January 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mwenyekiti Bavicha avuta pumzi Shinyanga

Mwenyekiti wa Baraza la Vijana Taifa la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Bavicha), Pastrobas Katambi

Spread the love

KADIRI uchaguzi mkuu wa Oktoba unavyokaribia, ndivyo sura mpya kwenye siasa zinachomoza na hivyo kuwatia hofu wawakilishi wanaoshikilia kata, majimbo na hata kiti cha urais kitakachokuwa wazi baada ya Rais Jakaya Kikwete kumaliza muda wake.

Pastrobas Katambi, ni Mwenyekiti wa Baraza la Vijana Taifa la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Bavicha). Ni Mwasheria kitaaluma na mmoja wa wanasiasa vijana anayejitokeza kwa mara ya kwanza kusaka ubunge katika Jimbo la Shinyanga Mjini.

Kwa sasa jimbo hilo, linashikiliwa na Naibu Waziri, Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Steven Masele (CCM), ambaye alimshinda kimiujiza mpinzani wake wa mwaka 2010, hayati Magadula Shellembi wa Chadema.

MwanaHALISIOnline limepata nafasi ya kufanya mahojiano na Katambi ili kujua sababu zinazomsukuma kujitosa kwenye ubunge katika jimbo hilo.

SWALI: Unaweza kutueleza historia yako kiufupi?

JIBU: Mimi naitwa Pastrobas Katambi, nimezaliwa mwaka 1985 katika familia ya mzee Katambi nikiwa mtoto wa nne kati ya watano.

Elimu yangu ya Msingi nimehitimu Mwenge mwaka 1999 na baadaye nikachaguliwa  kwenda Nsumba Sekondari ya jijini Mwanza lakini nilijiunga na Kahama Sekondari na baadaye nilihamia Seminari ya Mtakatifu Mary’s iliyopo Nyegezi Mwanza na kuhitimu mwaka 2004.

Baadaye nikachaguliwa kujiunga na shule ya Serikali ya wavulana Malangali iliyopo mkoani Iringa, nikasoma kidato cha tano na sita na kuhitimu mwaka 2007.

Mwaka 2007 nilichaguliwa katika vyuo vikuu vitatu vya Makerere nchini Uganda, Mtakatifu Augustino (SAUT) Mwanza na Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA), lakini nikajiunga SAUT kusoma shahada ya sheria kwa miaka mine.

Nikiwa mwaka wa tatu, nilianza kufanya kazi na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu cha jijini Dar es Salaam.

Baada ya kuhitimu masomo, uongozi  wa SAUT kwa ushawishi wa Makamu Mkuu wa Chuo mstaafu Dk. Charles Kitima ulitoa Scholarship kwa wanafunzi waliofanya vizuri katika shahada ya sheria, hivyo nikapata fursa ya kusoma shahada ya pili ya uzamilihapo hapo mwaka 2012.

Mwaka huo pia nikaanza kufanya kazi na ofisi za sheria za mawakili na baadaye nikaajiriwa katika kampuni ya Sahara Media Group.

Nikiwa katika kampuni hiyo kama Mwanasheria, nilifanya kazi kwa bidii na kupata mafanikio makubwa kwa muda mfupi na badaye nikaongezewa majukumu kuwa Meneja Utawala na Raslimali Watu msaidizi na baada ya kufanya kazi hiyo kwa kipindi kirefu nilijiuzulu nilipochaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Vijana Taifa.

Awali, bado nikiwa mwanachama wa kawaida wa Chadema pia nilifanikiwa kuongoza Tawi la SAUT kama mwenyekiti na baadaye nikawa mwanasheria wa kanda ya Ziwa Mashariki  (Serengeti) na Magharibi  Victoria wakati huo bado nikiwa nafanyakazi Sahara. 

SWALI: Una  muda gani tangu uingie kwenye siasa?

JIBU: Nimeanza siasa muda mrefu tangu mwaka 2003 na mwishoni mwa 2004 nilishiriki vyema uchaguzi mkuu 2005 nikiwa kidato cha tano kuipigia debe Chadema kwa sababu ya kuona nchi yetu imejaliwa rasilimali nyingi lakini viongozi wetu wengi ni wala rushwa.

SWALI: Kwanini umechagua jimbo la Shinyanga?

