SIKU moja baada ya Rais wa Uganda, Yoweri Museveni kuweka wazi kwamba atamlazimisha mwanaye Muhoozi Kainerugaba ambaye pia ni jenerali mkuu wa majeshi ya Uganda kwamba aache kutumia mtandao wa Twitter, Muhoozi ameibuka na kudai kwamba hang’atuki ng’o katika mtandao huo. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).
Muhoozi kupitia kwenye mtandao huo wa Twitter amejibu madai hayo na kusema kwamba hamna mtu yeyote atakayemlazimisha kufanya jambo lolote kwa sababu yeye pia ni mtu mzima.
Jenerali huyo wa jeshi ambaye hivi karibuni ameibua mijadala kutokana na jumbe zake anaoziweka katika mtandao huo wa twitter, amesisitiza kuwa mtu mzima ambaye hawezi kupigwa marufuku kufanya chochote.
“Nasikia mwanahabari fulani kutoka Kenya alimwomba baba’ngu anipige marufuku kutoka kwa Twitter? Je, huo ni utani fulani? Mimi ni mtu mzima na hakuna mtu atakayenipiga marufuku kwa lolote!” aliandika.
Museveni ambaye alikuwa katika mahojiano ya kipekee na mwanahabari wa Kenya, Sophia Wanuna alisema kwamba mtandao wa Twitter si mbaya bali kinachozingatiwa ni kile ambacho mtu anapakia kwenye akaunti yake.
“Unatarajia kumwambia Muhoozi atoke Twitter pengine?” Wanuna alimuuliza Rais Museveni ambaye alijibu;
“Jenerali Muhoozi ataondoka Twitter. Tumekuwa na mjadala huu, unajua Twitter sasa hivi ni njia ya kisasa ya kuwasiliana na yeye ameungana na vijana wenzake ambao anafanya mambo nao, lakini suala ni kuhusu ni kile unachotweet,” Museveni alijibu.
Leave a comment