Saturday , 15 June 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Minyukano waipeleka Bunge mpaka usiku
Habari za SiasaTangulizi

Minyukano waipeleka Bunge mpaka usiku

Spread the love

BUNGE jana lililazimika kuendelea na kikao chake hadi saa 3:27 usiku baada ya wabunge kutokana na wabunge kupinga marekebisho ya sheria mbalimbali ikiwamo ya Sekta ya Korosho. Anaripoti Dany Tibason … (endelea).

Mbali na korosho, wabunge walitumia muda mwingi kujadili kuhusu mgawanyo wa asilimia 10 ya mapato ya halmashauri kwenda kwenye makundi maalum ya wazee, vijana na watu wenye ulemavu pamoja na changamoto ya Zanzibar kulipa kodi kubwa kwenye huduma ya umeme inaoupata kutoka Shirika la Ugavi wa Umeme (Tanesco). 

Awali jana asubuhi, serikali kupitia kwa Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, iliwasilisha bungeni jijini Dodoma Muswada wa Sheria ya Fedha wa Mwaka 2018 unaokusudia kufuta Sheria ya Tume ya Mipango na kufanya marekebisho ya sheria nyingine 16.

Hata hivyo, Bunge lilipoketi kama kamati kupitia kila kifungu cha muswada huo, hoja kuhusu kufanya marekebisho kwenye sheria zinazohusu mambo hayo matatu (korosho, gharama za umeme Zanzibar na mgawanyo wa asilimia 10 ya mapato ya halmashauri kwenda kwa makundi maalum) zilichukua muda mrefu kupata mwafaka.

Kutokana na changamoto hiyo, Spika Job Ndugai aliyekuwa anaongoza kikao hicho, alimtaka Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Sera, Bunge, Ajira, Kazi na Watu Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama, kutengua kanuni ili kikao hicho kiendelee mpaka pale uchambuzi wa muswada huo ukamilike.

Jenista alitengua kanuni na wabunge wengi waliridhia jambo lililopelekea  Bunge kumaliza kazi yake saa 3:27 badala ya saa 2:00 iinavyotakiwa kikanuni.

Korosho

Baada ya mvutano wa takribani wiki mbili, Bunge juzi lilipitisha kifungu cha sheria kuhusu asilimia 100 ya ushuru wa mauzo ya korosho ghafi nje nchi (export levy) kupelekwa Mfuko Mkuu wa Serikali.

Sheria iliyopo ya Sekta ya Korosho, Kifungu cha 17A inataka mgawanyo wa mapato hayo kuwa asilimia 65 ipelekwe kwenye Bodi ya Korosho na asilimia 35 iwekwe Mfuko Mkuu wa Serikali.

Baadhi ya wabunge walioongozwa na wabunge wa mikoa ya Kusini, walikuwa wanapinga vikali uamuzi huo wa serikali, wakieleza kuwa utaua zao hilo.

Baada ya mvutano huo kuchukua takribani nusu saa, Spika Ndugai aliwahoji wabunge kuhusu hoja ya serikali na wengi waliikubali, hivyo kupitishwa na Bunge.

Kabla ya kufikia hatua ya kupiga kura, wabunge wa upinzani Zitto Kabwe (Kigoma Mjini-ACT Wazalendo), Zuberi Kuchauka (Liwale-CUF), Ahmed Katani (Tandahimba-CUF), walipinga vikali marekebisho ya sheria hiyo huku wakipinga maelezo yaliyotolewa awali na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dk. Adelardus Kilangi kuhusu suala hilo.

Pia Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti ilipinga uamuzi huo wa serikali, ikieleza kuwa utarudisha nyuma maendeleo ya zao hilo.

Kutokana na hali hiyo, Spika Ndugai alimtaka Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kutoa ufafanuzi kuhusu uamuzi wa serikali kuchukua asilimia 100 ya ushuru huo wa mauzo ya korosho ghafi ughaibuni.

Katika ufafanuzi wake, Waziri Mkuu Majaliwa amesema: “Ninawasihi sana waheshimiwa wabunge, maelezo ya AG (Mwanasheria Mkuu wa Serikali) ni sahihi, tunalenga kuyadumisha mazao yote bila kuwa na ‘double standard’ (kuwa na upendeleo).”

Amesema wabunge wameeleza kwa kina mawazo yao kuhusu suala hilo na yamechukuliwa na AG Kilangi na Waziri wa Kilimo, Dk. Charles Tizeba kwa ajili ya kufanyiwa kazi.

“Niwaombe wabunge tukubali ili serikali ichukue jukumu la kulihudumia kila zao na wale tuliowapa nafasi ya kuhudumia tuhakikishe wanafanya hivyo,” amesema Waziri Mkuu na kuongeza.

“Kila zao linahudumiwa kuanzia pembejeo na masoko na hakuna mahali tutaacha mazao yakaharibika bila hatua thabiti kuchukuliwa.”

Huku akishangiliwa na wabunge wa CCM, kiongozi huyo wa serikali amesema kuwa ili kupanua wigo wa mazao hayo, serikali imejidhatiti katika kuinua viwanda na kilimo.

