Thursday , 28 March 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Mwaka 1 SSH: Wasanii kicheko, watema nyongo
Habari za SiasaTangulizi

Mwaka 1 SSH: Wasanii kicheko, watema nyongo

Rais Samia Suluhu Hassan akishuhudia mchezo kati ya Simba Na Yanga kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam
Spread the love

 

WAKATI Rais Samia Suluhu Hassan akitarajiwa kutimiza mwaka mmoja madarakani tangu alipoapishwa rasmi tarehe 19 Machi, 2021, sekta ya sanaa na burudani ni miongoni mwa zilizofaidika na mapinduzi makubwa ya uongozi wake.

Mapinduzi hayo yamegusa maeneo nane, ambayo ni kuunda wizara ya utamaduni, sanaa na michezo; kuanzisha mpango wa wasanii kupatiwa mirabaha, kuanzisha tuzo za filamu na tuzo za muziki Tanzania.

Mapinduzi mengine ni kuboresha tamasha la Serengeti Festival, kuanzisha tamasha la utamaduni kwa kila mkoa, kuanzisha shule za michezo na sanaa kila jimbo na kuwasogeza wasanii karibu na taasisi hiyo ya urais kiasi cha kufungua milango ya kazi kwao.

MUUNDO WA WIZARA
Pamoja na mambo mengine, kuing’oa idara ya Habari na kubakisha Wizara kamili ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, ni kitendo ambacho kimetajwa kuleta mageuzi makubwa ndani ya sekta ya burudani.

Katika mabadiliko hayo yaliyofanyika tarehe 12 Septemba mwaka jana yalishuhudiwa wizara hiyo ikikabidhiwa kwa Waziri Innocent Bashungwa kabla ya kuhamishiwa TAMISEMI na nafasi yake kuchukuliwa na Mohamed Mchengerwa Januari mwaka huu.

Mabadiliko hayo yamechangia kuongezeka kwa ubunifu miongoni mwa watumishi wa wizara hiyo hasa ikizingatiwa idara ya habari ilikuwa kama imezimeza idara nyingine za sanaa, michezo na utamaduni.

MIRABAHA

Suala la wasanii kulipwa gawio kulingana na namna nyimbo zao zinavyotumika katika nyanja mbalimbali nchini yaani mirabaha, lilikuwa ni kama ngonjera kwani kwa miaka mingi lilizungumzwa bila kutekelezwa.

Itakumbukwa mara ya mwisho mwaka 2019, aliyekuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Harrison Mwakyembe alisema kwamba Agosti 28, 2019, ndio itakuwa mwisho wa kazi za sanaa kutumika bila kulipia, akizungumzia zaidi redio, kumbi za starehe na vyombo vya usafiri japo suala hilo halikutekelezwa.

Lakini ni Rais Samia aliyeamua kufunga mjadala kuhusu suala hilo wakati akizungumza na vijana jijini Mwanza tarehe 15 Juni, 2021 na kuweka bayana kuwa kuanzia Disemba, 2021 wasanii wataanza kulipwa mirabaha yao kutokana na kazi zinazotumiwa kwenye runinga, redio na mitandaoni.

Usiku wa Ijumaa tarehe 28 mwezi Januari mwaka 2022 Taasisi inayosimamia hakimiliki na hakishiriki (COSOTA) iliwagawia wasanii wa muziki pesa ambazo ilizikusanya kwa niaba yao na kuanza kuinua morali ya wasanii kujiona nao wapo katika taaluma inayotambulika na kuwaletea faida.

Katika kutekeleza agizo hilo la Rais Samia, ilishuhudiwa kiwango kikubwa cha ‘mpunga’ kikielekea kwa Kwaya ya Mtakatifu Cecilia ya Arusha walioongoza kwa kupata hundi ya Sh milioni 8.7 ikifuatiwa na msanii Ali Kiba ambaye alipokea milioni 7.5 na Rose Muhando ambaye alipata milioni 5.7.

Hata hivyo, katika ugawaji huo wa mirabaha wapo wasanii walionung’unika kwa kutopatiwa chochote kama ilivyo kwa Khadija Shabani ambaye kwa jina la kisanii anafahamika kama Keisha.

Keisha ambaye pia ni Mbunge wa vitimaalum (CCM) mbali na kupongeza hatua hiyo kwa kusema kwamba mwanzo ni mzuri na kazi nzuri imefanyika, alidai kushangaa jina lake kutotajwa.

Aidha, Keisha, alimshukuru Rais Samia na Serikali yake kwa usikivu wa mambo na kuona namna ya kubadilisha Sheria ziweze kutekelezeka kwa urahisi zaidi.

Hoja hiyo inaungwa mkono na mkali wa muziki wa dansi na sanaa za majukwaani, Mrisho Mpoto ameieleza MwanaHalisi Online kwamba suala la mirabaha limevunja mfupa uliowashinda watangulizi wake wengi.

TUZO ZA FILAMU TANZANIA

Tarehe 18 Disemba mwaka 2021, kulifanyika kinyang’anyiro cha kuwania tuzo za filamu Tanzania.

Hii ni mara ya kwanza tuzo hizi kuandaliwa na Serikali ya Tanzania hali ambayo imezidi kuwasogeza wasanii karibu na Serikali yao kiasi cha kujenga uaminifu kwa kila kundi.

Zaidi ya filamu 35 ziliingia katika kinyang’anyiro cha kuwania Tuzo za Filamu Tanzania ambazo zilifanyika mjini Mbeya na tuzo 29 zitatolewa.

Akizungumza umuhimu tuzo hizo katika tasnia ya filamu, Mwenyekiti wa jopo la majaji saba waliozipitia filamu hizo, Profesa Martin Mhando alisema hiyo ni hatua kubwa ya maendeleo ya tasnia ya sanaa.

