June 19, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Mwalimu Nyerere, Mwinyi vinara wa kusaini unyongaji

Spread the love

TAKWIMU zilizotolewa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), kuhusiana na utekelezwaji wa adhabu ya kifo hapa nchini, zinaonyesha kuwa ni rais wa awamu ya kwanza na ya pili pekee ndiyo waliokubali kusaini kunyongwa kwa baadhi ya watu waliohukumiwa adhabu hiyo, anaandika Charles William.

Takwimu hizo zinafafanua zaidi kuwa, katika kipindi cha utawala wa awamu ya kwanza na ya pili chini ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere na baadaye Alhaji Ali Hassan Mwinyi, jumla ya watu 72 walinyongwa baada ya marais hao kutia saini kwa nyakati tofauti tofauti.

Adhabu ya kunyongwa mpaka kufa, imekuwa ikitekelezwa hapa nchini tangu mwaka 1945 wakati wa ukoloni, kwa sasa utaratibu wa adhabu hiyo ni kuwa Mahakama Kuu au Mahakama ya Rufaa inapotoa hukumu hiyo, mtu hunyongwa baada ya rais aliyepo madarani kusaini.

“Ni miaka 22 sasa imepita, nchi yetu haijatekeleza adhabu ya kifo licha ya watu wengi kuhukumiwa kwani kwa mujibu wa sheria zetu Rais ndiye mwenye mamlaka ya kusaini ili kuidhinisha mtu kunyongwa. Inaonekana hata wao wanaogopa kufanya hivyo ili mtu afe,” amesema Dk. Hellen Kijo-Bisimba, Mkurugenzi wa LHRC.

Kwa mujibu wa sheria za Tanzania mtu anaweza kuhukumiwa adhabu ya kunyongwa mpaka kufa iwapo atatiwa hatiani kwa kosa lolote kati ya haya matatu:- Kufanya mauaji ya kukusudia, kosa la uhaini na kosa la ugaidi.

Kumbukumbu zinaonyesha kuwa Benjamin Mkapa, Rais wa awamu ya tatu na Jakaya Kikwete, Rais wa awamu ya nne katika vipindi vya utawala wao, hawajawahi kuidhinisha utekelezwaji wa adhabu ya kifo kwa mtu yoyote.

Rais John Magufuli wa awamu ya tano ambaye ana miezi 11 sasa tangu aingie madarakani, ana mzigo wa watu 472 wakiwemo wanaume 452 na wanawake 20 wanaosubiri utekelezwaji wa adhabu hiyo kwa idhini yake, ingawa jumla ya watu 244 wamekata rufaa ili kujinusuru na adhabu hiyo.

Adhabu ya kifo imekuwa ikizua mvutano mkali baina ya mataifa mbalimbali duniani huku baadhi ya mataifa yakiifuta na wanaharakati wa Haki za Binadamu wakishikia bango kuondolewa kwa hukumu hiyo kwa madai kuwa ni ya kikatili na kigaidi.

Jumla ya nchi 140 duniani zikiwemo 17 za bara la Afrika tayari zimeshaifuta adhabu hiyo kwa watu wanaopatikana na hatia ya makosa mbalimbali.

error: Content is protected !!