January 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mwandosya awaangukia UKAWA

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Kazi Maalum), Profesa Mark Mwandosy

Spread the love

KUTOKANA na wabunge wanaounda umoja wa katiba ya wananchi (UKAWA), kutangaza kutomsikiliza Rais, Jakaya Kikwete wakati wa hotuba yake ya kuvunja bunge, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Kazi Maalum), Profesa Mark Mwandosya, ameibuka na kutaka bunge litunge kanuni zinazowataka wabunge wote kuwapo bungeni wakati rais anapokuwa akilihutubia Bunge. Anaandika Dany Tibason … (endelea).

Amesema iwapo itatungwa kanuni hiyo itawalazimisha baadhi ya wabunge wenye tabia ya kususia vikao vya Bunge katika mazingira yasiyokubalika.

Profesa Mwandosya alitoa pendekezo hilo bungeni alipokuwa akichangia Muswada wa Kutunga Sheria ya Tume ya Utumishi wa Walimu ya Mwaka 2015.

Kauli ya Prof .Mwandosya ilionesha moja kwa moja kuwalenga wabunge wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), ambao wamesusia vikao vya Bunge mwanzoni mwa wiki hii japo hakuwataja.

Kwa pamoja wabunge hao wakiongozwa na Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, walichukua uamuzi huo baada ya kutoridhishwa na hatua ya Serikali ya kuwasilisha na kupitisha miswada ya sheria ya mwaka huu inayohusu masuala ya gesi, mafuta na petroli.

Amesema kitendo cha kuodoka bungeni wakati rais wa nchi anatarajia kulihutubia Bunge ni tukio la fedheha na halitakiwi kuungwa mkono.

Amesema duniani kote ujio wa rais katika Bunge ni jambo muhimu kitaifa.

Alieleza kwamba bora itungwe kanuni ya kuwalazimisha wabunge wote kuwapo bungeni siku rais anapokwenda bungeni vinginevyo mbunge awe na sababu maalum.

Wakati Mwandosya akisema hayo, Mbunge wa Bariadi Mashariki, John Cheyo (UDP), naye alionyesha kutoridhishwa na tabia ya wabunge wa Ukawa kususa vikao vya Bunge.

Cheyo, amesema hakuna mtu anayeweza kuzuia mhimili wowote usifanye kazi hata kama mtu huyo haridhishwi na kazi zinazofanywa na mhimili huo.

“Leo hii nataka niwaambie wananchi ni kwa nini mimi niko hapa wakati wenzangu wa upande huu (eneo wanalokaa Ukawa) hawapo.

“Hakuna mtu anayeruhusiwa kuzuia mhimili wowote usifanye kazi.

“Kwa mfano, huwezi kwenda Ikulu ukasema rais haiingi hapa ili asifanye kazi zake, huwezi kwenda mahakamani ukasema mahakama isifanye kazi na vile vile huwezi kuja bungeni ukasema Bunge lisifanye kazi.

“Tulipokuwa kwenye Bunge la Katiba wenzetu hao walikimbia Bunge, tulipokuwa tukijadili miswada ya gesi, mafuta na petroli wakakimbia Bunge, sasa mimi nimebaki kwa sababu nataka kuwawakilisha wananchi wangu,” amesema Cheyo.

error: Content is protected !!