Friday , 19 April 2024
Home Kitengo Maisha Elimu Mwanachuo aliyepasuliwa korodani na Polisi afichua mazito
ElimuMakala & UchambuziTangulizi

Mwanachuo aliyepasuliwa korodani na Polisi afichua mazito

Waren Lyimo
Spread the love

 

MWANACHUO wa Chuo Kikuu cha SAUT mkoani Mwanza, Warren Lyimo anayedaiwa kupigwa na kuteswa  na Polisi hadi kupasuka korodani, amesimulia mambo mazito na yakutisha katika mkasa huo. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Tukio la Warren kupigwa na kuteswa na Polisi, liliibuliwa kwa mara ya kwanza Gazeti hili Mei 17 na kuibua sintofahamu ambapo wananchi na wadau mbalimbali walilalamika.

Akizungumza na Raia Mwema katika mahojiano Maalum, ikiwa ni mara ya kwanza tangu alipopata  mkasa huo, Warren alidai alikamatwa na askari mgambo wawili ambao waliagizwa na Mkuu wa Kituo cha Polisi Buhongwa wilayani Nyamagana, Sajini Octovian Fabian, mwenye namba F.3728.

Alipofikishwa katika kituo hicho, Waren alitundikwa miguu juu kichwa chini huku akiwa amefungwa pingu kwa zaidi ya saa sita

Anasema mgambo mmoja akaingia ndani akachukua mti kubwa kama gogo, akaweka viti virefu na lile gogo alilipitisha katikati kama daraja na  akasema leo lazima niseme ukweli.

“Wakanipachika kwenye lile gogo kiasi naning’inia kichwa chini nikafungwa kama mbuzi anachunwa ngozi, miguu yangu ikiwa kwa mbele mikono kwa nyuma,  ona jinsi nilivyofungwa  ule mtindo wa adhabu kuna jina wanauita…. Nimesahau. Wakaanza kunipiga na rungu sehemu za nyayo, magoti na matakoni.

Waliendelea kunipiga mpaka yule askari mmoja alinipiga kwenye korodani  mpaka zikapasuka.

Kisa kizima kiko hivi

Mwanachuo huyo alianza simulizi kwa kujitambulisha kuwa anaitwa Warren Lyimo, mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha St Agustione (SAUT), mkoani Mwanza.

Anasema anakumbuka tarehe 15 Mei mwaka huu, majira ya saa mbili usiku  alipigiwa simu na Kaka yake Binamu anayeitwa Rudovic Lingia.

Anasema Rudocic alimpigia, akimtaka wakutane pahala kuna jambo anataka kumwambia na kuna pesa za matumizi ya hapo chuoni.

Anasema alilazimika kuchukua bodaboda ili kumuwahi Rudovic kwani lilikuwa  jambo la dharula.

“Mimi nilikuwa nakaa Nyamazobe, basi nikamuomba muendesha pikipiki ambaye tunafahamiana (anaitwa Sila), anipeleke pahala ambapo kaka Rudovic alikuwepo.

Flex Msanjo (kushoto) Baba Mdogo wa Warren Lyimo

Nilipofika pale nikaenda kwenye gari ambayo kaka Rudovic alikuwemo, nilipofika nikastuka askari mgambo ananikamata kwa kunikunja kwenye kola ya shati langu,” anasema Warren.

Kwa mujibu wa Warren, aliingizwa kwenye gari kwa nguvu  na yule dereva wa bodaboda alishindwa kufanya chochote kwasababu nilisha mwambia nakwenda kuonana na  binamu yangu, hivyo aliishia kuangalia tu kwani aliamini ni ugomvi wa ndugu.

Anasema alipokuwa kwenye gari, alimwuuliza kaka yake (Rudovic) kwamba kuna kitu gani, akamjibu kuwa Kompyuta yake mpakato (Laptop) imeibiwa, haionekani nyumbani.

Laptop hiyo aina ya HP ENVY 360 alipewa  zawadi na mkewe Mei 14 mwaka huu, siku ya kumbukizi yake ya kuzaliwa.

“Nikamuuliza unanihisi mimi ndio nimekuibia hiyo Laptop? ni muda gani mimi na wewe hatujaongea wala kuonana?, akajibu hajui,” anasema Waren.

