Friday , 29 March 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Mwaka 2020 Taifa limepoteza vigogo hawa 
Habari za Siasa

Mwaka 2020 Taifa limepoteza vigogo hawa 

Spread the love

MWAKA 2020, umekuwa wa vilio na majonzi kwa Watanzania baada ya kuondokewa na viongozi waandamizi mbalimbali akiwemo, Rais mstaafu wa awamu ya tatu, Benjamin William Mkapa. Anaandika Hamis Mguta,… (endelea).

Ni siku kadhaa zimesalia kuuhitimisha mwaka 2020, ukiwa umeacha machozi na maumivu kwa ndugu, jamaa na marafiki waliowapoteza wapendwa wao.

Baadhi yao ni wanasiasa, majaji, wafanyabiashara pamoja na watumishi wa Mungu, waliofariki kwa nyakati tofauti.

MwanaHALISI TV linaangazia baadhi ya vigogo hao waliotutoka katika uso wa dunia.

Makongoro Mahanga

Katikati ya mapambano ya ugonjwa wa corona nchi, iliondokewa na mwanasiasa mkongwe aliyewahi kuwa mbunge wa Segerea na naibu waziri katika serikali ya awamu ya nne, Makongoro Mahanga.

Naibu Waziri wa Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana, Makongoro Mahanga akizungumza na waandishi wa habari juu ya uamuzi wake wa kujitoa CCM na kuomba kujiunga na Chadema

Mahanga ambaye baada ya kutoswa katika kura za maoni ndani ya CCM mwaka 2015, aliamua kuhamia Chadema ambako alishika nyadhifa mbalimbali ikiwemo Mwenyekiti wa Chadema mkoa wa Ilala, alifikwa na mauti alfajiri ya Jumatatu ya tarehe 23 Machi 2020 Hospitali ya Taifa ya Muhimbili jijini Dar es Salaam na alizikwa Alhamisi ya Machi 26 2020 katika makaburi ya Segerea jijini humo.

Bosi wa Katani

Alfajiri ya tarehe 30 Machi 2020, Mkurugenzi wa Kampuni ya Katani Limited, Salum Shamte, alifariki dunia katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), alikokuwa anapatiwa matibabu.

Kabla ya umauti kumfika, Shamte alikuwa mahabusu akikabiliwa na mashtaka ya uhujumu uchumi, utakatishaji fedha na kusababisha hasara ya Sh.1.14 bilioni  kwa Vyama vya Msingi vya Ushirika (Amcos).

Shamte aliwahi kuwa Mwenyekiti wa Taasisi Binafsi Tanzania (TPSF) na alipandishwa

Salum Shamte

mahakamani kwa mara ya kwanza kuhusu tuhuma hizo, tarehe 31 Oktoba 2019.

Mchungaji Rwakatare

Miongoni mwa vifo vilivyoishtua watu wengi mwaka 2020 ni kilichomhusu Mchungaji wa Kanisa la Mlima wa Moto (Mikocheni B Assemblies of God), Gertrude Rwakatare, aliyefariki dunia alfajiri ya tarehe 20 Aprili 2020.

Licha ya Rwakatare kuwa mchungaji lakini alikuwa mwanasiasa na hadi umauti unamfika, alikuwa mbunge viti maalumu kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM).

Mch. Getrude Lwakatare

Miezi michache kabla ya umauti kumfika, Mchungaji Rwakatare alivuma na ibada yake ya upepo wa kisulisuli aliyowaombea wanawake wasioolewa ili wapate wanaume wa kuwaoa.

Kutokana na ibada hizo, zilimfanya kupata waumini wengi zaidi siku za Jumapili waliokwenda kuhudhulia na kuwaombea.

Jaji Ramadhan

Tarehe 28 Aprili 2020, Taifa lilikumbwa na simanzi baada ya kuondokewa na aliyekuwa  Jaji Mkuu Mstaafu wa Tanzania, Augustino Ramadhani aliyefariki dunia katika Hospitali ya Agha Khan jijini Dar es Salaam baada ya kuugua kwa muda mrefu maradhi ya saratani na mwishoni kupata mshtuko wa moyo.

Jaji Ramadhani alianza kuugua mwaka 2011 na kugundulika kuwa na ugonjwa wa saratani  ambapo alitibiwa katika hospitali mbalimbali nje na ndani ya nchi.

Hospitali alizotibiwa ni pamoja na hospitali za Apollo na Bangalow nchini India, Afrika ya Kusini, Nairobi, Agha Khan na Dar es Salaam.

