MWAMUZI wa kati, Hery Sasii aliyechezesha mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara kati ya Simba dhidi ya KMC na kutoa penati iliyozua utata kwenye mchezo huo ni miongoni mwa waamuzi 17 walitunukiwa beji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Dunia (FIFA) leo tarehe 18 Desemba, 2020. Anaripoti Kelvin Mwaipungu, Dar es Salam … (endelea).
Katika mchezo huo ambao ulichezwa kwenye Uwanja wa Benjamini Mkapa jijini Dar es Salaam, Sasii alipatia Simba penati kwenye dakika ya 77, mara baada kutafsili kuwa mchezaji wa KMC, Hassan Kabunda alishika mpira mkononi wakati akiwa kwenye harakati za kuokoa mpira golini kwake.
Penati hiyo ilipigwa na mshambuliaji wa Simba, Medie Kagere na kumfunga golikipa imara, Juma Kaseja, bao hilo ndiyo lilikuwa pekee katika mchezo huo uliokuwa na ushindani mkubwa na kufanya Simba kuondoka kifua mbele kwa pointi tatu.
Taarifa kutoka ndani ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imeeleza kuwa FIFA ilituma orodha ya waamuzi 17 watakaotunukiwa beji hiyo kwa mwaka 2021, huku kati yao waamuzi wa kati wakiwa sita, waamuzi wasaidizi tisa na waamuzi watatu kutoka soka la ufukweni.
Waaamuzi wengine wakati waliopata beji hiyo ni Florent Zablon, Jonesia Rukyaa, Martin Saanya, Mfaume Nassoro na Ramadhani Kayoko.
Kwa upande wa waamuzi wasaidizi ni Abdulaziz Ally, Ferdinand Chacha, Frank Komba, Hellen Mduma, Janet Balama, Kassim Mpanga, Mbaraka Haule, Mohamed Mkono na Soud Lila, huku soka la ufukweni wakiwakilishwa na Geofrey Tumaini na Jackson Msilombo.
Beji hizo zitawasaidia waamuzi hao kuchezesha michuano ya kimataifa kwa ngazi ya klabu au timu za Taifa kama wakipata nafasi kwa kuwa wanatambulika na Fifa.
Leave a comment