Aliendelea kusema” Nikamwuuliza pale nyumbani  kuna watu wengi, kwanini unihisi mimi  maana hata Dada yupo, akajibu Dada tushadili naye, watoto wa pale nyumbani uliwauliza? akasema kwahiyo unawahisi watoto wangu.

Nikamwambia kwanini unakuja kunihisi mimi moja kwa moja bila uthibitisho wowote, akasema tuelekee kituo cha Polisi, itajulikana huko huko, nikamwambia sawa.

Muda huo nilikuwa najibu kwa kujiamini kwasababu nilikuwa na uhakika sijachukua hiyo Laptop yake.

Basi kaka akawasha gari kuelekea kituoni nikiwa nimevishwa pingu, nikiwa siti ya nyuma nimekaa na mgambo wawili. Kule mbele alikuwa yeye Rudovic na mke wake.

Anasema msafara ukaanza akipelekwa kwenye kituo cha Polisi cha Buhongwa akiwa chini ya ulinzi wa wanamgambo wawili.

“Tulipofika pale kituoni, baada ya kushuka tu, niliamriwa nipige magoti, nikaulizwa hiyo Laptop umeipeleka wapi,?” Nikawajibu Laptop sina na sina taarifa za kupotea kwa hiyo Laptop.

Wakasema unajifanya kiburi,  utatuambia tu usiku wa leo utakuwa mrefu sana kwako.

Mgambo mmoja akaingia ndani ya kituo  cha Polisi, alipotoka akachukua mti kubwa kama gogo hivi, akaweka viti virefu lile gogo likapita katikati kama daraja,  kisha akasema leo utasema.

Wakanipachika kwenye lile gogo kiasi kwamba nikawa naning’inia kichwa chini  miguu juu. Nikafungwa kama mbuzi anachunwa ngozi, miguu yangu ikiwa kwa mbele mikono kwa nyuma ona jinsi nilivyofungwa, ule mtindo wa adhabu kuna jina wanaiita…nikiukumbuka  nitasema.

Basi wakaanza kunipiga na rungu sehemu za nyayo, magoti, na matakoni.

Waliendelea kunipiga, wakanipiga hadi yule mgambo mmoja alinipiga mpaka kwenye korodani.

Nililia sana kwa uchungu mpaka nikawaomba waniitie kaka yangu (Rudovic) ambaye ndiye aliyenipeleka hapo kituoni na ambaye muda huo mimi nateswa ndani, alikuwa yupo nje ya kituo.

Alipokuja nikamwambia, kaka unauhakika kama mimi ndio nimekuibia Laptop yako, akasema atatuambia tu mahala ilipo.

Huku nikiwa nimening’inizwa nikamwambia, kaka Mwenyezi Mungu atalipa hivi vyote unavyonifanyia, akatoka nje ambako alikuwa anazungumza na mkuu wa kituo hicho aitwaye Fabian ambaye  muda wote huo alikuwa anakunywa bia hapo nje ya kituo.

Yule Mkuu wa Kituo Fabia, akatoa kule nje akaja akachukua lile rungu, akanipiga nalo kwa nguvu kwenye korodani, nilisikia maumivu makali sana, nikaona damu zimeanza kutoka.

Huku nikilia,  nilimwambi kama nilivyomwambia Rudovic na wale migambo  kuwa nimesema ukweli wangu kuwa hiyo Laptop sina.

Baada ya mateso ya kuning’inizwa na kupigwa kwa saa mbili hivi,wakanishusha wakidai kuwa wananipa dakika tano za kupumzika.

Kwa kuwa sikuweza kusimama, nilibwagwa chini kama mzigo wa mahindi nikiwa na pingu mikononi.

Dakika tano zilivyoisha walinirejesha kwenye ile adhabu, walinifunga tena huku wakinipiga na kuzidi kunitisha kuwa nitasema tu.

Kwa vile sauti ya mtu aliyekunywa Pombe naijua basi, nikatambua kuwa Mkuu wa Kituo Fabian na mgambo mmoja, walikuwa wamekunywa pombe na Kaka Rudovic hapo nje ya kituo

Basi ilipofika mida ya saa sita usiku, alinishusha kwa kunibwaga tena kama mzigo na kuniingiza kwenye gari ili niiende nao nyumbani kwangu ninakoishi, wakafanye ukaguzi kama hiyo Laptop nimeificha.