Tarehe 8 Januari 1980, Augustiono Ramadhani aliapishwa kuwa Jaji Mkuu wa Zanzibar wadhifa alioushikilia mpaka mwaka 1989 ambapo tarehe 28 Januari 1989 aliteuliwa na Rais wa awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani.

Jaji Augustino Ramadhani akionesha mkoba wenye fomu za kuwania Urais kupitia CCM. Kulia ni mke wake

Aidha akiwa na wadhifa huo, aliwahi kuwa Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) nchini Tanzania.

Akiwa mahakamani, aliendelea kupanda vyeo vya kijeshi mpaka kufikia kuwa Brigedia Jenerali mwaka 1995.  Mwaka 1997 alistaafu jeshi kwa hiari.

Mwaka 2007, Rais wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete alimteua Ramadhani kuwa Jaji Mkuu wa Tanzania ambapo alidumu kwenye cheo hicho mpaka tarehe  27 Desemba 2010 alipostaafu kwa mujibu wa sheria.

Miongoni mwa nyadhifa nyingine alizowahi kushika ni pamoja na kuwa Jaji wa Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu, wadhifa alioushika kwa kipindi cha miaka miwili kuanzia mwaka 2014 hadi 2016.

Jaji Ramadhani pia aliwahi kuwa Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyoundwa na Rais wa awamu ya nne Jakaya Mrisho Kikwete Julai  2012.

Mwaka 2015, Jaji Ramadhan, alikuwa miongoni mwa wanachama 42 wa Chama Cha Mapinduzi, aliyejitosa kuchukua fomu kuwania kuteuliwa kuwania urais.

Hata hivyo, ndoto zake hazikufanikiwa kwani CCM ilimpitisha Dk. John Magufuli kuwa mgombea wake wa urais.

Richard Ndassa

Tarehe 29 Aprili 2020, aliyekuwa Mbunge wa Sumve mkoani Mwanza kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Richard Ndassa alifariki dunia akiwa mkoani Dodoma.

Marehemu Richard Ndassa

Mbunge huyo alifariki dunia akiwa mkoani Dodoma aliokwenda kushiriki vikao vya Bunge vilivyokuwa vikiendelea kama sehemu ya majukumu yake ya kibunge.

Ndassa aliyezaliwa tarehe 21 Machi 1959, katika historia yake, alianza kuwa Mbunge katika jimbo la Sumve tangu mwaka 2010.

Balozi Mahiga

Alfajiri ya tarehe 01 Mei 2020, hazikuwa nzuri kwani zikaibuka taarifa za kifo cha Waziri wa Katiba na Sheria, Balozi Augustine

Philip Mahiga, (aliyekuwa mbunge).

Balozi Mahiga aliugua ghafla akiwa nyumbani kwake mjini Dodoma na akafikishwa hospitali akiwa ameshafariki dunia.

Balozi Mahiga ambaye amekuwa kwenye duru za kimataifa tangu ujana wake, Katika uhai wake,  amewahi kushika nyadhifa mbalimbali ndani na nje ya nchi.

Balozi Dk. Augustine Philip Mahiga

Kwa miaka mingi alikuwa mwakilishi wa kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa.

Akiwa katika chombo hicho cha kimataifa, alishiriki kikamilivu katika michakato ya kusaka amani katika eneo la nchi za maziwa makuu na nyinginezo za Afrika.

Aliwahi pia kuwa mwakilishi wa aliyekuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon nchini Somalia ambako alisaidia kuleta utangamao katika taifa hilo la pembe ya afrika.

Alikuwa kiungo muhimu kati ya Tanzania na mataifa ya magharibi wakati alipokuwa akitekeleza majukumu yake kama waziri wa mambo ya nje baada tu kuapishwa kwenye wadhifa huo mwaka

2015 na Rais Magufuli.

Job Lusinde

Alfajiri ya tarehe 7 Julai 2020 nchi ikampoteza mkongwe mwingine wa siasa, Job Lusinde ambaye alikuwa miongoni mwa mawaziri 11 wa kwanza wa Serikali ya Tanganyika.

Balozi Job Lusinde

Mzee Lusinde aliyezaliwa tarehe 9 Oktoba 1930, Kikuyu jijini Dodoma, alikuwa mjumbe wa Baraza la Wadhamini la Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Enzi za uhai wake, aliwahi kuwa waziri wa uchukuzi na mawasiliano mwaka 1965 katika utawala wa awamu ya kwanza chini ya Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Hayati Benjamin Mkapa

Kabla nchi haijapoa vizuri na majonzi hayo, usiku wa tarehe 23 Julai mwaka 2020, tukapata pigo lingine la kuondokewa na Rais mstaafu wa awamu

ya tatu Hayati Benjamin William Mkapa, akihitimisha safari yake ya siku 29,845 za kuishi duniani.

