April 18, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Mwanadiplomasia Balozi Mahiga afariki dunia

Balozi Dk. Augustine Philip Mahiga

Spread the love

BALOZI Dk. Augustine Philip Mahiga, amefariki dunia, asubuhi hii ya leo, tarehe 1 Mei 2020, mjini Dodoma. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).

Mwanadiplomasia huyo mahiri ulimwenguni, anakuwa mbunge wa tatu kufariki dunia ndani ya kipindi cha wiki mbili. Wengine waliofariki dunia ndani ya kipindi hicho, ni Mchungaji Gertrude Pangalile Rwakatare, aliyekuwa mbunge wa Viti Maalum na Richard Ndassa, aliyekuwa mbunge wa Sumve. Wote ni kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Ndassa alifariki dunia juzi Alhamisi na amezikwa jana, nyumbani kwake Sumve, mkoani Mwanza. Lakini mwili wake, haukuingizwa bungeni kama utaratibu unavyotaka.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Gerson Msigwa, mkurugenzi wa mawasiliano ya Rais (Ikulu), Balozi Mahiga alifariki dunia baada ya kuugua ghafla akiwa nyumbani mkoani Dodoma; alifikishwa hospitali akiwa tayari amepoteza maisha.

Dk. Mahiga alikuwa mkoani Dodoma kushiriki mkutano wa Bunge la Bajeti. Dk. Mahiga alikuwa waziri wa Katiba na Sheria.

Katika salamu zake za pole kwa familia ya Balozi Mahiga na Spika wa Bunge, Job Ndugai, rais amesema, atamkumbuka Balozi Mahiga kwa uzalendo wake kwa nchi, pamoja na kuiwakilisha vyema Tanzania katika nyanja za kimataifa kwa miaka mingi.

Amesema, “Balozi Mahiga kuwa alikuwa mchapakazi, mwadilifu, mzalendo na mwanadiplomasia mahiri aliyeiwakilisha na kuipigania Tanzania, katika nyanja za kimataifa kwa miaka mingi.”

Dk. Mahiga alizaliwa 28 Agosti 1945, Tosamanganga, jimboni Kalenga, mkoani Iringa. Agosti mwaka huu, alikuwa anafikisha miaka 75.

Alikuwa mwanadiplomasia wa muda mrefu wa Tanzania na waziri wa mambo ya nje wa nchi hiyo kutoka mwa 2015 hadi 2019.

Amepata elimu yake ya msingi katika shule za Serikali enzi ya mkoloni na alihitimu darasa la Nane, muda mfupi baada ya uhuru.

Alikuwa mmoja wa wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), waliojitosa katika kinyang’anyiro cha urais, katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015. Hata hivyo, hakubahatika kuteuliwa na chama chake.

Safari ya elimu ya Dk. Mahiga ilikuwa ya umaskini uliopitiliza, alishindwa kuendelea na elimu ya sekondari kwa kutokuwa na fedha za kulipia mashuka na mablanketi hadi aliposaidiwa na msamaria mwema kutoka Shirika la Kennedy.

Aliendelea na masomo ya sekondari hapahapa nchini na mwaka 1968, alijiunga na Chuo Kikuu cha Afrika Mashariki (Dar es Salaam) na kuhitimu mwaka 1971, shahada ya Sanaa akibobea kwenye elimu.

Mwaka huohuo, Dk Mahiga alipata ufadhili na kuendelea na masomo ya juu katika Chuo Kikuu cha Toronto, nchini Canada ambako alihitimu Shahada ya Uzamili. Aliendelea na masomo ya Shahada ya Uzamivu (PhD) katika chuo hichohicho akijikita katika Uhusiano wa Kimataifa na kuhitimu mwaka 1975.

Mwaka huohuo 1975 (akiwa na miaka 30), Dk Mahiga alirejea nchini akiwa daktari wa falsafa kitaaluma na alipangiwa kazi ya kufundisha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam akiwa mhadhiri katika Idara ya Kimataifa na Ushirikiano wa Kikanda.

Balozi Dk. Augustino Mahiga (kushoto) enzi za uhai wake, akifurahia jambo na Mbunge wa Ubungo, Saed Kubenea

Alifanya kazi hiyo hadi mwaka 1977 alipohamishiwa katika Ofisi ya Rais kuwa Mkurugenzi wa Utafiti na Mafunzo na alidumu hapo akifanya kazi pamoja na Mwalimu Julius Nyerere hadi mwaka 1980.

Kati ya mwaka 1980 hadi 1983, Dk Mahiga alikuwa Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa (TISS). Nafasi hii aliitumikia kwa weledi mkubwa katika historia ya watu waliowahi kuitumikia. Anatajwa kuwa aliweza kuifahamu vizuri nchi na mifumo yake kwa mtizamo wa ndani na nje.

