ALIYEKUWA Mkurugenzi wa Manispaa ya Temeke, mkoani Dar es Salaam, Lusubilo Mwakabibi, amefunguliwa kesi ya uhujumu uchumi, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).
Leo Ijumaa, tarehe 20 Agosti 2021, Mwakabibi na mwenzake, Edward Haule, wamesomewa mashtaka mawili yaliyomo katika kesi hiyo na Wakili Serikali Mwandamizi, Ester Martin, mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi wa mahakama hiyo, Evodia Kyaruzi.
Wakili Martin aliyekuwa anasaidiana na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Mkunde Mshanga, waliwasomea washtakiwa hao mashtaka ya matumizi mabaya ya madaraka na utumishi wa umma.
Mbele ya Hakimu Kyaruzi, Wakili Martin alidai kwamba, Mwakabibi na mwenzake walitenda kosa hilo kati ya Machi 2020 na Machi 2021, mkoani Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa mashtaka hayo, Mwakabibi anadaiwa kutenda makosa hayo alipokuwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Temeke na Mratibu wa Mradi wa Uendelezaji Jiji la Dar es Salaam (DMDP).
Anadaiwa kutumia madaraka yake vibaya kwa makusudi, kwenda kinyume cha sheria ya ardhi.
Kufuatia uamuzi wake wa kuelekeza ujenzi wa stendi ya mabasi ya Buza, katika kiwanja ambacho ni mali ya Dayosisi ya Kanisa la Anglikana bila kupata ruhusa.
Baada ya washtakiwa hao kusomewa mashtaka, Hakimu Kyaruzi alitoa masharti ya dhamana ambayo, kila mshtakiwa alitakiwa kuwasilisha fedha taslimu Sh. 10 milioni, au mali isiyohamishika yenye thamani hiyo.
Pia kuwa na wadhamini wawili watakaosaini bondi ya Sh. 10 milioni.
Hata hivyo, Mwakabibi na mwenzake walishindwa kutimiza masharti ya dhamana hiyo.
Mahakama hiyo imewapa masharti washtakiwa hao, kuwasilisha mahakamani hapo hati ya kusafiria pamoja na kutosafiri nje ya mkoa wa Dar es Salaam, bila kibali chake.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi tarehe 2 Septemba mwaka huu.
Leave a comment