August 8, 2022

Uhuru hauna Mipaka

MwanaHALISI ndani ya Ikulu

John Magufuli, Mwenyekiti wa CCM (wa pili kulia) akiwa na viongozi wenzake katika Mkutano wa NEC uliofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam

Spread the love
MABADILIKO makubwa ya uongozi yaliyofanywa ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Dk. John Pombe Magufuli, yalitabiriwa na gazeti dada la MwanaHALISI Online (MSETO), miezi sita iliyopita, anaandika Yusuph Katimba. 

Katika toleo lake Na. 475 la tarehe 30 Juni hadi 6 Julai 2016, MSETO liliripoti kuwa zipo taarifa kuwa CCM inatarajia kufanya mabadiliko ya muundo na ungozi, kwa lengo la kuleta ufanisi.

Habari kwenye MSETO ilibeba kichwa cha maneno kisemacho: “Lukuvi kupangua Baraza la Mawaziri.”

Gazeti la MSETO linamilikiwa na kampuni ya Hali Halisi Publishers Limited (HHPL), inayomiliki pia MwanaHALISI, MwanaHALISI Online na MwanaHALISI Forum.

Habari katika MSETO ilimtaja mwanasiasa anayechipukia kuchukua nafasi ya Nape Nnauye, Katibu wa Halmashauri Kuu (NEC), Itikadi na Uenezi, Humphrey Polepole.

Polepole hajawahi kuwa mwanachama wa CCM. Anatarajiwa kupewa kadi kwa siri muda wowote kutoka sasa.

Hata hivyo, MSETO lilifungwa na serikali kwa miezi 36, kuanzia 11 Agosti 2016. Lilituhumiwa kuandika habari za uchochezi na uzushi.

Soma habari kamili juu ya mabadiliko ndani ya chama tawala kama iliyoandikwa na MSETO:

RAIS John Magufuli yuko mbioni kufanya mabadiliko makubwa katika Baraza la Mawaziri, MSETO linaripoti.

Mabadiliko yatatokana na mkakati unaosukwa kwa ustadi na baadhi ya viongozi waandamizi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Viongozi hao wanalenga kumshinikiza Rais Magufuli kumteua mmoja wa mawaziri wake waandamizi kushika wadhifa wa katibu mkuu wa CCM.

Anayetajwa kuwa chaguo la viongozi waandamizi wa CCM katika nafasi ya katibu mkuu wa chama hicho ni Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi.

Lukuvi anapigiwa chapuo ya kushika nafasi hiyo na rais mstaafu Benjamin Mkapa; mwenyekiti wa chama hicho, Jakaya Mrisho Kikwete na makamu mwenyekiti wa CCM (Bara), Philip Mangula.

Kwa sasa, nafasi ya katibu mkuu wa CCM inashikiliwa na Abdulrahaman Kinana (pichani) aliyekichukua chama hicho mikononi mwa Wilson Mkama.

“Huyu Lukuvi (William Lukuvi) ndiye anayetufaa katika nafasi ya ukatibu mkuu. Tunamfahamu. Amekuwa katika chama hiki tokea akiwa mdogo,” ameeleza mmoja wa viongozi wa chama hicho kwa sharti la kutotajwa gazetini.

Anasema, “Lukuvi ni miongoni mwa makada wachache ambao hawana makundi ndani ya chama chetu. Kutokana na sifa hizo na ukongwe wake kwenye chama, tunashawishika kumkabidhi nafasi hiyo.”

Kabla ya kuingia serikalini, Lukuvi amefanya kazi katika Umoja wa Vijana wa chama hicho (UV-CCM) kwa miaka mingi; amekuwa serikalini mfululizo tangu utawala wa awamu ya tatu chini ya Benjamin Mkapa.

Mkutano Mkuu Maalum wa CCM umepangwa kufanyika tarehe 23 Julai mwaka huu mjini Dodoma; na utatumiwa na Kikwete kung’atuka katika nafasi ya uenyekiti na kumkabidhi Rais Magufuli.

Kwa mujibu wa taratibu za CCM, Rais wa Jamhuri ya Muungano anayetokana na chama hicho, ndiye hukabidhiwa mikoba ya kuongoza chama.

Habari zaidi zinasema kuwa mabadiliko yatakayofanyika endapo Lukuvi atakuwa Katibu Mkuu, yanaweza kuwa makubwa ya kwanza kufanywa na Rais Magufuli.

Hata hivyo, Lukuvi anakabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa baadhi ya viongozi ambao wako  karibu na Rais Magufuli ambao wanampigia chapuo Abdallah Bulembo, mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya chama hicho ili ateuliwe kuwa katibu mkuu wa CCM.

