Wednesday , 29 March 2023
Home Gazeti Habari Mchanganyiko Mwaka 2020 waondoka na waandishi hawa  
Habari Mchanganyiko

Mwaka 2020 waondoka na waandishi hawa  

Spread the love

MWAKA 2020 unahitimishwa siku chache zijazo huku ukiwa umeshuhudia Tasnia ya Habari nchini Tanzania, ikiwapoteza wanataaluma wenzao zaidi ya kumi. Anaripoti Faki Sosi, Dar es Salaam … (endelea).

Wakati mwaka 2020 ukiacha machungu na simanzi katika tasnia hiyo kwa kuondokewa na wanahabari, 2019 pia uliacha majonzi kwa wanahabari kuwapoteza waasisi na wamiliki wa vituo vya habari.

Waasisi wa vyombo vya habari waliopoteza maisha 2019 ni, DK. Reginard Mengi, aliyekuwa Mmiliki wa Kampuni za IPP Media yenye magezeti ya Nipashe, The Guardian, Televisheni ya ITV, EATV, Radio one na  Capital Radio.

Na Ruge Mutahaba, aliyekuwa Mkurugenzi wa Clouds Media lakini mwaka huu utakaomalizika siku chache zijazo, umekuwa zamu ya waandishi wa habari ambapo kwa nyakati tofauti, walihitimisha safari zao hapa duniani.

Pius Yalula

Pius Yalula, aliyekuwa mwandishi wa habari wa Televisheni ya Mtandao ya Dar 24 afariki dunia tarehe 27  Januari 2020 baada ya kuugua kwa muda mfupi. 

Deogratius David

Tasnia ya habari ilianza kupata pigo tarehe 27 Januari 2020, baada ya kupata taarifa ya kifo cha aliyekuwa mwandishi wa habari wa kujitolewa wa Shirika la Habari Tanzania (TBC), Deogratius David.

Taarifa ya kifo hicho ilitolewa na Kamishna Msaidizi wa Polisi Mkoa wa Ilala, Janeth Magomi, baada ya mwili wa David kukutwa chumbani kwake maeneo ya Vingunguti Mji Mpya wilayani Ilala jijini Dar es Salaam huku ukiwa umeharibika vibaya.

Mwili wa mwanahabari huyo, uligundulika siku tatu baada ya majirani zake kutoa taarifa polisi kutokana na mwili kuanza kutoa harufu.

Majirani hao waliriripoti polisi baada ya kutokumuona David kwa muda wa siku tatu sambamba na kusikia harufu hiyo.

Wakishirikiana na Jeshi la Polisi, walivunja mlango wa chumba alichokuwa akiishia David kisha wakaukuta mwili wake ukiwa kifudifudi kitandani kwake. Mwili wa David, ulizikwa nyumbani kwao Sumbawanga mkoani Rukwa.

Asha Mhaji

Tarehe 25 Machi 2020, aliyekuwa mwandishi mwandamizi wa habari za michezo wa Kampuni ya New Habari (2006) Limited inayozalisha magazeti ya Dimba, Bingwa, Mtanzania na Rai, Asha Mhaji alifariki dunia katika hosptali ya Hindu Mandal, Dar es Salaam alipokuwa amelazwa kwa matibabu.

Enzi za uhai wake, Asha aliwahi kuwa Msemaji wa Klabu ya Simba na mwili wake ulizikwa jijini Dar es Salaam.

Marine Hassan Marine

Moja ya watangazaji maarufu wa muda mrefu akitumikia Shirikala Utangazaji Tanzania (TBC), Marine Hassan Marine alihitimisha safari ya maisha yake hapa duniani alfajili ya tarehe 1 Aprili 2020 jijini Dar es Salaam baada ya kuugua ghafla.

Marine alikuwa mjuzi wa utangazaji na alitumia vyema sauti yake na moja ya vipindi alivyokuwa akivitangaza ni ‘Safari ya Dodoma’ ya Serikali kuhamia makao makuu ya nchi jijini Dodoma kutoka Dar es Salaam.

Mwili wa Marine ulizikwa nyumbani kwao Unguja visiwani Zanzibar tarehe 2 Aprili 2020.

Lutengano Haonga

Wakati TBC wakiwa hawajapoa kwa kumtoteza, Marine, siku kumi baadaye yaano tarehe 11 Aprili 2020, mtangazaji wake mwandamizi Lutengano Haonga alifariki dunia jioni ya tarehe 10 Aprili 2020 akiwa  Hospitali ya Mloganzila jijini Dar es Salaam.

Eliya Mbonea

Tasnia hiyo ya habari,ikiwa haijapoa kwa kumpoteza Marine, siku tano baadaye yani tarehe 6 Aprili 2020, Eliya Mbonea, aliyekuwa mwandishi wa habari wa Kampuni ya New Habari inayomiliki magazeti ya Mtanzania, Dimba, Rai na The African alifariki dunia.

Mbonea alifariki dunia Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) alikokuwa anapatiwa matibabu kwa zaidi ya wiki tatu, baada kusumbuliwa na uvimbe tumboni.

Marehemu Mbonea alianza kusumbuliwa na tatizo hilo tangu Oktoba 2019. Kabla umauti kumfika, alianza kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Kanda ya Kaskazini (KCMC).

Kwa mujibu wa familia ya marehemu Mbonea, chanzo cha kifo chake kilikuwa ni tatizo la kuishiwa damu kutokana na uvimbe huo. Mwili wa Mbonea ulizikwa jijini Arusha.

