MAHAKAMA ya Mkoa wa Kilimanjaro, imemhukumu kifungo cha mwaka mmoja mwamuzi wa mpira wa miguu, Safiel Mjema baada ya kumtia hatiani kwa kosa la kuomba na kupokea hongo ya Sh.120,000. Anaripoti Regina Mkonde, Kilimanjaro … (endelea).
Taarifa iliyotolewa jana Ijumaa tarehe 5 Juni 2020 na Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Mkoa wa Kilimanjaro, Fidelis Kalungura ilisema, hukumu hiyo ilitolewa tarehe 22 Mei 2020.
Alisema, hukumu hiyo ilikuwa ya kwenda jela mwaka mmoja au kulipa faini ya Sh. 500,000.
“Mtuhumiwa alishindwa kulipa faini hiyo hivyo alipelekwa jela kutumikia kifungo cha mwaka mmoja jela,” amesema Kalungura.
Alisema, mtuhumiwa huyo alifikishwa mahakamani hapo akikabiliwa na kosa la kuomba na kupokea hongo kiasi cha Sh.120,000 ili aweze kutoa upemndeleo kwa timu ya ‘New Generation’ iliyokuwa ikicheza na timu ya ‘La Familia’ kinyume cha kifungu cha 15 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Na.11/2007.
“Tunatoa rai kwa wanamichezo kutojihusisha na vitendo vya rushwa kwa namna yoyote ile kwani vinadumaza maendeleo ya michezo na ustawi wa jamii yetu,” alisema Kalungura
“Vilevile, tunatoa rai kwa wananchi wote kuendeleza mapambano dhidi ya rushwa kwa kutoa taarifa kwa ofisi yetu iliyoko karibu au kupitia namba yetu ya dharura 113,” aliongeza.
Leave a comment