Akizungumzia msiba huo, mbunge wa Ubungo, Saed Kubenea amesema, taifa limempoteza mwanadiplomasia shupavu, jasiri na mahiri, katika kipindi ambacho alikuwa anahitajika sana.

“Balozi Dk. Mahiga, ameondoka katika kipindi ambacho taifa lilikuwa bado linamhitai mno. Uhusiano wetu na baadhi ya mataifa ya nje umevurugika na hivyo, mtu kama Dk. Mahiga alikuwa anahitajika katika kusaidia kurejesha uhusiano wa kimataifa na wenzetu,” ameeleza.

Amesema, “tunakwenda kwenye uchaguzi mkuu wa rais, wabunge na madiwani, Oktoba mwaka huu. Hekima za Dk. Mahiga, pamoja na kwamba hakuwa tena waziri wa mambo ya nje na uhusiano wa kimataifa, lakini uzoefu wake katika mambo ya kimataifa, ulikuwa na msaada mkubwa kwa serikali na taifa.”

Kubenea amesema, alimfahamu Dk. Mahiga kwa kumsoma, lakini alianza kuwa karibu naye sana, baada ya kujitosa kwenye mbio za urais mwaka 2015 na baadaye kuwa mbunge na diwani katika manipaa ya Kinondoni.

Anasema, “nilimfahamu Dk. Mahiga kama ni mtu wa kujisimamia na mara nyingi hafungwi na mitizamo au matakwa ya kikundi chake ikiwa mitizamo na matakwa hayo havina manufaa.”

Anasema, “tume ya Mabadiliko ya Katiba ilipotoa Rasimu ya Kwanza ya Katiba, Dk. Mahiga hakujali misimamo na matakwa ya chama chake katika kukosoa waraka ule. Wakati CCM ilikuwa inapinga kwa nguvu suala la Serikali tatu, yeye alieleza kuwa muundo huo umekuja kwa wakati muafaka. Alisisitiza kuwa Rasimu ile ya Kwanza imebeba majibu na kero zote za Muungano.”

Historia ya Dk. Mahiga katika nyanja za kimataifa, ni ndefu sana. Mwaka 1989 hadi 1992, Mahiga aliteuliwa kuwa mwakilishi wa kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Kimataifa (UN), akifanyia kazi zake Geneva – Uswisi.

Mwaka 1992 hadi 1994, Balozi Mahiga aliteuliwa kuwa Kiongozi (Mwakilishi) wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi duniani (UNHCR) mjini Monrovia, Liberia na huu ndiyo wakati aliponusurika kuuawa na Majeshi ya Rais Charles Taylor, kwenye vita ya wenyewe kwa wenyewe.

Kuna wakati akiwa katikati ya operesheni ya wakimbizi hapo Monrovia, Serikali ya Tanzania ilimteua kuwa Balozi na kumuongezea jukumu jingine zito.

Mwaka 1994–1998, Balozi Mahiga alihudumu akiwa Mratibu na Mkurugenzi Msaidizi wa Operesheni ya dharura ya Ukanda wa Maziwa Makuu akifanyia kazi hiyo kutokea Geneva–Uswisi na kati ya mwaka 1998 – 2002 aliteuliwa kuwa Kiongozi Mkuu (Mwakilishi) wa Shirika la Wakimbizi Duniani (UNHCR) huko mjini Delhi India, kabla ya kuteuliwa tena kuwa mwakilishi wa shirika hilo katika nchi za Italia, Malta na Jamhuri ya San Marino kati ya mwaka 2002 – 2003.

Balozi Mahiga amepata pia kuwa Balozi wa Kudumu wa Tanzania katika kipindi cha mwaka 2003 hadi 2010 na alishiriki kikamilifu katika mipango ya kimataifa pamoja na kusimamia mazungumzo ya kuanzishwa kwa Kamisheni ya Ujenzi wa Amani (mwaka 2005).

Pia alishiriki kwenye masuala ya maingiliano ya serikali mbalimbali na makundi yanayofanya kazi zisizo rasmi, maendeleo, amani, usalama na ujenzi wa ushirikiano wa uhakika kati ya Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika.

Balozi Mahiga aliirejesha heshima ya Tanzania hadi kuwa mojawapo ya nchi zilizounda Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na nchi yetu ilipopata heshima hiyo, yeye aliteuliwa kuwa mkuu wa ujumbe wa Tanzania katika Baraza hilo, hii ilikuwa ni mwaka 2005.

Dk. Mahiga anatajwa kuwa ameacha mke na watoto watatu.

error: Content is protected !!