JIBU: Nimeamua kuomba kugombea jimbo hilo kutona na jimbo hilo kukosa maendeleo kwa muda mrefu na viongozi wa leo wanaopata nafasi wametanguliza mbele rushwa na kusababisha wananchi kukosa maendeleo.

SWALI: Mapungufu yapi umeyaona?

JIBU: Ndani ya chama changu sijaona mapungufu, hiki ndicho chama pekee ambacho hata Baba wa Taifa hayati Mwalimu Nyerere katika maoni yake aliwahi kusifu sera zake za utu, uadilifu, kupinga na kuchukia rushwa.

SWALI: Endapo utachaguliwa nini kipaumbele chako?

JIBU: Nikichaguliwa kuwa mbunge katika jimbo la Shinyanga mjini, kwa kuwa matatizo ni mengi sana na jimbo linahitaji mbunge muadilifu na mwajibikaji anaejua kero na shida sugu na umaskini wa watu wake, nitapambana ili watu wafahamu haki na usawa kwa wote, pamoja na kuboresha  huduma za jamii kwa kukuza na kuimalisha uchumi wa Shinyanga.

SWALI: Hali ya jimbo ikoje kielimu na miundombinu?

JIBU: Kwa kweli ni miaka 53 sasa tangu uhuru wa nchi  hii na jimbo hili limeongozwa na wabunge wa CCM lakini bado katika maeneo mengi hayajaunganishwa na barabara kwa kiwango cha lami.

Mkoa wenye dhahabu kila kona lakini unapambwa na barabara za mashimo hadi mjini pia huduma za maji na umeme kwa watu wengi hazipatikani, shule hazina vitabu na vifaa vya kufundishia pamoja na upungufu wa maabara.

SWALI: Unadhani tatizo ni nini?

JIBU: Tatizo ni uhaba wa walimu na vifaa na hilo linasababisha wanafunzi wengi kutokufaulu vizuri pia walimu hawana nyumba za kuishi, mishahara midogo na bado wanaidai Serikali na wanachereweshewa kupanda madaraja. Haya yote ni matatizo na kero zinazopaswa kutatuliwa.

SWALI: Umejipanga vipi kuwasaidia wananchi?

JIBU: Nikipitishwa na Chadema na kuchaguliwa mbunge wa Shinyanga, nitaweka mipango imara na sera makini zinazotekelezeka, ushirikishwaji na uwajibikaji wa kila mtu kwa uadilifu na upendo kwa manufaa ya wananchi.

Nitahakikisha nyota ya matumaini inarejea na kutoa nuru kupitia utetezi na usimamiaji makini wa kodi za wananchi katika halmashauri na bungeni.

SWALI: Vijana wanamchango gani katika uchaguzi?

JIBU: Vijana wana mchango mkubwa sana wa kushiriki moja kwa moja kwa kugombea ama kupitia uwakilishi kumchagua kijana katika nafasi ya uongozi ikiwa ni pamoja na kunadi sera, kampeni, kusimamia kituo kama mawakala, kuhesabu na kulinda kura kwani wizi wa kura huvuruga amani kwa kulazimishwa kuongozwa na mtu ambaye hawakumchagua.

SWALI: Kwanini vijana wengihawapigi kura?

JIBU: Vijana wengi hawashiriki katika uchaguzi kwa sababu zamani walikuwa hawaelewi umhimu wa kuchagua viongozi bora, matatizo ya vijana yanasababishwa na kukithiri kwa rushwa, ubaguzi na upendeleo kwa watoto wa viongozi na matajiri na kuweka tabaka la wasiokuwa nacho na kusababisha vijana kukosa fursa za ajira. 

Wito wangu sasa kwa vijana waliokuwa wakilalamikia kero hizo, kutumia vizuri fursa ya kujitokeza kwa wingi kujiandikisha katika daftari jipya la kudumu la wapiga kura mara tu uandikishaji huo utakapotangazwa katika maeneo yao.

Hii ndiyo itakuwa fursa pekee kwao, kuendelea kulalamika hakutawasaidia kama hawatachukua hatua kwa vitendo ili kupata haki ya kuwachagua viongozi bora na makini wawatakao.

Makala haya yameandikwa na Mwandishi Wetu mkoani Mwanza 

error: Content is protected !!