December 9, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mwaka 2020: Vigogo wengi wameanguka

Spread the love

HAUKUWA mwaka mzuri kwa baadhi ya wanasiasa nchini Tanzania na ulimwenguni kwa ujumla, kufuatia wanasiasa na watu wengine mashuhuri, kufariki dunia.  Anaripoti Saed Kubenea, Dar es Salaam … (endelea).

Miongoni mwa waliokutwa na mauti, ni pamoja na aliyekuwa rais wa Tanzania, Benjamin William Mkapa; mwanadiplomasia mashuhuri ulimwenguni, Balozi Augustine Mahiga na Jaji Mkuu Mstaafu wa Tanzania, Augustine Ramadhani.

Mkapa aliyekuwa na umri wa miaka 81 na ambaye aliongoza Tanzania kati ya mwaka 1995 hadi 2005, alikutwa na mauti tarahe 26 Julai 2020, alipokuwa akipatiwa matibabu jijini Dar es Salaam.

Rais wa Tanzania, John Pombe Magufuli, alitangaza siku 7 za maombolezo ya kitaifa kufuatia kifo cha rais huyo mstaafu wa awamu ya tatu.

Rais John Magufuli akitoa heshima ya mwisho kwa mwili wa Hayati Benjamin Mkapa

Huu ulikuwa ni msiba mwingine mkubwa wa kitaifa baada ya ule wa aliyekuwa rais wa kwanza wa taifa hilo, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, ambao ulitokea 14 Oktoba 1999.

Kwa upande wa Balozi Dk. Mahiga, ambaye mbali ya kuwa mwanadiplomasia mashuhuri, aliongoza Idara ya Usalama wa Taifa (TISS),  alifariki dunia tarehe 1 Mei mwaka huu.

Kabla ya kifo chake, Dk. Mahiga, alipata kushika nafasi mbalimbali ndani ya nchi na na katika duru za kimataifa, ikiwamo kuwa mwakilishi wa kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa.

Akiwa katika chombo hicho cha kimataifa, alishiriki kikamilivu katika michakato ya kusaka amani katika eneo la nchi za maziwa makuu na nyingine za Afrika.

Balozi Dk. Mahiga, alitekeleza majukumu muhimu ya kutuliza mizozo. Amewahi pia kuwa mwakilishi wa aliyekuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon nchini Somalia, ambako alisaidia kuleta utangamano katika taifa hilo la pembe ya afrika.

Alikuwa kiungo muhimu kati ya Tanzania na mataifa ya magharibi wakati alipokuwa akitekeleza majukumu yake kama waziri wa mambo ya nje baada kuapishwa kwenye wadhifa huo mwaka 2015.

Balozi Dk. Augustine Philip Mahiga

Taarifa zinasema, Balozi Dk. Mahinga, wakati akiwa waziri wa mambo ya nje, alifanikiwa sana kutuliza mizozo kati ya serikali ya Rais Magufuli na mataifa mengine ulimwenguni, yanayotuhumu utawala wake, kuminya demokrasia, uhuru wa kujieleza na ukiukwaji wa haki za binadamu.

Baadhi ya wachunguzi wa mambo walisema, Tanzania na Afrika kwa ujumla wake, imepoteza tunu iliyokuja kwa wakati, lakini imeondoka nyakati ambazo bado ingali ikihitajika.

Balozi Dk. Mahiga, alikutwa na mauti wakati akiwa waziri wa Katiba na Sheria. Alifariki dunia akiwa nyumbani kwake mjini Dodoma.

Taarifa iliyotolewa na Ikulu, ilimnukuu Rais Magufuli akisema, Balozi Dk. Mahiga aliugua ghafla na wakati alipofikishwa hospitalini, alikuwa tayari amepoteza maisha.

Kwa upande wake, Jaji Ramadhani alifariki dunia 28 Aprili, majira ya saa 2 asubuhi, wakati akipatiwa matibabu katika hospitali ya Agha Khan jijini Dar es Salaam.

Taarifa rasmi za Mahakama na Serikali, ni kwamba Jaji Ramadhani alikuwa akisumbuliwa na saratani kwa zaidi ya miaka miwili na alipelekwa hospitali siku chache kabla ya kifo chake baada ya kuzidiwa.

Jaji Ramadhani mbali ya kuwa amepata kuwa Jaji Mkuu, alikuwa mwanajeshi katika Jeshi la Ulinzi wa Tanzania (JWTZ), aliyefikia cheo cha Brigedia. Amepata kuwa makamu mwenyekiti wa Tume ya taifa ya uchaguzi (NEC) na ile ya Zanzibar (ZEC).

