MWAKILISHI Mteule wa Pandani kupitia Chama cha ACT-Wazalendo, Abubakar Khamis Bakar (69) amefariki dunia usiku wa kuamkia leo Jumatano tarehe 11 Novemba 2020, akiwa nyumbani kwake Mbweni visiwani Unguja, Zanzibar. Anaripoti Mwandishi Wetu…(endelea).
Taarifa hiyo imetolewa na Katibu wa Idara ya Uenezi, Habari na Mawasiliano kwa Umma, Salim Bimani wakati anazungumza na MwanaHALISI Online kwa simu.
Bimani amesema, mwili wa Bakar aliyezaliwa tarehe 2 Novemba 1951 utazikwa jioni ya leo katika makaburi ya familia yake yaliyopo maeneo ya Kiyanga visiwani humo.
“Inaonekana alifariki nyumbani kwake Mbweni Unguja saa saba. Mazishi yatafanyika leo jioni katika makaburi ya familia yake maeneo ya Kiyanga,” amesema Bimani.
Kuhusu chanzo cha kifo hicho, Bimani amesema hadi sasa hakuna taarifa rasmi juu ya chanzo chake ila anahisi itakuwa ni shinikizo la moyo.
“Chanzo cha kifo chake hadi sasa hatujui rasmi kwa kuwa alikuwa mzima, nahisi alipata shinikizo la moyo,” amesema Bimani.
Awali, taarifa za kifo hicho zilitolewa na Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe kupitia ukurasa wake wa Twitter.
Zitto amesema kifo hicho ni pigo kwa chama chake kwa kuwa marehemu Bakar alikuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya ACT-Wazalendo pamoja na Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili.
“Kwa uchungu mkubwa. nawajulisha kuhusu msiba mkubwa tuliopata wa Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama na Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili Maalim Abubakar Khamis Bakar,” ameandika Zitto.
Leave a comment