July 29, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Mwandishi wa Z’bar aliyetekwa asakwa

Spread the love

SALMA Said, mwandishi wa Gazeti la Mwananchi linalomilikiwa na Kampuni ya Mwananchi Communication (MCL) anasakwa na wadau wa habari nchini, anaandika Faki Sosi.

Mwandishi huyo ambaye pia ni mwakilishi wa Shirika la Utangazaji la Ujerumani (DW), alitekwa jana kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.

Taarifa za awali zinaeleza kwamba, Salma tayari alikuwa amepata taarifa kwamba anasakwa na Jeshi la Polisi visiwani humo na hivyo kuamua kuondoka.

Leo Dar es Salaam Baraza la Habari Tanzania (MCT), Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) Taasisi ya Vyombo vya Habari Afrika ya Kusini (Misa-Tanzania), Mtandao wa Kutetea Haki za Binaadamu (THRDC), Umoja wa Klabu za Wanahabari Tanzania (UTPC) amekutana kujadili hali iliyomkuta mwandishi huyo

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jijini Dar es Salaam, Kajibi Mkajanga, Katibu Mtendaji wa MCT amelaani kitendo cha kukamatwa kwa mwandishi huyo.

Amesema, kitendo hicho ni kinyume cha haki za binaadamu na kinaminya uhuru wa wanahabari na haki ya kupata habari na kuwa kinajenga hofu kwa wanahabari na wanajamii.

Mkajanga amesema kuwa, hadi sasa haijulikani madhira gani ambayo anayapata na kuwa, haijajulikana yupo kwenye hali gani.

Amesema kuwa, Salma aliwahi kutumiwa jumbe na kupigiwa simu za vitisho juu ya habari anazoziripoti.

Mkajanga ametoa msisitizo kwa Jeshi la Polisi na vyombo vyote vya usalama kuhakikisha kuwa, yupo salama na kufuatilia kilichomsibu kwa undani,

Onesmo Olengurumwa, Mratibu wa Kitaifa wa THRDC amesma kuwa, endapo hatopatikana hadi Jumatatu mtandio huo utafungua kesi mahakamani ya kuitaka serikali imtafute mwandishi huyo.

Theophil Makunga, Mwenyekiti wa TEF amesema kuwa, waandishi hawatakiwi kukata tamaa wala kurudi nyuma kwenye kuripoti na kuandika.

Maongezi ya Salma na DW

Baada ya Salma kutekwa na watu hao, walimpa simu ili kutoa taarifa kwamba amekamatwa. Salma aliwasiliana na DW ambapo na kuwaeleza maelezo yafuatayo.

“Nilipotoka nje ya Uwanja wa Ndege wa Dar es Salaam namtafuta mwenyeji wangu ambaye alikuja kunipokea sikumuaona, nikajaribua kupiga simu sikumpata ndio mbele nikaona gari nyeusi imesimama wakatoka watu wakaniingiaza katika gari hilo kwa nguvu.”

Salma akaendelea kusema kuwa, aliwaambia watu hao kuwa yeye ni mgonjwa wa Moyo lakini ‘walimuliza ‘wewe si unaripoti DW?’ Akajibu ndio.

Wakamwambia ‘unaandika kwenye magazeti na mitandao, hujui kwamba taarifa zako zinaharibu sifa ya serikali.”

error: Content is protected !!