Profesa Mhando alisema kuna mapinduzi makubwa katika sinema za Tanzania na ikiwa na hadhira ya lugha ya Kiswahili kwa watu milioni 200 na kama kutakuwapo na sera inayokidhi mahitaji ya sasa na baadaye kuwepo na ruzuku kwa tasnia.

TUZO ZA MUZIKI TANZANIA

Ikumbukwe kwamba tuzo hizi zinaandaliwa na Baraza La Sanaa Tanzania (BASATA), ambalo limejumuishwa kuhakikisha uadilifu na utunzi bora wa mashairi katika nyimbo za wasanii

Hizi ni tuzo ambazo sasa zinarejeshwa chini ya uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita baada ya waandaaji wa tuzo hizo kutoka sekta binafsi kusuasua na kushindwa kuziandaa tena katika kipindi cha zaidi ya muongo mmoja.

Hakika ni furaha kwa wasanii kujipima na kuona ukubwa wa kazi wanazozifanya na haya yote yanafanyika katika kipindi cha mwaka mmoja wa Rais Samia pekee.

Kaimu Katibu Mtendaji, Matiko Mniko kutoka BASATA amesema katika tuzo hizo zitakazotolewa mwezi huu, kutakuwa vipengele 23 na ndani ya vipengele hivyo kuna tuzo zipatazo 51

TAMASHA LA SERENGETI FESTIVAL

Tamasha la Muziki la Serengeti hili nalo limepewa nguvu ya kipekee kutokana na mabadiliko aliyofanya Rais Samia.

Serengeti Festival ni jukwaa lingine ambalo Mrisho Mpoto anasema ni kimbilio maridhawa kwa wasanii wote nchini bila kujali umri na ukubwa wao katika tasnia ya Sanaa.

Anasema jukwaa hili linazidi kuwaimarisha wasanii kwa kuwapa fursa ya kufanya kile ambacho kitazidi kumjengea heshima na jina katika siku za usoni.

Tamasha hilo ambalo linafanyika kwa mara ya tatu, linawaleta pamoja wasanii wa kizazi cha zamani, kati na kizazi cha sasa na kuratibiwa na Wizara husika, limefanyika mapema Machi mwaka huu mkoani Dodoma.

TAMASHA LA UTAMADUNI

Itakumbukwa baada ya kuapishwa kuwa Chifu Mkuu, Septemba mwaka jana, Rais Samia aliagiza kila mkoa kuandaa tamasha la utamaduni.

Hatimaye mkoa wa Kilimanjaro ulifungua dimba tarehe 22 Januari katika tamasha hilo ambalo pia Rais Samia alilizindua huko katika Viwanja vya Chuo Kikuu cha Ushirika mjini Moshi.
Makabila yote mkoani Kilimanjaro yalijitokeza kuwafundisha na kuwaonesha wahudhuriaji wa tamasha hilo tamaduni mbalimbali za mababu zao.

SHULE ZA MICHEZO KILA JIMBO

Mbunge wa Morogoro Kusini Mashariki, Hamis Taletale maarufu kama Babu tale’ naye anasema hili ni mojawapo ya jambo analijivunia akiwa kama mdau wa sanaa.

Babu tale ambaye ni mmoja wa mameneja wa Msanii Diamond Platnums anasema uanzishwaji wa shule hizo utatibu kilio cha siku nyingi ambacho kilikuwa kimeighubika jamii ya Watanzania kwa watoto kutotambua wala kupata jukwaa la kuonesha vipaji vyao.

KUWASOGEZA WASANII KARIBU

Hili ni jambo ambalo Mrisho Mpoto anasema limekuwa furaha kwa wasanii wengi nchini.
Anasema kitendo cha Rais Samia kutambua kazi za wasanii, kuwasogeza karibu na kuwashirikisha katika shughuli mbalimbali, kumezisogeza taasisi hususani za kiserikali kuondokana na urasimu wa kuogopa kuwatumia wasanii.

Anasema hata vipato vya wasanii sasa vinaongezeka kutokana na ushirikishwa huo wa karibu.

Hoja za Mpoto zinaungwa mkono na staa wa Bongo fleva, Rajabu Abdul au ‘Harmonize’ ambaye anasema mapinduzi hayo ya sekta ya sanaa kama vile tuzo za ndani ya Tanzania, ni hatua kubwa itakayowasaidia wasanii kupima ukubwa wao ndani ya Taifa na ni kwa kiasi gani mashabiki wao wanakubali kazi zao.

Aidha, penye mafanikio hapasi changamoto, ndio maana Staa namba moja wa Bongofleva nchini, Naseeb Abdul anatoa wito kwa wizara na mamlaka mhusika kujipanga vema hususani katika masuala ya tuzo ili wasiitie aibu serikali.

Makala hii imeandaliwa na Gabriel Mushi.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaTangulizi

CAG: Wastaafu, wenza wao chanzo NHIF kufilisika

Spread the loveRIPOTI ya ukaguzi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu...

Habari za SiasaTangulizi

Vikundi hewa 851 vyalamba bilioni 2.6 mikopo ya halmashauri

Spread the loveVIKUNDI hewa vya wajasirimali wadogo 851 kutoka katika halmashauri 19...

Habari za SiasaTangulizi

Mashirika matano yapata hasara mabilioni ya fedha

Spread the loveMASHIRIKA matano ya Serikali yanayojiendesha kibiashara, yamepata hasara ya mabilioni...

Habari za SiasaTangulizi

CAG aibua madudu halmashauri 10, TANESCO na MSD

Spread the loveRIPOTI ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali...

error: Content is protected !!