Siku moja baadaye, tarehe 29 Aprili, aliyekuwa mbunge wa miaka mingi katika jimbo la Sumve, mkoani Mwanza, Richard Mganga Ndassa, naye alifariki dunia.

Marehemu Richard Ndassa

Ndasa, aliyekuwa mbunge wa Sumve kwa miaka takribani 25, aliaga dunia ghafla mjini Dodoma alikokuwa akihudhuria mkutano wa Bunge.

Ndasa aliyezaliwa tarehe 21 Machi 1959 na kuingia bungeni, Novemba 1995, alikutwa na mauti akiwa chumbani kwake, mjini Dodoma.

Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Mchungaji Getrude Lwakatare, ambaye alikuwa mchungaji mkuu wa Kanisa la Mlima wa Moto, jijini Dar es Salaam, aliaga dunia 20 Aprili jijini Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa familia yake, kifo chake kilisababishwa na shinikizo la damu na matatizo ya moyo. Siku moja baadaye, Spika wa Bunge Job Ndugai akatangaza kuwa mazishi yake yatasimamiwa na serikali na kuwa yatahudhuriwa na watu wasiozidi 10.

Japo haikusemwa kuwa ni Corona, lakini utaratibu wa serikali kuongoza mazishi ya watu waliofariki kwa virusi hivyo na kuzuia idadi ya waombolezaji kwa uchache, ulizua minong’ono kwamba huenda amekufa kwa ugonjwa huo.

Dk. Masumbuko Roman Lamwai

Hicho kilikuwa ni kifo cha tatu cha mbunge katika kipindi cha chini ya wiki mbili. Hali hiyo ilileta taharuki bungeni, hadi kumlazimu aliyekuwa Kiongozi wa Upinzani bungeni, Freeman Mbowe, kutoa wito kwa Bunge kughairishwa kwa angalau siku 21.

Hata hivyo, Spika wa Bunge, Job Ndugai, alipuuza wito huo, jambo ambalo lilimfanya Mbowe kuagiza wabunge wake kutokuhudhuria bungeni na kujitenga karantini kwa siku 14.

Siku chache baadae, tarehe 25 Aprili 2020, aliyewahi kuwa mbunge wa Mafia, mkoani Pwani, Abdulkarim Shah alifariki dunia katika hospitali moja jijini Dar es Salaam na kuzikwa na watu wachache.

Usiku wa tarahe 3 Mei, Mchungaji maarufu wa Kanisa la Ghala la Chakula cha Uzima, Peter Mitimingi, alifariki dunia baada ya kuugua ghafla.

Mitimingi alikuwa maarufu kwa mahubiri yake ya mitandaoni yaliyokuwa yakilenga nyanja mbalimbali za kimaisha kuanzia mahusiano, masomo mpaka ujasiriamali.

Usiku wa tarahe 4 Mei, mwanasheria nguli na mwanasiasa maarufu nchini Tanzania, Dk. Masumbuko Lamwai, pia alifariki ghafla.

Taarifa zilizothibitishwa na familia yake ni kuwa Dk. Lamwai aliumwa na kuzidiwa ghafla na alipokimbizwa hospitali madaktari walithibitisha kuwa ameshafariki.

Dk. Lamwai alikuwa ni miongoni mwa wanasiasa wachache wa mwanzo wa upinzani na alishinda ubunge mwaka 1995, katika jimbo la Ubungo, kupitia NCCR- Mageuzi.

Alikuwa pia wakili maarufu na mhadhiri mwandamizi wa Sheria.

Usiku wa kuamkia Jumatano, tarahe 6 Mei mwaka 2020, Shehe maarufu nchini, Suleiman Kilemile, naye aliaga dunia.

Mwanazuoni huyo wa kiislamu, alikutwa na mauti, siku chache baada ya kutoa wito kwa waislamu kuchukua tahadhari na ugonjwa wa Corona na kuwataka wenye nacho kutoa sadaka ya sabuni misikitini ili watu wanawe kwa maji na sabuni kama wanavyoshauri wataalamu wa afya.

Kufuatia taharuki hiyo, serikali ya Tanzania ilitoa tahadhari kuwa si kweli kuwa watu wote wanaofariki katika kipindi hiki cha Corona, wanafariki kutokana na mlipuko wa virusi hivyo.

Akilihutubia taifa siku ya Jumapili, Rais Magufuli alisema haiwezekani wote wanaokufa kuwa na corona na kuwa kuna magonjwa mengine pia.

Mbunge wa Newala Vijijini, kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rashidi Ajali Akbar, naye alifariki dunia katika mwaka huu unaoisha.