Hayati Mkapa aliyezaliwa tarehe 12 Novemba 1938 katika kijiji cha Lupaso, Masai mkoani Lindi alifariki dunia kwa mshtuko wa moyo.

Kuanzia tarehe 12 Novemba 1938 hadi Jumatano ya tarehe 29 Julai 2020 ambayo alizikwa ni sawa na siku 29,845 ambazo ni miezi 980 na siku 17.

Pia, ni sawa na saa 716,280 na wiki 4,263 alizotumia kuwa katika uso wa dunia.

Mkapa aliongoza Tanzania kwa nafasi ya juu ya uongozi kwa miaka kumi mfululizo kuanzia mwaka 1995 akichukua nafasi iliyokuwa imeachwa na Rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi hadi mwaka 2005 alipomwachia kijiti, Jakaya Mrisho Kikwete.

Mkapa alihitimisha safari yake akiacha mjane, Mama Anna na watoto wawili wa kiume, Stephano na Nicholas.

Mkapa ameondoka katika uso wa dunia akiwa ameacha kitabu kinachoelezea maisha yake cha My Life, My Purpose (Maisha Yangu, Kusidio Langu) kilichozinduliwa tarehe 12 Novemba 2019 siku aliyotimiza miaka 80.

Kutokana na uzito wa kifo chake, Rais John Magufuli aliamua kubadili jina la uliokuwa Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaalm kwa kuitwa Uwanja wa Benjamin Mkapa katika kumuenzi kwenye mchango wake kwenye sekta ya Michezo.

 

Uwanja huo ambao ulianza kujengwa mwaka 2003 chini ya utawala wa Hayati Benjamini William Mkapa baada ya kuahidi kujenga Uwanja huo mwaka 2000 na kukamilika mwaka 2007.

Magufuli alifanya uamuzi huo alipokuwa anahutubia Taifa wakati wa tukio la kutoa heshima za mwisho kwa mwili wa Hayati Mkapa, katika Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam na kusema Mkapa hakupenda vitu vingi viitwe kwa jina lake.

Rais John Magufuli akitoa heshima ya mwisho kwa mwili wa Hayati Benjamin Mkapa

Uwanja huo, ulikamilka mwaka 2007 chini ya utawala wa Jakaya Mrisho Kikwete katika serikali ya awamu ya nne, wenye uwezo wa kubeba Watazamaji 60,000 ulioghalimu dora za kimarekani 56 milioni.

Yassin Abdallah ‘Ustadhi’

Asubuhi ya tarehe 7 Septemba 2020, Rais wa Oganaizesheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBO), Yassin Abdallah ‘Ustadhi’ alifariki dunia nyumbani kwake Buza jijini Dar es Salaam baada ya kuugua kwa kipindi kirefu.

Enzi za uhao wake, Ustadhi atakumbukwa jinsi alivyokuwa akipambana kuwatetea mabondia wa ngumi za kulipwa na kuutangaza vyema mchezo huo ndani na nje ya nchi.

Mwili wa Ustadhi ulizikwa tarehe 8 Septemba 2020, Buza jijini humo.

Jaji Mark Bomani

Usiku wa kuamkia tarehe 11 Septemba 2020, aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa kwanza Tanzania (AG), Jaji Mark Bomani alifariki dunia katika Hospitali ya Taifa Muhimbili jijini Dar es Salaam alipokuwa akipatiwa matibabu.

Bomani aliongoza Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuanzia mwaka 1965 hadi 1976 chini ya serikali ya kwanza ya kwanza ya Hayati Mwalimu Julius Nyerere.

Jaji Mark Bomani (kulia) akimpa tuzo Mkurugenzi wa Hali Halisi Publishers, Saed Kubenea

Mwaka 2019 aliugua na kupata matibabu nchini Afrika Kusini na India, hali yake ilikuwa nzuri na aliweza kurejea katika kazi alizozipenda za sheria, lakini hali yake ilibadilika ghafla na alifariki dunia tarehe 11 Septemba 2020 huku akiwa ameacha mke, watoto watatu na wajukuu sita.

