November 27, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mwalimu alalamika kunyimwa ruhusa ya kuuguza mama yake

Barua ya Afisa ya Elimu kupinga uhamisho wa Mwalimu Rose Mgulambwa

Spread the love

MWALIMU wa shule ya msingi Chazungwa, wilayani Mpwapwa, Dodoma, Rose Mgulambwa amesema anashangazwa na Afisa Elimu Msingi, Mery Chakupewa kwa kumnyima uhamisho kwa ajili ya kumuhudumia mama yake mzazi ambaye ni mgonjwa. Anaripoti Danson Kaijage, Mpwapwa … (endelea).

Mwalimu Rose, ameomba uhamisho kutoka Mpwapwa kwenda katika shule za Dodoma ili aweze kupata nafasi ya kumuhudumia mama yake mzazi ambaye anasumbuliwa na magonjwa mbalimbali.

Anadia kuwa amenyimwa ruhusa hiyo kwa kupewa masharti ya kutafuta mwalimu mwingine kutoka Dodoma ili aende katika iwlaya ya Mpwapwa ili naye apate nafasi ya kuhamia huko aweze kumuuguza mama yake mzazi ambaye anasumbuliwa na maradhi mbalimbali.

Akizungumza na MwanaHALISI Online, Mwalimu Rose amesema kuwa kutokana na ugonjwa wa mama yake amekuwa akiomba barua ya uhamisho ili aweze kuwa karibu na mama yake ambaye ni mgonjwa.

“Baba yangu ambaye alikuwa mume wa mama yangu alishafariki na mama yangu kwa sasa anaumwa sana, kutokana na hali hiyo niliomba uhamisho nitoke shule ya msingi ya Chachazungwa na kwenda shule yoyote ya Dodoma ili niweze kumuhudumia mama yangu.

“Niliamini kuwa nikiomba ruhusu nitapewa kwa kuzingatia maagizo ya Waziri wa  Utumishi na Utawala Bora, George Mkuchika kuwa kila mtu ambaye anataka kuhama kwa sababu za msingi anaweza kuhama.

“Kimsingi mama yangu anaumwa, na sina msaada wowote wa kumsaidia mama yangu msaada pekee ni kuomba ruhusa lakini kinachotokea ni afisa elimu Msingi Wilaya ya Mpwapwa, Mery Chakupewa amekuwa akinikatalia na kudai kuwa nitafute wa kubadilishana naye.

“Mimi nitampata wapi mwalimu wa kubadilishana naye ninachojua ni kuwa anayeweza kutafuta mwalimu mwingine ni afisa utumishi na siyo mimi,” ameeleza Mwalimu Rose.

Alipotafutwa afisa elimu Msingi Mery Chakupewa ili aweze kupewa ufafanuzi ni kwanini amekuwa akimnyima ruhusa alisema kuwa hama muda mzuri wa kuzungumzia suala hilo.

Alipotafutwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mpwapwa, Paul Mamba ili aweze kuelezea changamoto ambayo mwalimu anakumbana nayo amesema kuwa ofisi yake haijapokea barua yake na wala hajapata maombi ya mwalimu huyo.

“Huyo mwalimu kishafika ofisini kwangu? au amefika wapi walimu wote ni wangu na wapo ofisini kwangu sasa sijapata taarifa zake ofisi yangu ipo wazi na kwa watumishi wote,” amesema Mkurugenzi Mamba.

error: Content is protected !!