July 5, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mwambene: Hakuna mwenye hati miliki ya nchi?

Mkurugenzi wa Idara Habari Maelezo, Assah Mwambene

Spread the love

UHUSIANO wa gazeti la MAWIO na serikali – Idara ya Habari Maelezo – ni wa mashaka. Ni bahati njema, tunafahamu kwa undani kinachosababisha uhusiano huo kuwa mbaya.

Ni msimamo wa gazeti letu na waandishi wake kutotaka kulamba viatu vya watawala. Kitendo hicho kimemuudhi mkurugunzi wa Maelezo, Bw. Assah Mwambene hadi kudiriki kutusingizia.

Hata hivyo, matatizo yetu na ofisi ya Mkurugenzi wa Maelezo, hayakuanza leo, jana wala juzi. Yalianza tangu wakati wa uhai wa gazeti la MwanaHALISI; ambalo waandishi wake wengi ndiyo wanaoandikia MAWIO hivi sasa.

Watumishi wa ofisi hii wamediriki kuongopa eti sisi hatutumii ofisi tuliyosajili kuwa ndiyo ofisi ya gazeti na kudai kuwa eti wamepata habari hizo kutoka kampuni ya mawakili ya Haki Law Chambers.

Kibaya zaidi, mtumishi mmoja wa Ofisi ya Habari (Maelezo) amediriki kunitamkia kwamba: “Tunajua gazeti lenu lina uhusiano na Kubenea (Saed) lakini hatuchukui hatua zozote kwa sababu, hayo ni maneno ya kusikia tu; kumbuka watu wanawaona na wanatuambia.”

Matamshi haya kutoka kwa mtumishi wa ofisi ya umma inayohusika na habari yanakera sana.

Kwanza, yanamaanisha kuwa serikali au watu fulani fulani serikalini, wameamua kuwapiga marufuku wandishi fulani fulani akiwamo Saed Kubenea.

Kwa maana nyingine ni kwamba, sisi tuliokuwa wandishi wa MwanaHALISI hatutakiwi kuandika habari au hatupaswi kumiliki gazeti. Tusichokifahamu sisi, ni nani hasa ndani ya serikali; au ni kundi gani la watu wakiwamo watumishi wa Idara ya Habari (Maelezo), walioamua sisi tusiandike habari.

Sisi wa MAWIO ndiyo sasa tunafahamu kama hatutakiwi kuandika habari ndiyo maana tunaambiwa kwamba ofisi ya Maelezo inajua gazeti hili lina uhusiano na Kubenea, kumbe ndiyo maana tunazushiwa kila siku.

Maelezo wanataka tushinde na kulala ofisini ili kila wakija hata bila taarifa watutukute. Maelezo wanataka wawakute waandishi akina Nyaronyo Mwita Kicheere, Josta Mwangulumbi, Jabir Idrissa, Yusufu Aboud na wengineo ofisini bila kuwakuta ofisini basi ofisi hiyo haitumiki.

Tungependa kumfahamisha Mkurugenzi wa Habari (Malezo) kwamba sheria ile mbaya kabisa kuwahi kutungwa na serikali ya Tanzania ili kuyanyorosha magazeti (The Newspaper Act of 1976 Cap ) haimruhusu Mkurugenzi huyo au bosi wake kuwapiga marufuku watu kuandika habari.

Tunachojua sisi ni kwamba lililofungiwa ni gazeti la MwanaHALISI na siyo wandishi wake. Hivyo Maelezo iache kutuandama na kutuzushia. Nyaronyo, kubenea, Jabir, Yusufu, Mwangulumbi na wengine hawakupigwa marufuku ya kuandika; tafadhili waachwe wandike.

Hata kama Maelezo hawatutaki basi wao watuvumilie tu kama sisi tunavyowavumilia. Kuwatii na kuwapenda hata kama wengine wetu wanadhani kwamba hawastahili kukalia ofisi ile kuu. Na tungependa kuwapasha Maelezo kwamba wajitokeze hadharani kusema hawataki tuandike habari.

Pili, Malezo tumewapelekea maombi ya kutaka kugeuza gazeti la MSETO kutoka kuwa gazeti la habari na sasa kuwa gazeti la habari na michezo kama yalivyo magazeti ya Nipashe; Mwananchi; Mtanzania; Jambo leo na habari leo lakini ofisi hii kwa sababu inazozijua yenyewe imegoma kabisa kutoa majibu kama ndiyo au hapa.

Maelezo watoe tu majibu kama ni kukataa au kukubali. Wanakaa kimya miaka miwili sasa kwa nini? Je wangekuwa walioomba kufanya hivyo ni wengine kama Jambo Leo, Mtanzania au Habari leo, Maelezo ingekuwa kimya hadi leo? Hatutaki ubaguzi hapa na huenda tukaenda mahakamani kumlazimisha Mkurugenzi huyu kufanya kazi yake.

Maelezo pia wanadai kuambiwa na wanasheria waliopo gorofa ya pili ya jengo la Mwembechai Plaza kwamba eti sisi hatutumii ofisi ile. Kibaya zaidi Haki Law Chambers wanafahamika kwamba ni mawakili wa kampuni ambayo mmoja wa wamikiki wake, ni mkurugenzi wa MAELEZO katika shauri lake dhidi ya MAWIO. Sasa iweje leo MAELEZO iwatarajie kutoa habari sahihi kuhusu sisi?

Hebu tuache usanii katika hili. Maelezo wanapaswa kufahamu kwamba sisi ni walipa kodi kama raia wengine na kwamba kodi yetu ndiyo inayotumika kuwalipa mishahara minono wanayopata na kwa hivyo wasiukate mkono unaowalisha.

Nimalize kwa kusema kwamba tunao uhakika wa uraia wetu na hasa mimi Nyaronyo Mwita Kicheere ambaye nalifahamu kaburi la babu wa babu yangu kwa hiyo hoja ya uraia hapa haipo. Tutekeleza wajibu na siyo kuzushiana.

Makala hii imeandikwa na Nyaronyo Mwita Kicheere

error: Content is protected !!