November 29, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Mwenzake Mbowe adaiwa kukutwa na silaha isiyosajiliwa

Spread the love

 

MRAJISI wa leseni za bunduki kutoka Jeshi la Polisi, Kamisheni ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai, Kitengo cha Udhibiti na Usajiliwa Silaha za Kiraia, SSP Sebastian Madembwe, amedai silaha aina ya bastola, inayodaiwa kuwa ya mshtakiwa wa pili, Adam Kasekwa, haijasajiliwa. Anaripoti Regina Mkonde, Dar ea Salaam … (endelea).

Ni katika kesi inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe na wenzake akiwemo Kasekwa, iliyopo Mahakama Kuu, Divisheni ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, Mawasiliano jijini Dar es Salaam.

SSP Madembwe ametoa madai hayo leo Alhamisi, tarehe 4 Novemba 2021, akitoa ushahidi upande wa Jamhuri mbele ya Jaji Joackim Tiganga.

Mrajisi huyo wa leseni za bunduki, ambaye ni shahidi wa sita ametoa madai hayo akiongozwa kutoa ushahidi wake mahakamani hapo na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Pius Hilla, akielezea uchunguzi uliofanywa na kitengo chake dhidi ya silaha hiyo bastola aina ya Luger yenye Serial Number A5340.

SSP Madembwe maedai, tarehe 25 Novemba 2020, alipokea barua ya maombi kutoka kwa Jeshi la Polisi, makao makuu ndogo jijini Dar es Salaam, Idara ya Upelelezi, kwa ajili ya kufanya uchunguzi wa silaha hiyo.

Shahidi huyo wa sita wa Jamhuri, amedai barua hiyo ilimtaka afanye uchunguzi wa taarifa za silaha hiyo ili kubaini kama inamilikiwa na mtu yeyote.

Amedai, baada ya kupokea maombi hayo alianza kufanya uchunguzi dhidi ya silaha hiyo, ambao ulionesha haijasajiliwa katika kitengo chake.

Amedai, baada ya matokeo hayo aliindika barua ya kuonesha matokeo ya uchunguzi kwenda kwa mleta maombi akieleza kufuatia uchunguzi uliofanyika, matokeo yake yanaonesha silaha hiyo haijawahi sajiliwa.

Silaha hiyo aina ya bastola inadaiwa kuwa ya Kasekwa, ambayo alikamatwa nayo tarehe 25 Agosti 2020, maeneo ya Rau Madukani, Moshi mkoani Kilimanjaro.

Kasekwa anadaiwa kwa kosa la kumiliki silaha aina ya bastola, risasi tatu na maganda ya risasi, kinyume cha sheria.

Mbali na Mbowe na Kasekwa, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni, Halfan Hassan Bwire na Mohammed Abdillah Ling’wenya.

Washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka ya kula njama za kufanya vitendo vya ugaidi.

Shahidi anaendelea kutoa ushahidi wake. Endelea kufuatilia MwanaHALISI TV, MwanaHALISI Online na mitandao yetu ya kijamii kwa habari na taarifa mbalimbali

error: Content is protected !!