August 15, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mwenyekiti Jumuiya Wazazi CCM asema kipindi cha nyuma walikalia msumari

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi CCM Taifa Dk. Edmund Mndolwa

Spread the love

 

MWENYEKITI wa Jumuiya ya Wazazi CCM Taifa Dk. Edmund Mndolwa, meupiga madogo uongozi uliopita kwa kile alichoeleza kuwa ni kupitia kipindi kigumu kiasi cha “kulazimishwa kukalia msumari uliogeuzwa.” Anaripoti Danson Kaijage, Dodoma … (endelea).

Dk.Mndolwa ametoa kauli hiyo leo Ijumaa tarehe 15 Julai, 2022, alipokuwa akitoa salamu za utangulizi kwenye kikao cha wakuu wa shule za umoja wa Wazazi CCM pamoja na kumkaribisha mgeni rasmi wa kikao hicho kilichofanyika makao makuu ya chama hicho Jijini Dodoma.

Akitoa salamu hizo Dk.Mndolwa amesema kuwa Jumuiya hiyo imepitia katika kipindi kutokana na kukosekana kwa utawala bora pamoja na kutokuwepo kwa uwazi katika utendaji wa kazi katika sekta mbalimbali.

“Mheshimiwa Katibu Mkuu Jumuiya yetu imepitia katika wakati mgumu wa kulazimishwa kukalia msumari uliogeuzwa na kulazimika kukaa.

“Lakini kwa sasa hali ni nzuri na Walimu Wakuu ambao wanaendesha shule za jumuiya ya wazazi wanaendelea kufanya kazi na hakuna mtu anayewaambia wanapoomba fedha waongeze cha juu na kama mwalimu yupo aseme,” ameeleza Dk.Mndolwa.

Katika hatua nyingine Mwenyekiti huyo wa Jumuiya ya Wazazi CCM Taifa ameeleza kuwa shule hizo zimekuwa zikifanya vizuri kuliko shule za serikali na shule za binafsi kwani hazijawahi kuwa na ufaulu wa daraja sufuri.

Amesema kuwa shule za jumuiya ya Wazazi CCM Taifa zimekuwa zikitoa ufaulu kwa asilimia 90 kwa kupata ufaulu wa daraja la 1-2 tofauti na shule za binafsi na shule za serikali.

Aidha amemuomba Katibu Mkuu wa CCM, kuona umuhimu wa kupitisha haraka mwongozo wa kuendesha shule hizo ili kuweza kuzidisha ufanisi zaidi.

Naye Katibu Mkuu wa CCM Taifa Daniel Chongolo amewataka wakuu wa shule hizo kuongeza bidii zaidi kwani pamoja na kufanya vizuri zinatakiwa kufanya vizuri zaidi.

Aidha amesema kuwa kuanzishwa kwa shule hizo kulilenga makundi matatu ambayo ni wanafunzi waliokuwa na ufaulu mzuri ,ufaulu wa kati na wale ambao hawakuweza kupata ufaulu mzuri wala wa kati lakini wanahitaji kuendelea na masomo.

“Kwa malengo hayo bado hayajaisha tunaitaji kuendelea kutimiza malego hayo kwa kuwapatia elimu bora waliofaulu vizuri,wenye ufaulu wa kati na wale ambao hawakuwa na ufaulu mzuri lakini wanahitaji kupata elimu ili nao wafaulu vizuri,” amesema Chongolo.

Mwisho.

error: Content is protected !!