Saturday , 15 June 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Mwanasheria Bawacha: Spika atimize wajibu wake
Habari za Siasa

Mwanasheria Bawacha: Spika atimize wajibu wake

Esther Daffi, Mweka Hazina Bawacha, Jimbo la Kawe
Spread the love

 

MHAZINI wa Baraza la Wanawake la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (BAWACHA), katika jimbo la Kawe, Esther Dafi amesema, amesikitishwa na upotoshaji wa makusudi unaofanywa na Spika wa Bunge, Job Yustino Ndugai na baadhi ya wabunge 19, waliofukuzwa uanachama katika chama hicho. Anaripoti Nasra Bakari, DMC … (endelea).

Amesema, “…nimekuwa mfanyakazi wa makao makuu ya Chadema, kwa takribani miaka 10 sasa. Nimebahatika kufanyakazi Bawacha. Nimeshiriki baadhi ya vikao vya Kamati Kuu na nimewahi kuwa katibu wa Kamati Ndogo za Kamati Kuu, zilizoundwa kushughulikia mambo mbalimbali. 

“Mimi ni mwanasheria. Ninafahamu taratibu, kanuni na Katiba ya Chadema, kuhusiana na jambo hili. Kamati Kuu, haijawahi siyo tu kupeleka majina, hata kufanya maamuzi ya jambo hilo.” 

Esther ameeleza hayo, katika taarifa yake aliyoituma kwa vyombo vya habari, imeeleza kuwa hoja ya wanaoitwa, “wabunge wasio na chama” kudai kuwa katibu mkuu wa Chadema, John Mnyika, amepeleka orodha ya majina Tume ya taifa ya uchaguzi (NEC), ni uwongo unaolenga kupindisha mjadala wa uvunjifu wa Katiba, unaofanywa na Spika wa Bunge, Job Ndugai.

 Mwanasheria huyo, alikuwa akijibu madai ya Felister Njau, mmoja wa waliokuwa wanachama wa Chadema, waliofukuzwa ndani ya chama hicho.

Job Ndugai Spika wa Bunge la jamhuri ya muungano wa Tanzania

Njau ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Bawacha, katika jimbo la Kawe, alinukuliwa wiki iliyopita akisema, kuwapo kwao bungeni, kuna baraka za chama.

Alisema, Kamati Kuu ya Chadema, iliridhia kupelekwa majina ya wabunge wa Viti Maalum, na kwamba baada ya mashauriano, walikubaliana kuundwa kwa Kamati Ndogo ya Kamati Kuu, ili kufanya kazi ya uchambuzi.

Njau alidai kuwa Mnyika, alipeleka majina NEC, lakini hayakuwa yale waliokubaliana kwenye vikao.

Aidha, Njau aliendelea kudai kuwa mwenyekiti wa NEC, ndiye aliyemjulisha Halima Mdee, aliyekuwa mwenyekiti wa Bawacha taifa, kuhusu jambo hilo na baada ya kumsomea majina hayo, ndipo Mdee akamueleza kuwa siyo yenyewe. Mwenyekiti wa NEC, akaruhusu kupelekwa mengine.

Esther anahoji: “Kama madai haya ya Njau, ni ya kweli, majina ya round ya pili, aliandika nani? NEC yawezekana kuwasiliana na Mdee, badala ya katibu mkuu wa chama.”

Anaongeza: “Nani aliyejaza fomu Na. 8 (d), inayojazwa na katibu mkuu wa chama, kwa wabunge wa viti maalum.”

Halima Mdee

Kabla ya madai haya kujitokeza, kulikuwa na clip ya mmoja wa hao wabunge feki,” akinukuliwa akimtaja Mkurugenzi wa NEC, Dk. Wilson Mahera, kuwa amewasiliana naye na kwamba majina yaliandaliwa nyumbani kwa Mdee. 

Akizungumzia hoja ya Spika Ndugai, kwamba Chadema kiwasilishe  mwenendo wa shauri la Mdee na wenzake ofisini kwake, ili kujiridhisha kuwa Kamati Kuu, ilitenda haki na kiambatanishe orodha ya wajumbe wake; na huo ndio utakuwa utaratibu wa kushughulikia masuala ya aina hiyo, mwanasheria huyo alisema, “hoja ya Ndugai, haina mashiko kwenye macho ya kisheria.”

Amesema, “Bunge letu linaendeshwa kwa mujibu wa Katiba, Sheria za nchi, Kanuni, mila na destuli za mabunge ya Jumuiya ya Madola, maamuzi mengine ya spika waliotangulia na busara za kiti.

“Katika jambo hili, Ibara Ibara ya 67 (1) (b), ya Katiba inaelekeza, mtu anayepaswa kuwa mbunge, ni sharti awe mwanachama wa cha siasa na aliyependekezwa na chama chake. Wanaoitwa wabunge wa Chadema, tayari wamefukuzwa uanachama.”

