January 19, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mwalimu ainanga CCM

Naibu Katibu Mkuu Chadema Zanzibar, Salim Mwalim

Spread the love

NAIBU Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Zanzibar, Salim Mwalimu, amekivaa Chama cha Mapinduzi (CCM), akisema kinatumia vibaya rasiliamali za taifa. Anaandika Moses Mseti, Mwanza … (endelea).

Mwalimu alitoa kauli hiyo jana, wakati wa mkutano wa watia nia ubunge zaidi ya 70 kutoka Geita, Kagera na Mwanza, uliofanyika katika hoteli ya Kingdom jijini hapa.

Amesema CCM imekuwa ikitumia vibaya rasilimali za taifa ikiwemo kubinafishisha mbunga za wanyama pamoja na migodi lakini wamekuwa wakishindwa kuwatatulia wananchi kero zinazowakabili.

Mwalimu amesema serikali ya CCM imeshindwa kutambua na kuwajali wananchi wake ambao wanawapa dhamana ya kuingia Ikuru na wakati mwingine wamekuwa wakijilimbikizia mali za Watanzania bila ya huruma.

“Watanzania wamekuwa wakitafuta Tanzania mpya kwa muda mrefu sana kutoka kwa CCM na walidhani wakiwachagua viongozi wa chama hicho wataipata lakini mpaka sasa imeshindikana.

“Pia katika uchaguzi wa mwaka huu, tukishindwa sio kama tumeshindwa Chadema, watakuwa wameshindwa wananchi ambao ni walalahoi walikata tamaa na CCM pamoja na polisi wanaolipwa mshahara mdogo,” amesema.

Mwalimu alitoa rai kwa viongozi wa mikoa kuacha tabia ya kuwakatisha tamaa, wabunge hao watarajiwa pale ambapo wanapofanya kazi za kukijenga chama kwa kutumia usafiri wa helikopta.

Naye Makamu Mwenyekiti Chadema kanda ya Ziwa Victoria, Rodrick Kabangira, amesema serikali ya CCM imeshindwa kuwasimamia wawekezaji nchini kulipa kodi, kitendo kinachosababisha uchumi kuyumba.

Kabangira amesema kushuka kwa uchumi wa taifa inatokana na serikali kushindwa kuwabana wawekezaji na badala yake inajenga viwanda vingi ambavyo hawalipi kodi.

“Chadema kinalenga kwamba ifikapo 2025, Watanzania wawe wanajisimamia kwa mali zao na kupata huduma ya afya na miundombinu ya barabara inayopitika kila kona ya nchi,” amesema Kabangira.

error: Content is protected !!