Thursday , 28 March 2024
Home Habari Mchanganyiko Mwandishi wa habari, swahiba wa January Makamba, ahojiwa uraia wake 
Habari MchanganyikoTangulizi

Mwandishi wa habari, swahiba wa January Makamba, ahojiwa uraia wake 

Spread the love

JESHI la Polisi, Kanda Maalum ya Dar es Salaam, limekiri kwa mara ya kwanza hadharani kuwa linamshikilia mwandishi wa habari za uchunguzi, Erick Kabendera. Anaripoti Hamis Mguta … (endelea).

Akizungumza na waandishi wa habari leo, Jumanne ofisini kwake jijini Dar es Salaama, Kamanda wa Polisi wa Kanda hiyo, Lazaro Mambosasa amekiri kuwa jeshi lake, linamshikilia Kabendera kwa madai ya utata wa uraia wake.

Mombasasa ametoa kauli hiyo, katika kipindi ambacho waandishi wa habari wa ndani na kimataifa; asasi za kiraia na nchi wahisani, wakipaza sauti yao kutaka kujua kilichompta Kabendera na hatima yake.

Kwa mujibu wa Mambosasa, jeshi lake lilimkamata Kabendera jana tarehe 29 Julai 2019, nyumbani kwake Mbweni, jijini Dar es Salaam. Amedai kuwa hatua ya jeshi hilo kuvamia nyumbani kwa mwandishi huyo na kumkamata, imetokana na kile alichokiita, “kukaidi amri ya jeshi la Polisi.”

“Tofauti na inavyoelezwa na baadhi ya watu, kwamba mwandishi huyu wa habari alitekwa na watu wasiojulikana. Ukweli ni kuwa hajatekwa. Amekamatwa na jeshi la polisi na sasa tunamshikilia kutokana na utata wa uraia wake,” ameeleza Mambosasa.

Amesema, “tulimuita kwa njia ya kawaida ili kufanya naye mahojiano. Lakini akakataa kuja. Hivyo tukaamua kumkamata kwa kutumia taratibu zetu na sheria nyingine za nchi.”

Amesema, Jeshi la Polisi linamhoji Kabendera kwa kuwa lina mashaka na uraia wake. Amedai mwandishi huyo awali aliandikiwa barua ya wito kufika polisi kwa ajili ya mahojiano lakini hakuitikia wito huo.

Kamanda Mambosasa amesema, mahojiano yakimalizika, watamfikisha Kabendera kwenye Idara ya Uhamiaji.

Amesema, “tutakapobaini kuwa anayo makossa, mara moja tutamkabidhi kwenye idara ya uhamiaji ili kushughulika naye; na ndiyo maana alikuwa akikaidi wito wa polisi na kujihami kuwa ametekwa.”

Erick Kabendera, ni mwandishi wa habari za uchunguzi na mchambuzi wa masuala ya kisiasa; uchumi na usalama wa kikanda. Anaripoti katika magazeti mbalimbali, likiwamo Africa Confidential linalochapishwa nchini Uingereza. Aliwahi kuhojiwa uraia wake miaka 10 iliyopita, lakini polisi walisema wamejiridhisha kuwa hakuwa na shida.

Katika siku za karibuni, Kabendera ameripotiwa kuandika Makala kwenye gazeti la The East Africa, inayokosoa hatua ya Rais John Magufuli, kutengua wadhifa wa uwaziri wa Janury Makamba.

Kabendera, ni mmoja wa marafiki wa karibu wa January na kwamba katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, kwa kutumia ukaribu wake na January, mwandishi huyo wa habari alisaidia kwa kiwamgo kikubwa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kufanya uchambuzi wa kampeni zake za uchaguzi.

Mwandishi mmoja mwandamizi ambaye hakupenda kutajwa gazetini amesema, “nashangaa yanayoendelea nchini. Yaani mtu anakamatwa kama mnyanganyi au mhaini, bila kuelewa tuhuma dhidi yake, kinyume kabisa cha sheria.

“Waandishi tunawindwa kama Eagle awindavyo Sungura mbugani? Eti, tufanye nini ili tusione matukio ya aina ya Eric, Azory Gwaga ni mabaya? Watetezi wa watesi tusaidieni, ujinga huu wa kujijingisha tuukubali vipi?

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaTangulizi

CAG: Wastaafu, wenza wao chanzo NHIF kufilisika

Spread the loveRIPOTI ya ukaguzi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu...

Habari za SiasaTangulizi

Vikundi hewa 851 vyalamba bilioni 2.6 mikopo ya halmashauri

Spread the loveVIKUNDI hewa vya wajasirimali wadogo 851 kutoka katika halmashauri 19...

Habari za SiasaTangulizi

Mashirika matano yapata hasara mabilioni ya fedha

Spread the loveMASHIRIKA matano ya Serikali yanayojiendesha kibiashara, yamepata hasara ya mabilioni...

Habari Mchanganyiko

Mtandao watetezi wa haki za mazingira Tanzania waundwa

Spread the loveMTANDAO wa watetezi wa haki za mazingira nchini Tanzania, umeundwa...

error: Content is protected !!