Anasema, hata sheria ya uchaguzi, inavitaka vyama vya siasa, vinavyoshiriki uchaguzi mkuu wa rais, wabunge na madiwani, kuwasilisha kwa mkurugenzi wa uchaguzi, orodha ya majina ya wanachama wake, wanaopendekezwa kuwa wabunge wa viti maalum.

“Chadema hakijawahi kupendekeza kwa NEC, majina ya wabunge wa Viti Maalum. Chadema hakijawahi kujaza fomu Na.8, inayopaswa kujazwa na wanachama wa chama cha siasa, waliopendekezwa na chama chao, kuwa wabunge wa Viti Maalum,” ameeleza.

Kuhusu hoja ya kupeleka mwenendo wa kamati kuu, Esther anasema, “sheria hairudi nyuma. Kama kuna sheria mpya inatungwa na Bunge, basi utekelezaji wake, utakuja kwenye jambo jingine litakalofuata. 

“Maamuzi ya sasa ya Spika ya kutaka Chadema, kuwasilisha nyaraka hizo, ni batili kwa mujibu wa sheria, kwa kuwa maamuzi dhidi ya wahusika yameshafanyika.”

Akifafanua zaidi, Esther ambaye kitaaluma ni mwanasheria anasema, “Spika hawezi kuamua jambo moja kwa kutumia taratibu mbili tofauti. Maamuzi yake ya sasa, yanapingana na maamuzi yake kwa wabunge nane wa Chama cha Wananchi (CUF), waliofukuzwa uanachama na chama chao. 

“Maamuzi yake ya sasa, yanapingana na yale aliyoyafanya dhidi ya Sophia Simba, ambaye alikuwa mbunge wa Viti Maalum (CCM). Kama anataka kutengeneza taratibu mpya kwenye kesi moja, basi kazi hiyo, inapaswa kutungiwa kanuni, na siyo maamuzi yake binafsi na utekelezaji wake, sharti ufanyike kwa jambo jingine litakalokuja.”

“Anachotaka kufanya hapa, ni kupanua goli, katikati ya mchezo. Hilo haliwezekani,” amesisitiza. 

Anasema, amesikika Spika Ndugai akisema, baada ya kupokea barua ya Chadema, atawaita wahusika na kuwapata nafasi ya kuwasilikiza.

“Nijuavyo mimi,” Esther anasema, “Spika siyo mamlaka ya rufaa ya wabunge wala vyama vinavyofukuza wabunge wake,” anaeleza na kuongeza, “anaposema anataka kuwasikiliza kina Mdee, maana yake pia atatoa nafasi ya kuisikiliza Chadema?” Anahoji, mamlaka hayo anayo?

Mdee na wenzake 18, walifukuzwa uanachama wa Chadema na Kamati Kuu, iliyokutana tarehe 27 Novemba 2020, jijini Dar es Salaam. Wengine waliofukuzwa pamoja na Mdee, ni Ester Bulaya na Esther Matiko; Nusrat Hanje, Grace Tendega, Hawa Mwaifunga, Jesca Kishoa na Agnesta Lambat.

Wengine, ni Tunza Malapo, Asia Mwadin Mohamed, Cecilia Pareso, Naghenjwa Kaboyoka, Sophia Mwakagenda, Kunti Majala, Salome Makamba,  Anatropia Theonest, Conchesta Lwamlaza, Felister Njau na Stella Siyao.

Mdee na wenzake hao walifukuzwa uanachama baada ya kutuhumiwa na kupatikana na makosa ya utovu wa nidhamu na usaliti; kuhujumu chama, upendeleo, kutengeneza migogoro; kushirikiana na wanaokitakia mabaya chama, kughushi nyaraka na kwenda bungeni kujiapisha, kinyume na maekelezo na maamuzi ya chama.

Esther anasema, “kufuatia maamuzi haya,  Spika Ndugai, hana uhalali wowote wa kuwabakiza bungeni Mdee na wenzake, kwa kuwa mtu hawezi kuwa mbunge, bila kupitia chama cha siasa. Hili limeelezwa vizuri na Spika mstaafu, Pius Msekwa, ambaye ni mmoja wa viongozi wanaoheshimika sana nchini.”

Anasema, ni wajibu wa Spika kutekeleze wajibu wake wa kulinda na kuitetea Katiba, badala ya kuendelea kuisigina na kuchafua taswira ya nchi.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

BiasharaHabari za Siasa

Tanesco yawasha mtambo namba 8 Bwawa Julius Nyerere

Spread the loveNaibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko...

Habari MchanganyikoHabari za SiasaTangulizi

Samia: Wakuu wa mikoa, wilaya wanaendeleza ubabe

Spread the loveRAIS Samia Suluhu Hassan amesema bado wakuu wa wilaya na...

Habari za SiasaKimataifaTangulizi

Ramaphosa achaguliwa tena kuwa rais Afrika Kusini

Spread the loveRais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa amechaguliwa na wabunge wa...

Habari za SiasaKimataifaTangulizi

DA, ANC waridhia kuunda serikali ya mseto Afrika Kusini

Spread the loveChama tawala nchini Afrika Kusini cha African National Congress, ANC,...

error: Content is protected !!