Ingawa Bulembo hana uzoefu mkubwa ndani ya chama hicho ukilinganisha na Lukuvi, bado anaweza kuteuliwa kushika nafasi hiyo kutokana na ukaribu na Rais Magufuli.

Bulembo anatajwa kuwa mmoja wa watu waliofanya kazi kubwa ya kufanikisha kampeni na hatimaye ushindi wa Rais Magufuli katika uchaguzi mkuu uliopita.

Taarifa kutoka ndani ya chama hicho zinasema, mara baada ya Rais Magufuli kukabidhiwa uenyekiti wa CCM, atamtangaza mmoja wa hao wawili – Lukuvi au Bulembo – kushika nafasi ya ukatibu mkuu wa chama chake.

Duru za siasa ndani ya CCM na Ikulu zinasema, mwenye uwezekano mkubwa wa kushika nafasi hiyo ni Lukuvi. Hiyo ni kama Rais Magufuli atatekeleza matakwa ya vigogo wa chama hicho na hivyo kulazimika kufumua baraza lake la mawaziri.

Tayari Kinana ambaye amewahi kutajwa na baadhi ya viongozi wa chama hicho kuwa ndiye alikuwa ‘mpika mizengwe’ mkuu wakati wa kumtafuta mgombea urais wa CCM, anaelezwa na watu wa karibu kuwa anataka  kuachia ngazi.

Mbali ya nafasi ya katibu mkuu, wengine wanaotajwa kuwa wanaweza kuondolewa baada ya Magufuli kukabidhiwa chama, ni pamoja na Mangula na Nape Nnauye anayeshikilia nafasi ya Katibu wa Halmashauri Kuu (NEC), Itikadi na Uenezi.

Nape amenukuliwa na gazeti moja la kila siku akisema, hatagombea tena nafasi za uongozi ndani ya chama chake.

Hata hivyo, Mangula ambaye amepata kuwa Katibu Mkuu wa CCM wakati Rais Mstaafu Benjamin Mkapa akiwa Mwenyekiti, hajatangaza kuachia ngazi, hivyo Rais Magufuli anaweza kumwachia aendelee akiona inampendeza.

Nafasi ya Nape, ambaye kwa sasa ni Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, inatarajiwa kushikwa na mmoja wa makada wapya wa chama hicho anayechipukia kwa sasa.

Mtoa taarifa wa gazeti hili amesema, awali nafasi ya Nape ilikuwa inapigiwa chapuo kushikwa na Christopher ole Sendeka, ambaye sasa amepewa nafasi ya kuwa Msemaji wa CCM.

Anasema, “kwa jumla Magufuli atakapokuwa mwenyekiti, atafumua sekretarieti nzima ya chama. Miongoni mwa ambao wanatajwa katika korido za chama kuwa wataondolewa katika nafasi zao, ni pamoja na Sendeka.”

Taarifa zinasema, mbunge huyo wa zamani wa Simanjiro mkoani Arusha, ataondolewa katika nafasi hiyo kutokana na kile kinachoitwa, “kuchemka katika baadhi ya maeneo nyeti.”

Madai kuwa Sendeka amekuwa akichemka katika baadhi ya maeneo, yalitolewa na Mangula katika mkutano wake na waandishi wa habari wiki iliyopita jijini Dar es Salaam.

Mangula alisema, Sendeka amekuwa akitoa taarifa ambazo siyo sahihi juu ya kung’atuka au kutong’atuka kwa Kikwete katika nafasi ya uenyekiti.

Tayari Magufuli amewaondosha zaidi ya nusu ya wateule wa Kikwete katika serikali yake; huku mabadiliko makubwa akiyafanya kwa wakuu wa wilaya ambapo zaidi ya nusu ya wale walioteuliwa na mtangulizi wake amewatupa nje.

Aidha, Magufuli ametupa karibu nusu ya wakuu wa mikoa walioteuliwa na Kikwete, maofisa wa Ikulu, makatibu wakuu serikalini na sasa rungu linanyemelea watumishi ndani ya chama.

Mtoa taarifa anasema, Rais Magufuli amejaribu mara kadhaa kutaka kufanyia mabadiliko makubwa baraza lake la mawaziri, lakini amekuwa akishauriwa kuachana na mpango huo ili kupisha mkutano wa Bunge la Bajeti unaomalizika kesho, Ijumaa mjini Dodoma.

Mabadiliko hayo alipanga kuyafanya wakati alipojaza nafasi ya Charles Kitwanga, aliyekuwa waziri wa mambo ya ndani, aliyetimuliwa kazi kwa madai ya ulevi.

error: Content is protected !!