Enzi za uhai wake, Hayati Bomani alikuwa Mjumbe wa Tume ya Uchaguzi, Mwenyekiti wa Tume ya Utangazaji, Mwenyekiti wa Kamati ya Kupitia Sera ya Madini ambayo iliwezesha kutungwa kwa sheria ya madini.

Alikuwa mmoja wa Wajumbe wa Bodi ya Kwanza ya Udhamini ya Chama Cha Mapidunzi (CCM) hadi umauti ulipomkuta.

Mr. White

Usiku wa kuamkia tarehe 15 September, 2020, Salim Hassan Abdullah Turky maarufu ‘Mr. White’ aliyekuwa mbunge wa Mpendae tangu 2010 kupitia Chama cha Mapinduzi CCM alifariki dunia akiwa hospitali ya Tasakhta global baada ya kuugua ghafla na kuzikwa Fumba, Zanzibar.

Katika upande mwingine nje ya siasa, Salim Turky alikuwa mfanyabiashara maarufu Zanzibar, alizaliwa tarehe 11 Februari, 1963, mpaka anafikwa na mauti alikuwa mwenyekiti wa makampuni ya Turky ambapo chini yake yalikuwa makampuni 12 yanayoendesha biashara zake Tanzania Bara, Zanzibar na visiwa vya Comoro.

Baadhi ya makampuni hayo yanajumuisha hoteli ya Golden Tulip, hospitali kubwa ya Tasakhtaa Zanzibar, pia alijihusisha na biashara ya saruji, Nitak communications pamoja na vyakula na mafuta.

Turks Group iliazishwa mwaka 1978 kama duka la nguo na ndugu wa familia moja ambao ni Salim, Murtadha na marehemu Yunus pamoja na baba yao, Hassan Turky na miaka 40 baadae wakalibadilisha kuwa moja ya makampuni yanayoongoza Tanzania.

AG wa zamani Z’bar

Siku chache baada ya uchaguzi mkuu wa tarehe 27 na 28 Oktoba 2020 kumalizika, chama cha ACT-Wazalendo kiliondokewa na mwakilishi wake Aboubakar Khamis Bakar aliyeshinda uwakilishi katika jimbo la Pandani.

Aboubakar aliyefariki tarehe 11 Novemba 2020, akiwa nyumbani kwake Mbweni visiwani Unguja, Zanzibar akiwa hata hajaapishwa.

Pia, alikuwa mjumbe wa kamati kuu ya chama na mwenyekiti wa kamati ya maadili ya chama cha ACT Wazalendo.

Aliwahi kuwa mwandishi wa Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, Mwanasheria Mkuu Mstaafu wa Zanzibar (AG) kati ya mwkaa 1984 hadi 1988 na Naibu Jaji Mkuu kati ya mwaka 1989 hadi 1990.

Mbali na hayo, aliwahi kuwa ni mjumbe wa zamani wa kamati ya kutafuta mwafaka Zanzibar, pia mjumbe wa zamani wa kamati iliyofanikisha kuundwa kwa serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar (SUKI)

Aliwahi kushika nyadhifa mbalimbali wakati wa uhai wake ikiwemo ya kuwa Waziri wa Katiba na Sheria Zanzibar, katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa 2010 -2015.

Na mpaka mauti yanamfika, alikuwa ni mwakilishi mteule wa kuchaguliwa na wananchi katika jimbo la Pandani, Pemba, kupitia ACT-Wazalendo katika uchaguzi mkuu wa Zanzibar uliofanya tarehe 27 na 28 Oktoba 2020.

 Jaji Nsekela

Tarehe 6 Desemba 2020, Taifa likampoteza Jaji Mstaafu wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania na Kamishna wa Sekretarieti ya Maadili ya viongozi wa umma, Harold Nsekela baada ya kuugua kwa muda mfupi.

Marehemu Jaji Nsekela alizaliwa Oktoba 21 mwaka 1944. Jaji Nsekela aliteuliwa kuwa Kamishna wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Desemba 2016, wadhifa aliokuwa nao mpaka Alipofikwa na mauti jijini Dodoma na mwili wake, umezikwa mkoani Mbeya.

Profesa Mbilinyi

Huku tukiusubiri mwaka 2021 pamoja na mengine mengi yaliyotukuta, tarehe 8 Desemba 2020 taarifa zikatoka taarifa za kifo cha aliyekuwa mbunge wa zamani wa Peramiho (kati ya mwaka 1995-2005) na Waziri wa zamani wa Fedha, Profesa Simon Mbilinyi aliyefariki dunia katika Hospitali ya Aga Khan Jijini Dar es Salaam akiwa na miaka 86.

