January 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mwanaume apandikiziwa moyo wa nguruwe kwa mara kwanza duniani

Daktari wa upasuaji Bartley P. Griffith (kushoto) akiwa na David Bennett (kulia) mapema mwezi huu.

Spread the love

MWANAUME raia wa Marekani amekuwa mtu wa kwanza duniani kupandikizwa moyo wa nguruwe aliyebadilishwa vinasaba (GMO). Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea)

Kwa mujibu wa daktari ni kwamba mwanaume huyo aliyefahamika kwa jina la David Bennett, mwenye umri wa miaka 57, anaendelea vyema siku tatu baada ya upasuaji wa majaribio hayo uliofanyika katika mji wa Baltimore.

Upandikizaji wa moyo huo unachukuliwa kama matumaini ya kuyaokoa maisha ya Bennett, ingawa haijawaekwa wazi kama ni fursa ya kiasi gani aliyonayo ya kuishi maisha marefu.

“Ulikuwa ni upandikizaji wa kufanya niishi au nife,” Bennett alielezea siku moja kabla ya upasuaji.

“Ninafahamu kwamba ni jambo la kubahatisha, lakini ni chaguo langu la mwisho,” alisema.

Madaktari wa Chuo Kikuu cha Maryland cha tiba walipewa idhini maalum na wasimamizi wa matibabu kuendelea na upasuaji huo, kwa misingi kwamba iwapo Bennet angekufa.

Chuo kikuu cha tiba cha Maryland kilisema katika taarifa yake kwa umma, mwanaume huyo alikuwa ameonekana kwamba hakuwa na uwezo wa kupandikiziwa moyo wa binadamu, uamuazi ambao mara nyingi huchukuliwa na madaktari wakati mgonjwa anapokuwa na afya duni sana.

Kwa timu ya madaktari iliyofanya upandikizaji huo, mafanikio hayo yamehitimisha miaka kadhaa ya utafiti na yanaweza kubadili maisha kote duniani.

Daktari wa upasuaji, Bartley Griffith alisema upasuaji utaileta dunia katika “hatua moja ya kukaribia kutatua mzozo wa ukosefu wa kiungo cha mwili”.

Hatua hiyo imefikiwa huku watu 17 kwa siku hufariki nchini Marekani wakati wakisubiri kufanyiwa upasuaji wa kupandikiziwa viungo, huku zaidi ya 100,000 wakiripotiwa wakisubiri upasuaji.

Uwezekano wa kutumia viungo vya wanyama kwa ajili ya kile kinachoitwa xenotransplantation ili kufikia mahitaji umekuwa ukifikiriwa kwa muda mrefu na matumizi ya mishipa ya moyo wa nguruwe tayari limekuwa ni jambo la kawaida.

Mwezi Oktoba, 2021, madaktari wa upasuaji mjini New York walitangaza kwamba wamefanikiwa kupandikiza figo ya nguruwe kwa binadamu.

Wakati huo, upasuaji huo ulikuwa ni jaribio la teknolojia ya hali ya juu zaidi kuwahi kufikiwa.

Hatahivyo, ubongo wa mtu aliyepandikiziwa ulikufa na hakuna matumaini ya kupona.

Hata hivyo,  Bennett ana matumaini kuwa upandikizaji wake wa moyo wa nguruwe utamuwezesha kuendelea na maisha yake.

Alikuwa amelala kitandani kwa wiki sita mfululizo kabla ya kufanyiwa upasuaji na aliwekewa mashine ambayo ilimuwezesha kuendelea kuishi baada ya kupatikana na maradhi yanayoua ya moyo.

“Natazamia kunyanyuka na kuondoka kitandani baada ya kupona,” alisema wiki iliyopita.

Jana tarehe 10 Januari, 2022 – Bennett aliripotiwa kupumua mwenyewe huku akiendelea kufuatiliwa kwa karibu.

Aidha Shirika la Habari la Ufaransa (AFP) limeripoti kuwa kile kitakachotokea baadaye hakijawekwa wazi.

Nguruwe aliyetumiwa katika upandikizaji alifanyiwa mabadiliko ya vinasaba ili kuondoa jeni kadhaa ambazo zingefanya kiungo hicho kikataliwe na mwili wa Bennet.

Griffith anasema wanaendelea kumfuatilia kwa makini na kwa uangalifu mkubwa, huku mwanae wa kiume David Bennett Jr akiliambia Shirika la Habari la Associated Press kwamba familia yao iko “katika hali ya sintofamu wakati huu”.

Lakini aliongeza: “Alitambua ukubwa wa kile kilichofanyika na anatambua umuhimu wake.”

”Hatujawahi kufanya hili kwa binadamu na ninapenda kufikiria kwamba tumempatia chaguo bora kuliko kile ambacho kingetokea kama angeendelea kupewa matibabu aliyokuwa akiyapata,” alisema Griffith. Lakini hatujui iwapo ataishi kwa siku, wiki, mwezi au mwaka.”

error: Content is protected !!