HASSAN Mwakinyo, bondia raia wa Tanzania, amepanda katika viwango vya ubora duniani kutoka nafasi ya 13 hadi 11. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Mwakinyo amepanda kwenye viwango hivyo takribani siku nne zimepita tangu amtwangwe kwa TKO, Julius Indogo kutoka Namibia.
Pambano hilo lililokuwa la raundi 12, liliishia raundi ya nne baada ya Indogo kushindwa kumudu makonde ya Mwakinyo aliyetetea ubingwa wake wa Afrika (ABU) uzito wa Super Welter.
Vitasa hivyo vilipigwa usiku wa kuamkia Jumamosi tarehe 4 Septemba 2021, katika ukumbi Ubungo Plaza mkoani Dar es Salaam.
Viwango vilivyotolewa leo asubuhi Jumatano, tarehe 8 Septemba 2021, vinamuonesha Mwakinyo akiwa amepanda nafasi mbili zaidi kutoka 13 hadi 11.
Katika viwango vilivyotoka jumamozi mara baada ya pambano hilo la Mwakinyo na Indogo, lilimpandisha kutoka nafasi ya 24 hadi 13 huku akiendelea kushika nafasi ya kwanza barani Afrika.
Nafasi ya kwanza duniani inashikwa na Jermell Charlo wa Marekani, nafasi ya pili ikishikwa na Brian Carlos Castano wa Argentina.
Katika ukurasa wake wa kijamii wa Twitter, Mwakinyo ameandika “Alhamdulilah Guys rank imesoma tena kutoka nafasi ya 13 mpaka 11 Now I see pounds for pounds Ranking. Tunaitaka nafasi Ya Jermell Charlo.”
Leave a comment