Wakanipandisha kwenye gari na wale wana mgambo wawili huku wakiendelea kunipiga makofi kichwani.

Wakiwa wanaendelea kunipiga, niliwaomba sana wasinipige, lakini walinijibu kuwa sina mamlaka yoyote kwa sababu mimi ni mtuhumiwa tu.

Njiani nikamwuliza Kaka Rudovic, umewapa taarifa ndugu zangu kama nimeshikwa na Polisi, akajibu niwape taarifa ya nini.

Nikamwomba awape taarifa ili nikipata shida wajue kuwa nipo mikononi mwa Polisi, akasema watajua mbele kwa mbele.

Nikamwuuliza tena kama amempigia simu Baba mdogo ili ajue, akasema nisimfundishe kazi, nikamwambia kwa mara ya pili kuwa Mwenyezi Mungu atakulipa.

Tupofika nyumbani kwangu, tulishuka nikiwa nimefungwa pingu nikawaelekeza namna ya kufungua milango, nikawaelekeza na chumba changu kwasababu hiyo ilikuwa mara ya kwanza kwa Kaka Rudovic kufika ninapoishi.

Waliingia ndani, walitafuta kila pahali hawakuipata, wakasema kwahiyo umetuweza sio, nikawajibu kuwa huo ndio ukweli, sijachukua Laptop yenu ningeifichia wapi.

Wakachukua bangi wakaniwekea mfukoni wakasema hiyo ndio itakuwa kesi yako.

Na walipotoka nje walipekuwa mpaka sehemu tunayoweka uchafu, wakajiridhisha hakuna kitu wakasema tunakwenda Polisi, zoezi la pili linakwenda kuanza, nikawauliza bado mnataka kuniadhibu?

Wakasema ndio na utatuambia tu ilipo hiyo Laptop, ndipo utakapopona.

Nikawambia nitaonyesha nini wakati sijui chochote, mgambo mmoja akasema we mtaje tu mtu yoyote unayemjua kama wewe hujaichukua.

Wakaniingiza tena kwenye gari, na wakati zoezi la upekuzi linaendelea yule mgambo mmoja alikwenda kununua zile pombe kali na akiwa kwenye gari alikuwa amelewa na alilala.

Mwenzake akamuamsha, akisema wewe mbona umelala wakati sherehe ndio kwanza inaanza, akajibu tukifika kituoni mtaniamsha.

Yule mwengine ambaye hanywi Pombe alitetea na mimi kuwa nimlaghai Rudovic ili aniingize kesi ya bangi.

Tulipofika Polisi, nje tulimkuta Afande Fabian akiwa anaendelea kunywa pombe huku akiuliza kuna mafanikio yoyote?

Basi, tulipofika tu wale mgambo wakasema huyu dogo tumemkuta na bangi chumbani kwake.

Afande Fabian akasema, tuiache kwanza ishu ya bangi, tudili na ishu ya Laptop kwanza iliyomfanya aletwe hapa.

Wakaningiza ndani, lile zoezi la kuning’inizwa miguu chini kichwa juu, liliendelea huku nikipigwa kama mara ya kwanza. Nililia sana, nikawambia sina Laptop.

Ilopofika mida ya saa nane usiku, wakasema huyu akapunzishwe, saa tisa tunaamsha naye, zoezi liendelee hadi aseme ukweli alipoficha hiyo Laptop.

Wakaniingiza mahabasu, sikuweza kupata usingizi nilikuwa nina maumivu mgongoni, sehemu za siri yaani mwili mzima ulikuwa unauma.

Bahati nzuri nikapata usingizi nikastuka kumeshapambazuka, akaja yule mgambo ambaye hanywi pombe, akaniambia nimpe namba ya Baba yangu mdogo ili ampe taarifa, aliniambia  watakuua hawa, nikampa.

Nikiwa mahabusu wale watu niliowakuta humo ndani, walinipa pole, wakasema dogo pole umepigwa kama jambazi sugu.

