January 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

MwanaHALISI mtaani kesho

Spread the love

GAZETI la MwanaHALISI limerudi. Tayari limechapwa. Kesho litakuwa mtaani nchi nzima. Anaandika Pendo Omary … (endelea).

Kwa mujibu wa Meneja Mkuu wa Hali Halisi Publishers (HHPL) inayomiliki na kuchapisha gazeti hilo, Robert Katula nakala moja ya gazeti itauzwa kwa Sh. 1,000.

“Tumeamua kuongeza kidogo bei kwa sababu mbalimbali lakini. Kubwa zaidi ni kupanda kwa kasi kwa gharama za uchapishaji,” amesema Katula.

Kurudi mtaani kwa gazeti hilo baada ya miaka mitatu na siku 35, kumekuja kutokana na uamuzi wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam wa kulifungulia gazeti hilo kama hatua ya kufuta tangazo la serikali Na. 258 la tarehe 27 Julai, 2012.

Tangazo hilo lilitolewa na Waziri wa Habari, Michezo na Utamaduni, Dk. Fenella Mukangara akitangaza kufunga gazeti hilo kwa muda usiojulikana kwa maelezo linachapisha makala za uchochezi.

Jaji Salvatory Bongole katika uamuzi wake wa kesi Na. 27 ya mwaka 2013 amesema waziri alikosea kuchukua uamuzi huo kwa kuwa hakutoa nafasi ya haki ya walalamikiwa kusikilizwa ambayo ni kinyume cha Sheria ya Magazeti ya mwaka 1976 kwa kutoifuata ipasavyo.

Akitoa ufafanuzi wa uamuzi wa Jaji Bongole, Wakili wa MwanaHALISI, Dk. Rugemeleza Nshala amesema gazeti liko huru kuchapishwa baada ya taratibu za kisheria baada ya uamuzi kukamilika.

“Jaji ametoa amri kwamba wahusika kutoingilia kamwe shughuli za uchapishaji wa gazeti la MwanaHALISI na shughuli za kampuni ya Hali Halisi Publishers. Zuio limetolewa dhidi ya vitendo vyovyote vya kuwanyanyasa na kuwatishia waleta maombi ikiwa ni pamoja na kutowafungia au kusimamisha uchapishaji wa gazeti la MwanaHALISI,” amesema Dk. Nshala.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Hali Halisi Publishers, Saed Kubenea amesema kwa muda wa miaka mitatu ambao gazeti lilifugwa kampuni yake imepata hasara hivyo kusababisha shughuli za kampuni hiyo kudolola.

“Kwa muda wa miaka mitatu, mwezi mmoja na siku tano kwa makadilio ya hasara tuliyopata ni Sh. 6.8 Bilioni. Kitu kinachoskitisha ni kwamba fedha hizo ni za walipa kodi wa nchi hii. Ni fedha ambazo zinapaswa kwenda kuboresha huduma za afya, elimu, kuchimba visima na kujenga barabara,” amesema Kubenea.

Aidha, Mhariri wa MwanaHALISI, Jabir Idrissa ameitaka serikali kutunga sheria ambayo itawalazimisha viongozi wake wanaoisababishia hasara kulipa hasara hizo badala ya fedha za walipa kodi kutumika.

“Waziri Fenella anataka kwenda bungeni kutunga sheria wakati ameshidwa kufuata sheria.  Zipo nchi ambazo hasara kama hizi anarudishiwa ofisa wa serikali aliyezisababisha,” amesema Jabir.

error: Content is protected !!