Mgawo kwa wenye ulemavu

Katika mjadala huo, Mbunge wa Viti Maalum, Amina Mollel (CCM) alipinga pendekezo la serikali la kugawa asilimia 10 ya mapato ya halmashauri kwa asilimia 50 kwa 50 kwa vijana na wazee, huku  akipendekeza fedha hizo zigawanywe kwa utaratibu wa asilimia 40-40-20, yaani asilimia 40 kwa wazee, asilimia 40 nyingine kwa vijana na asilimia 20 kwa watu wenye ulemavu.

Mawaziri akiwemo, Luhaga Mpina wa Mifugo na Uvuvi na Jenista Mhagama wa Ofisi ya Waziri Mkuu – Sera, Bunge, Ajira, Vijana, Kazi na Watu Wenye Ulemavu, walisimama kutetea pendekezo hilo lakini Spika Ndugai aliporuhusu kura ipigwe, hoja ya Mollel ilishinda.

Hata hivyo, hoja hiyo iliibua hisia kali miongoni mwa wabunge huku Spika Ndugai akiwataka mawaziri kuwa makini nayo,kwani hoja nyingine zinasabaishwa na serikali kulichukulia muda mwingi na kufanya mjadara kufikia takribani nusu saa kufikia mwafaka.

Kodi mara mbili Umeme Zanzibar

Naye Mbunge wa Welezo, Saada Mkuya Salum (CCM), aliibua hoja kwamba Zanzibar inatozwa kodi ya ongezeko la thamani (VAT) mara mbili (yaani asilimia 36) kutokana na huduma ya umeme unaozalishwa na kusambazwa na Tanesco.

Kutokana na changamoto hiyo, Waziri huyo wa zamani wa Fedha, alisema kuna haja Zanzibar ionewe huruma, akieleza kuwa si sahihi kutozwa kiwango hicho kikubwa cha kodi.

Hoja hiyo iliungwa mkono na Mbunge wa Ubungo, Saed Kubenea (Chadema), Mbunge wa Muleba Kusini, Prof. Anna Tibaijuka (CCM), Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti, Hawa Ghasia pamoja na Spika Ndugai ambaye aliitaka serikali kutoa ufafanuzi.

Waziri wa Nishati, Dk. Medard Kalemani alisimama kutolea ufafanuzi suala hilo lakini maelezo yake yalionekana kutowakosha wabunge na Spika Ndugai.

“Zeco (Shirika la Umeme Zanzibar) siyo wakala wa Tanesco, bali ni shirika la umma na umeme unaozungumziwa hapa Mwenyekiti (Spika Ndugai) siyo umeme wa mtu mmoja mmoja bali ni wa umeme wa viwandani,” Kubenea alisema na kuongeza.

“Sasa umeme huo unapokwenda Zanzibar, Zeco inalazimika kuuza umeme kwenye kampuni kubwa kama za utalii kwa bei ya juu tofauti na umeme unaouzwa viwandani Tanzania Bara na ndiyo huohuo unatozwa VAT.

“Huo mfumo wa usafirishaji wa umeme wenyewe umechangia ni mfumo wa Muungano, siyo wa Tanesco peke yake. Sasa hili ni jambo linashirikisha nchi mbili kuitoza Zanzibar VAT mara mbili siyo sahihi hata kidogo na ndiyo maana waziri mwenyewe anakiri.

“Hili jambo limekuwa sehemu ya kero za Muungano. Kama tunautakia mema Muungano huu, tuondokane na hili jambo, wabunge wa Zanzibar wameongea kwa hisia kali sana juu ya jambo hili, wananchi wa Zanzibar wanaumia, leo hoteli za Zanzibar hazitumii umeme wa Tanesco, wanalazimika kutumia jenereta kwa sababu umeme unauzwa ghali.”

Kutokana na hali hiyo, Spika Ndugai aliitaka serikali kutoa uamuzi kuhusu suala hilo ndipo Waziri Mhagama aliposimama na kuliomba Bunge litoe muda kwa Serikali ya Muungano kujadiliana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ).

Maelezo hayo ya Waziri Mhagama hayakuungwa mkono na Spika ambaye aliweka wazi kuwa anashangazwa na serikali kuwa na kigugumizi katika suala hilo, lakini akawahoji wabunge na kupitisha uamuzi wa kuzipa muda wa majadiliano serikali hizo mbili.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari MchanganyikoHabari za SiasaTangulizi

Rais Samia amng’oa Matinyi Serikalini, ateua viongozi mbalimbali

Spread the loveRais Samia Suluhu Hassan, amefanya uteuzi wa viongozi mbalimbali akiwamo...

BiasharaHabari za Siasa

Tanesco yawasha mtambo namba 8 Bwawa Julius Nyerere

Spread the loveNaibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko...

Habari MchanganyikoHabari za SiasaTangulizi

Samia: Wakuu wa mikoa, wilaya wanaendeleza ubabe

Spread the loveRAIS Samia Suluhu Hassan amesema bado wakuu wa wilaya na...

Habari za SiasaKimataifaTangulizi

Ramaphosa achaguliwa tena kuwa rais Afrika Kusini

Spread the loveRais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa amechaguliwa na wabunge wa...

error: Content is protected !!