Omary Fungo

Moja ya wapiga picha maarufu nchini wa muda mrefu, Omar Fungo alifariki dunia tarehe 4 Mei 2020 akiwa Hospitali ya Malawi iliyopo Kiwalani jijini Dar es Salaam alipokuwa akipatiwa matibabu.

Enzi za uhai wake, alifanya kazi Kampuni ya IPP na hadi mauti yanamfika alikuwa mpiga picha wa Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) wachapishaji wa magazeti ya Mwananchi, MwanaSpoti na The Citizen.

Mwili wa Fungo ulizikwa tarehe 5 Mei 2020 nyumbani kwake Kiwalani.

Manuel Kaminyoge.

Aliyekuwa mwandishi wa habari wa kujitegemea katika Kituo cha runinga cha EATV mkoani Songwe, Manuel Kaminyoge, alifariki dunia tarehe 12 Juni 2020 katika Hospitali ya Ikonda mkoani Iringa alikokuwa anapatiwa matibabu.

Kaminyoge alifariki dunia siku kadhaa baada ya kupata ajali ya gari mkoani Songwe, ambapo alipewa rufaa kutoka mkoani humo hadi Iringa kwa ajili ya matibabu zaidi.

Raphael Kibiriti

Tasnia ya habari nchini Tanzania iliendelea kuwapoteza waandishi baada ya mwandishi mwandamizi wa The Gurdian Limited, Raphael Kibiriti alifariki dunia tarehe 2 Julai 2020 baada ya kuugua kwa kipindi Fulani na mwili wake, ulizikwa Wazo jijini Dar es Salaam.

Agnes Almas

Tarehe 3 Septemba 2020, moja ya watangazaji waliokuwa wakichipukie kwenye tasnia ya habari akitangaza Kituo cha Runinga cha ITV, Agnes Almas alifariki dunia baada ya kuugua ghafla.

Agnes alifariki dunia akiwa njiani kuelekea Hospitali ya Amana jijini Dar es Salaam, baada ya kujisikia vibaya alipokuwa nyumbani kwake akijiandaa kwenda kazini.

Mwili wa Agnes uliagwa tarehe 5 Septemba 2020, katika Kanisa la St. Nicholaus, Ilala jijini Dar es Salaam.

Baada ya mwili huo kuagwa ulisafirishwa kuelekea nyumbani kwao Bombo mkoani Tanga, kisha ulizikwa tarehe 6 Septemba 2020.

Elisha Elia

Elisha Elia, aliyekuwa mwandishi na mtangazaji wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), alifariki dunia tarehe 24 Oktoba 2020, katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), alikokuwa anapatiwa matibabu, baada ya kuugua akiwa mikutano ya kampeni ya mgombea urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais John Magufuli.

Taarifa ya kifo cha Elia ilitolewa na Mkurugenzi  Mkuu wa TBC, Dk. Ayub Rioba.

 

Elisha Elia

Elisha atakumbukwa na kipindi alichokitangaza kwa umaarufu mkubwa ‘Kishindo cha JPM’ kikielezea utekelezaji wa miradi mbalimbali ya Serikaliochini ya Rais John Pombe Magufuli.

Mwili wa mtangazaji huyo uliagwa na mamia ya watu wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Abubakar Kunenge, tarehe  26 Oktoba 2020 kisha ulisafirishwa hadi nyumbani kwao mkoani Mbeya kwa maziko yaliyofanyika tarehe 27 Oktoba 2020.

Frank Kimboi 

Tasnia ya habari iliendelea kuwapoteza wenzao ambapo tarehe 3 Dsemba 2020, aliyewahi kuwa Mwandishi wa Kampuni ya Mwananchi Comunication Limited (MCL) inayochapisha magazeti ya Mwananchi, The Citizen na MwanaSpoti, Frank Kimboi alifariki dunia. 

Mwili wa Kimboi aliyezaliwa tarehe 11 Machi 1983 ulizikwa nyumbani kwao jijini Arusha.

Deogratius Kessy

Tarehe 12 Desemba 2020, Kituo cha Redio cha Moshi FM mkoani Kilimanjaro kilimpoteza mtangazaji wake katika kipindi cha Base Show, Deogratius Kessy, aliyefariki kwa ajali ya gari mkoani Kilimanjaro.

Ajali hiyo ilitokea katika barabara ya Getifonga eneo la Kona ya kibao cha kuelekea Kahe mkoani humo, baada ya gari alilopanga Kessy kuacha njia na kugonga bajaji.

Benedict Kuzwa

Benedict Kuzwa, aliyekuwa mwandishi wa habari wa Redio Kili Fm iliyoko Moshi mjini mkoani Kilimanjaro alifariki dunia tarehe 7 Desemba 2020 kwa ajali ya gari mkoani humo.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari Mchanganyiko

Rais Samia awataka wahariri kufanya kazi bila uoga, upendeleo

Spread the love  RAIS Dk. Samia Suluhu Hassan amewataka wahariri wa vyombo...

Habari Mchanganyiko

STAMICO yasaini mkataba wa bilioni 55.2 kuchoronga miamba GGML

Spread the loveSHIRIKA la Madini la Taifa (STAMICO) limezidi kufanya vizuri katika...

Habari Mchanganyiko

NMB yatoa traksuti za Mwenge wa Uhuru Mtwara

Spread the loveBENKI ya NMB imetoa traksuti kwa mkoa wa Mtwara ambako...

Habari Mchanganyiko

Yara yaja na bima ya mazao kwa wakulima

Spread the love  WAKATI serikali ikiweka mikakati mbalimbali kuimarisha sekta ya kilimo...

error: Content is protected !!