June 26, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mwakyemba naye atumia makundi kusaka urais

Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dk. Herrison Mwakyembe (kushoto) na Rais wa Shirikisho la Mchezo wa Bao Tanzania (SHIMBATA), Monday Likwepa

Spread the love

KAMA ambayo baadhi ya makada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), wanatumia makundi ya kijamii kujipigia debe la urais wakidai kuombwa kugombea, Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk. Herrison Mwakyembe, naye ameingia kwenye mbio hizo. Anaandika Sarafina Lidwino … (endelea).

Hatua hiyo inaendelea huku makada sita wa chama hicho wakiwa bado hawajaondolewa katika kifungo cha kudaiwa kuanza kampeni mapemba kabla ya wakati.

Miongoni mwa waliofungiwa ni Edward Lowassa ambaye chama kimemshupalia zaidi kikimtaka azuie pia makundi yaliyokuwa yakienda kwake kwa madai ya kumshawishi agombee urais.

Wakati hali ikiwa hivyo, Dk. Mwakyembe naye katika maadhimisho ya fainali za mchezo wa bao jijini Dar es Salaam leo, ameonekana kupitia upenyo ule ule wa kudai kuombwa na makundi ili agombee urais Oktoba mwaka huu.

Mchezo huo, umechezwa chini ya Shirikisho la Mchezo wa Bao Tanzani (SHIMBATA) ukiwashirikisha baadhi ya wazee toka wilaya zote za mkoa wa Dar, ambao pia waliwahi kucheza mchezo huo na hayati Julius Nyerere.

Katika fainali hiyo, Dk. Mwakyembe ndiye aliandaliwa kuwa mgeni rasmi, akiwa mlezi msaidizi wa SHIMBATA, ambapo baada ya kukagua mchezo huo, wazee hao  wakamsomea risala ya kumpamba.

Wamesema kuwa, lengo la kumuandikia risala hilo ni kumtaka achukue fomu ya urais.

“Sisi wazee wa mkoa wa Dar, baada ya kuwaangalia na kuwachunguza watendaji wote wa Serikali, tumebaini kuwa Mwakyembe- mbunge wa Jimbo la Kyela, anastahili kuwania nafasi ya urais kwa sifa alizo nazo,” wamesema.

Dk.Mwakyembe baada ya kupata maombi hayo aliwashukuru kwa mtazamo wao na kuwaahidi kulifanyia kazi.

“Asanteni sana kwa sifa hizo, kama ni za kweli, nimezipokea, naombeni muda wa kutafakari hilo kisha nitawapatia jibu. Ila kuhusu mchezo huu mliouonyesha hapa nimeupenda kwani ni njia pekee ya kudumisha utamaduni wetu na niwaahidi kuwasaidia katika hilo,” amesema Mwakyembe.

error: Content is protected !!