakamani hapo, ni Chadema kuwapa mashtaka mapya.

Nusrat ametoa madai hayo mbele ya Jaji Cyprian Mkeha, katika kesi Na. 36/2022, aliyoifungua pamoja na wabunge wenzake viti maalum 18, kupinga mchakato wa kuwavua uanachama, wakidai si halali kwa kuwa hawakupewa nafasi ya kujitetea.

Wakili Mwamanenge alimhoji Nusrat wakati anahojiwa maswali ya dodoso na Wakili wa Mjibu Maombi namba moja (Chadema), Peter Kibatala, alikuwa anamaanisha nini aliposema Katibu Mkuu wa chama hicho, John Mnyika, alifanya zaidi tofauti na yaliyoanishwa katika muhtasari wa kikao cha Baraza Kuu la Chadema, cha tarehe 11 Mei 2022.

Ambapo alijibu akidai, “nianze kusema kwamba katika kitu kwenye maisha yangu, sijaona umafia kama mimi na wenzangu tuliofanyiwa,” amedai Nusrat.

Baada ya Nusrat kutoa majibu hayo, Wakili Kibatala alisimama na kuiomba mahakama hiyo imuelekeze Wakili Mwamanenge, amrudishe katika mstari pindi anapoona mteja wake anatoka nje.

Ambapo Jaji Mkeha, alimtaka Nusrat ajibu swali aliloulizwa.

Baada ya Jaji Mkeha kutoa muongozo huo, Nusrat aliendelea kudai kuwa walifanyiwa umafia kwa kutopewa nafasi ya kusikilizwa.

“Sababu ni kweli tumefanyiwa hivyo, ni ukweli mkiwa na malalamiko kuna upande mmoja watakuwa wanalalamika, upande wa wanaolalamikiwa na upande wa wanaotoa maamuzi. Ni kweli katibu mkuu anaruhusiwa kama mtendaji kufanya mawasilisho ya watu wanaolalamika Ili wanaotoa hukumu watoe. Huu ndio msingi wa malalamiko yangu, alipewa nafasi ya kuwasilisha lakini hatukupewa nafasi,” amedai Hanje.

Nusrat alidai kuwa, wakati Mnyika, anahitimisha kuwasilisha maamuzi ya Kamati Kuu ya chama hicho, ya kuwavua uanachama, aliibua mashtaka mapya.

Hata hivyo, Nusrat hakutaja mashtaka hayo mapya.

Alitoa madai ya kuongezewa mashtaka, baada ya Jaji Mkeha kumtaka ajibu swali la Wakili Mwamanenge, aliyemtaka ataje vitu gani ambavyo Mnyika alivifanya zaidi ya vile vilivyoandikwa katika muhtasari wa kikao cha Baraza Kuu la Chadema.

Nusrat alijibu kuwa Mnyika alikuwa miongoni mwa watu waliopiga kura katika kikao hicho. Alidai kitendo hicho hakikuwa sahihi kwani kulikuwa na nafasi ya kufanya mawasilisho.

Baada ya Wakili Mwamanenge kumaliza kumuuliza Nusrat maswali ya ufafanuzi kuhusu maswali ya dodoso aliyoulizwa na Wakili Kibatala dhidi ya malalamiko yake ya kufukuzwa Chadema bila kusikilizwa, Jaji Mkeha aliahirisha kesi hadi tarehe 8 na 9 Novemba 2022.

Siku hizo, watahojiwa maswali ya dodoso wabunge wengine wawili, Cecilia Pareso na Jesca Kishoa.

Wabunge hao viti maalum 19, wakiongozwa na Halima Mdee, walifungua kesi hiyo, wakiomba mahakama ifanye mapitio dhidi ya mchakato uliotumiwa na Chadema kuwavua uanachama, wakidai haukuwa halali.

Wabunge hao wanadai kuwa, Chadema hakikuwapa nafasi ya kujitetea.

Walifukuzwa Chadema tarehe 27 Novemba 2020 na Kamati Kuu ya chama hicho, ikiwa ni siku chache tangu waapishwe kuwa wabunge viti maalum, na aliyekuwa Spika wa Bunge, Job Ndugai.

Baada ya kufukuzwa, Mdee na wenzake walikata rufaa katika Baraza Kuu la Chadema, ambapo tarehe 11 Mei mwaka huu, Baraza Hilo lilitupilia mbali rufaa zao.

error: Content is protected !!