Wakaniuliza, hivi hawa waliokuwa hapa usiku wanaongea ni ndugu zako? nikawajibu kuwa yule mwanamme ni Kaka yangu Binamu Rudovic na mkewe na ndiyo walionileta hapa wakidai nimewaibia.

Mmoja wa mahabusu hao akasema, ndugu zako hawana huruma kabisa ‘kile kipigo ulichopigwa wewe inaonekana kuwa wametoa rushwa na angekuwa mtu mwingine hiyo, Laptop kama kaiba, angeirejesha.

Wakaniuliza kama nilishawahi kuwekwa mahabusu kabla ya tukio hilo, nikawajibu sijawahi.

Basi nikiwa na maumivu makali, nilijiegesha kwenye ukuta, mara Afande Fabian akaja akasema “wewe akamka wenzako wameamka wewe unalala hapa sio nyumbani kwako hapa.”

Mmoja wa mahabusu akamwambia Afande Fabian huoni huyu kijana ana hali mbaya, mmemtesa usiku mzima, mwacheni apunzike mwili wake wote una maaumivu,  akawajibu  msinifundishe kazi .

Basi muda huohuo, mahabusu sote tulitolewa tukapelekwa kusafisha vyoo, vilikuwa vinanuka sana.

Wale niliowakuta walinionea huruma, wakasema nipumzike muda huo siwezi chochote.

Afande Fabian akasema hakuna kupumzika, lakini wale mahabusu wakasema hapana tutamsaidia hawezi kufanya wakati huo mimi nikiwa nasinzia huku naugulia maumivu.

Usafi ulipoisha tukarejeshwa mahabusu, nikajiegesha maana nilikuwa nahisi kulala ndio kutanipunguzia maumivu.

Mara Fabian akapita na rungu, akilipigisha kwenye nondo akitaka niamke wale, mahabusu wakasema mwache apumzike, basi Afande Fabian akatamka kuwa aliyekuleta ndio atakayekutoa.

Ulipofika muda wa chai, wale mahabusu waliletewa chai na ndugu zao na kwa kuwa mimi hakuna mtu mwenye taarifa zangu, hakuna mtu aliyekuja zaidi ya wale walionileta.

Mahabusu wakanionea huruma wakawa wananipa chakula wakasema kula upate nguvu lakini sikuweza, wakawa wananisihi nisije kufa.

Baadaye akaja Rashid, namuita Uncle,  nahisi ni baada ya ile simu aliyopiga yule mgambo kwa Baba mdogo, akaja akafika mpaka pale mahabusu aliniita lakini nilishindwa hata kusimama kwa maumivu.

Wale mahabusu wakawa wana mhadithia hali halisi ilivyotokea, mateso niliyopata, mimi sikuweza tena kuzungumza.

Baada ya hapo nakumbuka nimeamka najistukia nipo Hospitalini  Bugando.

Sikumbuki chochote nakumbuka tu kuwa mtu wa mwisho kumuona ni Uncle Rashidi sikumbuki niliondokaje.Nilipoteza fahamu.

Nilishtuka nikiwa Bugando lakini niliambiwa nilipelekwa Hospitali ya kwanza ya wilaya walishindwa kunihuduma wakanikimbiza Bugando ambako nilikaa wiki mbili nikiwa ICU, sijitambui.

Nakumbuka nilikaa Bugando siku 23 nilifika tarehe 18 Mei 2022 na kutoka tarehe 10 Juni 2022.

Baada ya hapo alikuja jijini Dar es Salaam akipatiwa matibabu ya mazoezi.

Shukrani

Anasema anamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kumfanya aendelee kuwa hai kwa sababu alikuwa anahali mbaya kiasi kwamba amechungulia kaburi.

Anasema kuwa aliwahi kuitwa kwenye mahakama ya kijeshi kwa ajili ya kutoa maelezo juu ya kipigo alichopewa na mahakamani hapo aliambiwa kama anamtambua Fabian na kwamba ndio yeye aliyempiga.

Akasema kuwa alithibitisha kuwa ni yeye Octavian Fabian kuwa ndiye aliyempiga ambapo njiani alikutana na Rudovic, wakitoka mahakamani hapo akiwa na kaka yangu mwengine ambaye ni Afisa Ardhi kwenye Halmashauri ya Mwanza.

