
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEM), Aggrey Mwanri
SERIKAILI imezitaka halmashauri zote nchini kuhakikisha hawawalipi wakandarasi fedha za kukodisha vifaa wanavyotumia katika kufanya matengenezo mbalimbali katika miradi ya barabara. Anaandika Dany Tibason … (endelea).
Haya yamebainishwa bungeni na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEM), Aggrey Mwanri alipokuwa akijibu swali la msingi la Mbunge wa Hai, Freeman Mbowe (Chadema).
Amesema Halmashauri hazitakiwi kulipa malipo ya ukodishaji wa vifaa, bali hutakiwa kuwalipa wakandarasi fedha stahiki kwa kuzingatia vipimo vya kazi zilizofanywa.
“ Wazabuni wanapoandaa viwango vya malipo ya kazi hujumuisha gharama za mitambo, vifaa uendeshaji wa ofisi, faida, pamoja na nguvu kazi, hivyo halimashauri hazitakiwiki kuwalipa fedha za kukodishia mitambo,” amesema
Serikali ilisitisha matumizi ya wataalamu wa Halmashauri katika kutekeleza miradi ya barabara ambapo sasa kazi zinafanywa na makandarasi.
Aidha, Mwanri amesema Serikali imetoa jumla ya sh bilioni 3.7 katika kipindi cha miaka 10 kwa ajili ya matengenezo mbalimbali ya barabara za Wilaya ya Hai yenye mtandao wa barabara za lami, changarawe na udongo zenye urefu wa kilomita 412.
Akizungumzia ushauri wa kuzitaka halmashauri kuwa na mitambo ya ujenzi wa barabara, Mwanri amesema utekelezaji huo unafanywa na halmashauri zenyewe kwa kuzingatia vipaumbele vilivyowekwa na kupata kibali kutoka wizara na kutolea mfano halmashauri ya Mbinga, Masasi.
Amesema halmashauri zinatakiwa kutumia asilimia 2 ya fedha zinazotengewa halmashauri, hivyo kuzitaka kutumia vyanzo vingine katika kununua vifaa hivyo.
Katika swali la msingi, Mbowe alitaka kujua kama Halmashauri ya Hai inamtandao wa barabara za lami, changarawe na udongo za kilomita ngapi.
Aidha, alitaka kujua Serikali imetoa fedha kiasi gani kwa ujenzi wa barabara hizo kwenye fedha zilizotolewa, ni kiasi gani kimetumika kwa ajili ya kukodishaji wa mitambo ya ujenzi.
More Stories
Dk. Mpango atoa maelekezo saba matumizi ya Kiswahili
Wadau wa mwani kukutana Zanzibar
DUWASA wakata maji Soko la Mavunde, wafanyabiashara walia