Taarifa iliyotumwa katika vyombo vya habari na Mbunge wa Jimbo la Madaba, Joseph Mhagama Ilisema, Mbilinyi atakumbukwa kwa mengi katika jimbo la Madaba na Mkoa wa Ruvuma kwa ujumla kutokana na mchango wake mkubwa wa kujenga jimbo na mkoa huo kwa ujumla.

Inaelezwa, Profesa Mbilinyi alikuwa akisumbuliwa na figo na kulazwa katika katika Hospitali ya Aga Khan ambapo juhudi za kuokoa uhai wake zilishindikana na hatimaye kufariki.

Profesa Mbilinyi alihitimu shahada ya kwanza katika Chuo Kikuu cha Cornell kabla ya kujiunga na Chuo Kikuu cha Stanford California nchini Marekani na kuhitimu shahada ya Uzamili na baadaye alijiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam(UDSM) akisoma shahada ya Uzamivu.

Kuhusu kazini tovuti ya Bunge imeonesha kuanzia mwaka 1965 hadi mwaka 1975 alikuwa mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Mwaka 1975 hadi mwaka 1983 aliteuliwa kuwa mshauri wa kiuchumi katika Ofisi ya Rais katika serikali ya Awamu ya Kwanza chini ya Hayati Mwalimu Julius Nyerere.

Aliteuliwa kuwa Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo kuanzia mwaka 1983 nafasi aliyoihudumu hadi mwaka 1985. Marehemu Profesa Mbilinyi pia aliwahi kuwa balozi wa Tanzania nchi ya Ubelgiji na Luxembourg kuanzia mwaka 1985 hadi 1989

Kuanzia mwaka 1989 hadi mwaka 1991 Mbilinyi aliteuliwa kuwa Katibu Mkuu Hazina kabla ya kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) kuanzia mwaka 1991 hadi 1995 na baadae kuwa Waziri wa Fedha kuanzia mwaka 1995 hadi

2005.

Profesa Simon Mbilinyi ameacha mke na watoto watatu na mwili wake umezikwa jijini Mbeya.

Bilionea Shubash Patel

Tarehe 15 Disemba 2020, Taifa lilishuhudia likiwapoteza watu wawili kwa nyakati tofauti.

Mosi; ni mfanyabiashara maarufu nchini Tanzania ambaye pia ni alikuwa Mwenyekiti na Mtendaji Mkuu wa Kampuni za Motisun Group, Subash Patel alifariki dunia.

Bilionea Patel ambaye alizaliwa tarehe 25 Aprili 1978, Barwani nchini India, enzi za uhai wake, aliwahi kuwa Mwenyekiti wa Shirikisho la Wenye Viwanda Tanzania (CTI).

Mwili wake ulichomwa moto tarehe 17 Disemba 2020 ikiwa ni sehemu ya utamaduni wa wahindi, na baadaye majivu yake kuzikwa.

Mzee Jengua

Siku hiyo ya 15 Desemba 2020, tasnia ya sanaa, iliondokewa na Muigizaji maarufu, Mohamed Fungafunga maarufu Mzee Jengua alifariki dunia, akiwa Mkuranga mkoani Pwani nyumbani kwa mtoto wake alipokuwa akiugulia.

Jengua alijizoelea umaarufu katika tamthilia ya Kidedea iliyokuwa inarushwa katika kituo cha runinga cha ITV, aulizikwa Makaburi ya Mburahati jijini Dar es Salaam.

“Inna lillahi wa inna ilayhi raji’un.

“Mwenyezi Mungu azilaze roho za marehemu mahala pema peponi.”

 

 

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaTangulizi

Chadema: Samia aunde tume kuchunguza mauaji mgodi wa Barick

Spread the loveRAIS Dk. Samia Suluhu Hassan, ameombwa aunde tume huru kwa...

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Nani anasema kuna hasara ATCL?

Spread the loveRIPOTI za makusanyo na matumizi ya fedha katika Kampuni ya...

Habari za SiasaTangulizi

CAG: Wastaafu, wenza wao chanzo NHIF kufilisika

Spread the loveRIPOTI ya ukaguzi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu...

Habari za SiasaTangulizi

Vikundi hewa 851 vyalamba bilioni 2.6 mikopo ya halmashauri

Spread the loveVIKUNDI hewa vya wajasirimali wadogo 851 kutoka katika halmashauri 19...

error: Content is protected !!