Warren anasema kwa sasa anaendelea vizuri kwa upande wa afya ya mwili lakini anakiri kuwa amepata athari kwenye ufahamu wake.

Nimeambiwa na madaktari kuwa ubongo wangu ‘umeshake’ kwa hiyo mental sijakaa vizuri, nimepoteza uwezo wa kumbukumbu, kitu naweza kukisema sasa hivi baada ya muda kidogo nasahau, ninakasirika haraka, nimekuwa mwepesi kupata msongo wa mawazo.

Ametoa rai kwa Jeshi la Polisi kufanya kazi zao za kiuweledi kwa sababu kutotoa haki kwao kunaweza kukaharibu maisha watu.

“Naomba Polisi watoe haki kwa uweledi kwa sababu tukio kama hili lililonipata mimi hata mtu wa mwingine anaweza kupata.  Mimi sijahusika na wezi, lakini napigwa, nateswa kulazimisha kukiri kosa. ”

Anasema hata Mwandishi wa Habari wa Raia Mwema Mwanza, anashauri Polisi wapewe mafunzo maalum ya kumjua mtu mwenye hatia wakati wa mahojiano ya kawaida.

Anasema mpaka sasa hajarejeshewa simu zake mbili moja Iphone 8 na nyingine Itel ndogo.

Kauli ya Baba Mlezi

Flex Msanjo, Baba mdogo wa Warren ambaye pia ni Baba mlezi, anasema alipewa taarifa ya msamaria mwema kuwa Warren yupo Polisi, nikamtuma mtu afuatilie akaenda akamkuta kijana anahali mbaya.

Alimkuta kijana hawezi hata kusimama, alikuwa akisaidiwa na watu waliokuwa mahabusu.

Kijana wetu alikuwa mwaka wa mwisho chuoni, lakini kwa kuwa amepoteza muda mwingi bila kuwepo chuoni, atalazimika krudia mwaka.

Kijana huyu alining’ing’iziwa muda mrefu, ubungo amepoteza kumbukumbu.

Nilimuandikia barua Waziri Mkuu akanijibu kuwa Serikali inalishughulikia, ingawa ni muda umepita hatujapata majibu hao waharifu wamechukuliwa hatua gani.

Polisi wachache wanalichafua jeshi la Polisi, lakini niombe Serikali itende haki kwenye tukio la huyu kijana.

Amesema Laptop ina thamani ya shilingi laki tatu lakini  matibabu yake  ni zaidi y ash milioni saba hadi sasa.

Hasara nyingine aliyopata kijana huyo ni kwamba tukio hilo limemharibia maisha kwani afya yake hajakaa sawa ilhali kesi yenyewe ya kusingiziwa.

Amelishukuru Gazeti la Raia Mwema kwa kupasa sauti ya kijana huyu hadi wadau wengine kama wa haki za  binadamu, wamejitokeza kumsaidia kwa namna moja ama  nyingine.

Kwa namna ya pekee, amewashukuru Madaktari, Wahudumu wa Afya wa Hospitali ya Bugando, kwa kupigania uhai wa Warren na uongozi wa Juu wa Jeshi la Polisi waliotoa ushirikiano kwenye suala hilo.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

KimataifaTangulizi

Mkuu wa majeshi Kenya afariki, Ruto atangaza maombolezo

Spread the loveRais wa Kenya, William Ruto ametangaza maombezo ya siku tatu...

Habari za SiasaTangulizi

Tanzania, Uturuki zanuia kukuza biashara, uwekezaji

Spread the loveSERIKALI za Tanzania na Uturuki zimekubaliana kuendeleza dhamira ya kuimarisha...

BiasharaMakala & Uchambuzi

Kanda ya Ziwa yaonyesha NMB inavyosaidia afya ya mama na mtoto

Spread the loveMafanikio inayozidi kupata Tanzania katika kupunguza vifo vya mama na...

Habari za SiasaTangulizi

Chadema yatangaza ruti awamu ya pili maandamano

Spread the love  CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimesema awamu ya...

error: Content is protected !!