MWANAHARAKATI huru, Bihimba Mpaya ameshirikiana na wadau wengine kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi wa Mtaa wa Magole A, uliopo Kivule, jijini Dar es Salaam, kwa kuchangia ujenzi wa ofisi ya Serikali ya mtaa na ukarabati wa barabara eneo la mlima Nyang’andu ambalo ni korofi wakati wa mvua. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam…(endelea).
Bihimba amekabidhi misaada hiyo katika nyakati tofauti kwa Mwenyekiti wa Mtaa wa Magole, Abubakari Kindagule.
Akizungumza baada ya kukabidhi misaada hiyo ikiwemo lori la mawe kwa ajili ya ukarabati wa barabara na nondo kwa ajili ya ujenzi wa ofisi ya serikali ya mtaa, Bihimba alisema amechukua uamuzi huo ili kuunga mkono jitihada za viongozi wa nchi kuwaletea maendeleo wananchi wake.
“Kwa muda mrefu wananchi wamekuwa wakipata shida ya barabara hususan wakati wa mvua, magari huwa yanakwama na hata kuhatarisha usalama wao kutokana na eneo la mlima Nyang’andu kuwa korofi. Serikali ya mtaa imejitahidi kutatua lakini nimeona bora niongeze nguvu kwa kutoa roli moja la mawe,” amesema Bihimba.
Kwa upande wake Kindagule, ameshukuru kwa msaada uliotolewa na Bihimba, akisema utasaidia kukamilisha ujenzi wa ofisi yake.
“Kwa muda mrefu mtaani kwetu tulikaa bila ofisi ya Serikali ya mtaa, tulikuwa tumepanga na changamoto za upangaji mnazijua. Kama mwenyekiuti nilinunua kiwanja hiki kwa ajili ya familia lakini nimelitoa kwa ajili ya ofisi kisha nikaanza kutafuta wadau kwa ajili ya kuniunga mkono,” alisema Kindagule na kuongeza:
“Namshukuru Bihimba amejitokeza kwa kutoa msaada wa ujenzi wa ofisi, lakini pia amechangia ukarabati wa eneo la barabara ambalo limekuwa kero kwa wananchi kwa muda mrefu.”
Leave a comment