ASKARI wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), MT 89487 CPL, Hamis Ramadhan, anayedaiwa kumsukuma askari wa usalama barabarani kwa kutumia gari lake, amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni, jijini Dar es Salaam, kwa mashtaka ya kukataa amri halali. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Ijumaa tarehe 24 Februari, 2023 na Jeshi la Polisi, Ramadhan amefikishwa mahakamani jana tarehe 23 Februari 2023 na kusomewa mashtaka hayo mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Rahim Mushi na Wakili wa Serikali, Vailer Kyendesya.
Akimsomea mashtaka hayo, Wakili Kyendesya amedai tarehe 7 Februari 2023, Ramadhan akiwa eneo la Mlimani City Barabara ya Survey, Kinondoni, jijini Dar es Salaam, akiendesha gari namba T. 433 ALB , aina ya Nissan Patrol alisimamishwa eneo la kivuko cha watembea kwa miguu na Askari Polisi, ambapo alikaidi na kuanza kumsukuma kwa gari yake.
Baada ya kusomewa shtaka hilo, Ramadhan alikana na kisha Wakili Kyendesya alidai upelelezi wa kesi hiyo umekamilika, hivyo anaiomba Mahakama kupanga tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.
Hakimu Mushi ameahirisha kesi hiyo hadi tarehe 6 Machi mwaka huu, kwa ajili ya kutajwa.
Hatua hiyo imekuja baada ya Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Jumanne Sagini kuliagiza Jeshi la Polisi kumkamata na kumchukulia hatua dereva huyo aliyeonekana kwenye video iliyosambaa mitandaoni akikaidi amri ya kusimama iliyotolewa na Askari wa usalama barabarani.
Leave a comment