Akbar alifariki dunia 15 Januari 2020, katika eneo la Mnazi Mmoja mkoani Lindi.

Aliyekuwa mbunge wa Mpendae, Unguja (CCM) na mfanyabiashara maarufu Visiwani, Salum Turkey, afariki dunia, Septemba mwaka huu.

Wengine waliofariki dunia, ni aliyekuwa rais wa Kenya, Daniel Arap Moi, ambaye alikutwa na mauti tarehe 2 Aprili; aliyekuwa rais wa Misri Hosni Mubarak, aliyekutwa na mauti tarehe 25 Februari 2020 na aliyekuwa rais wa Congo, Joachim Yhombi Opango, aliyefariki dunia tarehe 30 Machi 2020.

Daniel arap Moi, Aliyekuwa Rais wa Kenya (1978-2002).

Katika orodha hiyo, yupo pia aliyepata kuwa Rais wa Burundi, Pierre Nkurunziza, aliyekutwa na mauti, tarehe 6 Agosti 2020; aliyepata kuwa rais wa Congo, Pascal Lisouba, aliyekutwa na mauti, tarehe 24 Agosti 2020 na aliyepata kuwa rais wa Mali, Moussa Traoré, aliyefariki dunia 15 Septemba.

Wengine, ni rais mstaafu wa Mali pia, Amadou Toumani Touré, aliyefariki dunia tarehe 11 Oktoba; aliyepata kuwa rais wa Ghana, Jerry John Rawlings, aliyefariki dunia tarehe 12 Novemba; aliyepata kuwa  rais Mauritania, Sidi Owalidou Abdallah, aliyefariki dunia tarehe 23 Novemba 2020; aliyepata kuwa rais wa Niger, aliyefariki dunia tarehe 24 Novemba na aliyepata kuwa rais wa Burundi, Pierre Buyoya, aliyefariki dunia tarehe 18 Desemba mwaka huu.

Kiongozi huyo wa zamani wa Burundi aliyekuwa na umri wa miaka 71, aliaga dunia  mjini Paris alipokuwa akipatiwa matibabu.

Kulingana na mtu wa familia yake aliyenukuliwa na shirika la AFP, kifo chake kimetokana na ugonjwa wa COVID-19.

RAIS wa zamani wa Burundi, Pierre Buyoya

Jumatano wiki iliyopita, Buyoya alilazwa katika hospitali moja mjini Bamako, nchini Mali alipokuwa akiishi, ambako alikuwa ameunganishiwa mashine ya kumsaidia kupumua.

Alisafirishwa kwa ndege kwenda nchini Ufaransa kupata matibabu zaidi. Chanzo hicho cha taarifa kimesema, aliwasili mjini Paris siku hiyo hiyo, lakini alipokuwa akisafirishwa kwa gari la kubeba wagonjwa kuelekea hospitalini, alikata roho akiwa bado njiani.

Buyoya aliiongoza Burundi kwa takribani miaka 13 katika vipindi viwili tofauti. Kwanza, ilikuwa ni kuanzia mwaka 1987 alipoingia madarakani kupitia mapinduzi ya kijeshi, hadi mwaka 1993 alipoachia madaraka baada ya kushindwa katika uchaguzi na mrithi wake Melchior Ndadaye ambaye aliuawa miezi mitatu tu baada ya kushika hatamu za uongozi.

Buyoya alirejea tena mamlakani mwaka 1996, baada ya mapinduzi mengine ya kijeshi, hadi 2003 alipokabidhi tena madaraka baada ya kusaini makubaliano ya amani ya Arusha.

Tangu mwaka 2012 Buyoya alikuwa mjumbe maalumu wa Umoja wa Afrika nchini Mali na katika ukanda wa Sahel, wadhifa aliojiuzulu Novemba iliyopita baada ya mahakama nchini mwake kumkuta na hatia ya mauaji dhidi ya mrithi wake Melchior Ndadaye, na kumhukumu kifungo cha maisha akiwa hayupo nchini mwake.

Buyoya alizikanusha shutuma dhidi yake, na kusema kesi hiyo iliendeshwa kisiasa.

Kuuawa kwa Ndadaye, rais wa kwanza wa Burundi kutoka jamii ya Wahutu walio wengi, na wa kwanza kuchaguliwa kwa njia ya kidemokrasia, kuliitumbukiza Burundi katika mzozo mbaya wa vita vya wenyewe kwa wenyewe, ambao uliangamiza maisha ya watu zaidi ya laki tatu.

error: Content is protected !!