July 1, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mwandosya atangaza nia ya urais kiaina

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Kazi Maalum), Prof. Mark Mwandosya akizungumza bungeni

Spread the love

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais (Kazi Maalum), Prof. Mark Mwandosya ametangaza kung’atuka ubunge wa Rungwe Mashariki, akisema kwamba sasa anahitaji kulitumikia Taifa katika majukumu mengine mazito. Anaandika Edson Kamukara … (endelea).

Akichangia hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya bajeti ya Ofisi ya Rais, Mwandosya ambaye anatajwa kuwa na mpango wa kugombea urais katika uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu, amesema kipindi cha miaka 15 kinatosha.

“Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla ya kumaliza mchango wangu, naomba kuwashukuru sana wananchi wa jimbo langu la Rungwe Mashariki. Hili tumeishazungumza lakini pia nisema hapa kwamba ubunge wangu wa vipindi vitatu vya kupita bila kupingwa, imetosha.

“Sasa nahitaji kufanya majukumu mengine makubwa ya kitaifa,” amesema Prof. Mwandosya bila kuweka wazi kama anamaanisha kuwania urais na hivyo kusababisha baadhi ya wabunge kumshangilia.

Hata hivyo, amewaonya baadhi ya vijana wa vyama vya upinzani wanaoendelea kutangaza nia za kutaka kulinyakuwa jimbo hilo, kuwa wawe makini kwa sababu wenye jimbo wapo.

Katika kinyang’anyiro cha uteuzi wa mgombea urais ndani ya CCM mwaka 2005, Prof. Mwandosya alishika nafasi ya tatu nyuma ya Rais Kikwete na Dk. Salim Ahmed Salim na hivyo kazidisha changamoto kwa watia nia katika uchaguzi ujao.

Miongoni mwa wabunge ambao wametangaza kutowania tena ubunge na hivyo kugeukia urais ni Dk. Khamis Kigwangalah (Nzega), Bernard Membe (Mtera), Lazaro Nyalandu (Singida Kaskazini), January Makamba (Bunbuli) na Mizengo Pinda (Mlele).

Wanasiasa wengine wa CCM ambao hawajaweka wazi nia zao za urais japo wanatajwa ni Stephen Wassira (Bunda), Edward Lowassa (Monduli), Mwigulu Nchemba (Iramba Magharibi), Samuel Sitta (Urambo Mashariki), Dk. Harrison Mwakyembe (Kyela), Dk. Emmanuel Nchimbi (Songea) na Dk. Asha-Rose Migiro (Kuteuliwa).

error: Content is protected !!