July 7, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mwelekeo Z’bar unatisha

Mbunge wa Jimbo la Mkanyageni, Injinia Mohamed Habib Mnyaa

Spread the love

KAMBI Rasmi ya Upinzani Bungeni imesema, hali ya kisiasa Zanzibar inatisha baada ya vikosi vya ulinzi visiwani humo kupewa silaha kisha kuwapiga wananchi wakati wa kujiandikisha kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura. Anaandika Dany Tibason … (endelea).

Kambi hiyo imesema, kitu kibaya zaidi ni kwa askari hao kuvaa ki-ninja ili kuficha sura zao kisha kuwachukua baadhi ya wananchi majumbani mwao usiku wa manane, kuwapiga na kuwatesa na baadaye kuwatupa msituni wakiwa taaban.

Kauli hiyo imetolewa leo bungeni na Msemaji wa Kambi ya Upinzani, Mohamed Habib Mnyaa (CUF) alipokuwa akiwasilisha maoni ya kambi hiyo kuhusu Muswada wa Sheria ya Benki ya Posta Tanzania katika kufuta na kuweka masharti ya mpito 2015.

Kutokana na hali hiyo, kambi rasimi ya upinzania bungeni imeitaka Serikali ya Jamhuri ya Muungano Tanzania kuchukua hatua madhubuti za kuzuia vitendo vinavyofanywa visiwani humo vinginevyo, wanakaribisha machafuko yasiyo na ulazima.

“Mwanzo wa kutoweka kwa amani unaanza taratibu na kama hatua zisipochukuliwa, majuto yatakuwa ni mjukuu na amani tayari imeanza kutoweka Zanzibar,” amesema Mnyaa.

Mnyaa amesema, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaisihi na kuionya kwa kuitaka serikali iwaandikishe watu wote wenye sifa katika Daftari la Wapiga Kura kwa Bara na Zanzibar ili kufikisha makisio ya wapigakura milioni 24.

Amesema, hakutakuwa na uchaguzi wa huru na haki ikiwa idadi kubwa ya wapiga kura imeachwa kuandikishwa na kukoseshwa haki yao ya kikatiba.

Amesema, hatua ya CUF kususia Baraza la Wawakilishi Zanzibar ni ya kidemokrasia na hufanyika popote pale Duniani pale chama kinaposhindwa kukubaliana na jambo kwa njia ya kistaarabu.

“Kwa kuwa uchaguzi huru ni mchakato unaoanzia katika daftari la kuandikisha wapiga kura, hivyo basi kitendo chochote cha kuwazuia au kutokuwaandikisha wapiga kura iwe Bara au Zanzibar ni jambo la hatari la kukiuka Demokrasia na kuufanya uchaguzi usiwe huru na wa haki,”amesema Mnyaa.

Kutokana na kauli hiyo Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, asiye na Wizara Maalum, Prof. Mark Mwandosya alilazimika kusimama na kumtaka msemaji huyo kujielekeza katika hoja badala ya kuedelea na taarifa za visiwani Zanzibar.

“Mheshimiwa Mnyaa tena mwanafunzi wangu sasa naona kuwa unaelekea kusahau, nimekusikiliza na tumejaribu kuvumilia kukusikiliza lakini naona unaacha mada unaelekea kwingine.

“Naomba uendelee kama nilivyokufundisha ili uweze kujielekeze katika mada iliyopo mezani badala ya kuendelea na mambo ambayo yanaonekana kuwa nje ya kile ambacho tunatakiwa kujielekeza kwake,” amesema Prof. Mwandosya.

Akimalizia amesema, Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) utatoa mgombea Urais mmoja na kuleta matumaini ya Watanzania na kwamba, wanaojidanganya kuwa umoja huo utafarakana, wajue wazi wanaota ndoto za mchana na watasubiri sana.

error: Content is protected !!