
Gerald Kitabu
MWANDISHI wa gazeti la The Guardian Gerald Kitabu amejitosa katika kinyang’anyiro cha ubunge katika Jimbo la Nsimbo Mkoa wa Katavi kupitia chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA). Anaandika Jimmy Mfuru … (endelea)
Kitabu ambae ni mshindi wa tuzo ya uandishi wa habari ya SADC ambayo hutolewa kwa mwandishi bora anaeandika habari za maendeleo na mazingira katika nchi za jumuiya ya nchi za kusini mwa Afrika, alichukua fomu hizo hapo katika ofisi za Chadema jimbo la Nsimbo zilizopo katika kijiji cha Songambele, Tarafa ya Nsimbo Wilaya ya Mlele, Mkoani Katavi.
Kadhalika, Mbali na kushinda tuzo ya SADC, mwandishi huyo pia hivi karibuni alishinda tuzo mbili kubwa katika nafasi ya kwanza, moja ikiwa ya TANAPA (2013), na nyingine ya Baraza la Habari Tanzania (MCT) (2014) katika kipengele cha mazingira.
Akizungumza na mamia ya wafuasi wa chama hicho pamoja na wananchi wa jimbo la Nsimbo waliokusanyika katika ofisi za chama hicho jimboni hapo, amesema amesukumwa na uzalendo wake kwa jimbo hilo kutokana na changamoto kadhaa zinazowakabili wananchi wa jimbo hilo.
Alizitaja baadhi ya changamoto hizo kuwa ni pamoja na usimamizi mbovu wa rasilimali, mikataba ya hovyo isiyojali maslahi ya wananchi na taifa ikiwemo mikataba ya uwekezaji katika kilimo, na rushwa hali ambayo imepelekea huduma duni za jamii kama vile maji, barabara, afya na elimu.
“Miaka michache iliyopita, kuna mkataba mmoja wa Katumba na Mishamo ulisainiwa kati ya viongozi wa Halmashauri ya wilaya ya Mpanda na mwekezaji wa kampuni ya AgriSol kutoka Marekani. Katika mkataba ule wa miaka 99, ikitokea kuna mgogoro kati yao na mwekezaji, unawalazimu wananchi husika kwenda kusikiliza kesi Uingereza hali ambayo wananchi maskini hawawezi kumudu gharama za usafiri na mawakili wa kuwasimamia ” alisema Kitabu.
Aidha, alizitaja kero nyingine kuwa ni kukithiri kwa aina mbalimbali za ushuru wa mazao ambao unaishia mifukoni mwa wajanja wachache hali ambayo ina lalamikiwa sana na wakulima na wafanya biashara hapa mkoani.
“Soko la Mkoa lina vibanda 356 na meza 284. Kila banda linalozwa ushuru wa sh. 15,000/- kwa mwezi, wakati meza moja inatozwa sh. 300 kwa siku ambayo ni sawa na sh.9,000 kwa mwezi. Hii ina maana kwamba jumla ya mapato yote kwa mwezi ni zaidi ya shilingi milion 7 na nusu. Cha ajabu pamoja na mapato makubwa, soko linazidi kuwa kongwe na chafu hata kufikia hatua ya kukimbiwa na baadhi ya wateja wastarabu wakiwemo baadhi ya watalii wanaokuja kutembelea Hifadhi ya taifa ya katavi” amesema.
Amesema endapo atapitishwa na chama chake kipaumbele chake kitakuwa kuweka mipango thabiti inayotekelezeka ikiwemo ufuatiliaji wa mikataba mibovu na usimamizi wa rasilimali zilizomo kama vile madini.
“Nina imani na chama changu ambacho kipo mbele kupiga vita ufisadi wa aina yoyote, tukiweza kupiga vita rushwa na tukasimamia vizuri rasilimali zetu na mapato yatokanayo na ushuru, maendeleo ya haraka yatapatikana katika jimbo langu na Mkoa kwa jumla” amesema.
Aidha,amesema Mpanda ina vipaji vingi, atahakikisha kuwa michezo ya aina yote inapewa kipaumbele ili kuinua vipaji vilivyokuwepo hapo awali.
Katika zoezi hilo la kuchukua fomu, wafuasi wa chama hicho, akina mama na vijana walimchangia pesa ya kuchukua fomu jumla ya sh.250,000.
More Stories
Sensa ya watu na makazi Tanzania ni zaidi ya kuhesabiwa
Mambo yanayombeba Rais Samia kimataifa
Waziri Mkuu Uingereza aponea kung’olewa