September 27, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mwanamke anyofoa sikio la mpenzi wake kisa nauli bodaboda

Spread the love

MWANAMKE mmoja mkazi wa mtaa wa Kawangware, Kaunti ya Nairobi nchini Kenya, amepandishwa kizimbani kwa tuhuma za kumng’ata sikio mpenzi na kulinyofoa kabisa.

Imeelezwa kuwa mwanamke huyo Zainab Ochero alifanya kitendo hicho baada ya Joseph Karanja, mpenzi wake kumpa KSh 100 (Tsh 2000) kama nauli ya kurudi nyumbani kiasi ambacho mwanamke huyo hakuridhika nacho. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea)

Mwanamke huyo alifikishwa mbele ya Hakimu Mwandamizi wa Kibera, Charles Mwaniki tarehe 1 Machi, 2022 na kukanusha shtaka la kumsababishia Joseph Karanja majeraha.Alidaiwa kutenda tukio hilo katika mtaa wa Kangemi jijini Nairobi tarehe 21, Februari 2022.

Taarifa ya polisi ilieleza kuwa mwanamke huyo kwa hasira alimvamia mwanaume huyo na kumng’ata sikio la kushoto kabla ya kulitema.

Alipoona sikio lake likiwa chini, Karanja alilinyanyua na kulibeba kwa uangalifu ndani ya mfuko wa plastiki na kuelekea hospitalini kwa matibabu.

Polisi wanasema kuwa mwanamume huyo aliambiwa atafute matibabu zaidi katika hospitali nyingine huko Eastlands, ambako aliambiwa kuwa sikio lilikuwa limeharibika kabisa hivyo atafanyiwa upasuaji baada ya matibabu ya miezi mitatu.

Wapenzi hao walikuwa wamekutana kufanya kikao ili kujadili tofauti zao baada ya Karanja kumshutumu mwanamke huyo kuwa si muaminifu.

Wawili hao hawakusuluhisha tofauti zao, na Ochero akaamua kumpigia simu mhudumu wa boadaboda ili ampeleka nyumbani Kawangware.

Kutokana na kauli hiyo, Karanja alimpa nauli mpenzi wake KSh 100 ya kurudi nyumbani hali ambayo ilielezwa kumpandisha hasira kwa sababu kilikuwa ni kiwango kidogo cha fedha.

Akiwa tayari amekerwa na madai ya kuwa na uhusiano wa kimapenzi na kupewa KSh 100 kama nauli, Ochero aliamua kumng’ata Karanja sikio na kumdhuru vibaya.

Hakimu Mwandamizi Charles Mwaniki aliagiza mwanamke huyo aachiliwe kwa dhamana ya KSh 300,000 (Tsh milioni 6) na kesi hiyo itajwe Jumatano tarehe 16 Machi, 2022.

error: Content is protected !!