Friday , 19 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Mbunge Ukerewe, naye aikimbia Chadema
Habari za SiasaTangulizi

Mbunge Ukerewe, naye aikimbia Chadema

Spread the love

ALIYEKUWA mbunge wa Chadema katika jimbo la Ukerewe, mkoani Mwanza, Joseph Mkundi, hatimaye amemwaga manyanga. Anaripoti Mwandishi Wetu …. (endelea).

Katika barua yake kwa Spika wa Bunge la Jamhuri, Job Ndugai, mbunge huyo ameeleza kuwa ameamua kujiuzulu wadhifa wake wa ubunge, pamoja na uwanachama wa Chadema, kufuatia “kutopata ushirikiano kutoka kwa viongozi wake wa juu.”

Anasema, “nimejiuzulu nafasi zangu zote ndani ya Chadema. Nimechukua uamuzi huo, kutokana na kutopata ushirikiano kutoka kwa viongozi wangu wa juu wa kilichokuwa chama changu.”

Aidha, Mkundi anasema, amejiuzulu wadhifa wake baada ya ndugu na wananchi wake wa Ukerewe kutelekezwa na chama chake, kufuatia janga la ajali ya meli ya MV Nyerere.

Mkundi ameeleza katika barua yake hiyo aliyoiwasilisha kwa Spika Ndugai, jana tarehe 10 Oktoba 2018, kuwa“…nimejiuzulu baada ya kuona wananchi wangu wa Ukerewe hawakuthaminiwa.”

Amesema, aawashukuru sana wananchi wake wa Ukerewe na hasa wana Ukara na Bugorora, kwa kusimama naye katika kipindi hicho kigumu cha msiba mkubwa uliowapata.

Anasema, “ajali ya MV Nyerere imenifundisha sana na kunifanya kuwa mnyeyekevu zaidi. Nimeelewa ndugu wa kweli wa kushirikiana wakati wa shida na wakati wa furaha. Nawashukuru sana wananchi wa Ukerewe na hasa Ukara na Bugorora kwa kusimama pamoja nami wakati wote tulipopata msiba mkubwa wa ajali hii ya MV Nyerere.”

Anaongeza, “kibinadamu nilishindwa kuelewa kwa nini watu niliowaona ndugu zangu kisiasa, hakuna hata mmoja ambaye alifika na kusimama nasi, ukiacha maneno ya mitandaoni ambayo hayakuwa na lengo la kutufariji wala kututia moyo katika kipindi kile kigumu.”

Mkundi ambaye alikuwa pia diwani wa Kata ya Bukiko anasema, kwa msingi huo, “leo Jumatano (jana), tarehe 10 Oktoba 2018, natangaza kujivua rasmi uanachama wa Chadema.”

Anasema, hii ni kwa mujibu wa katiba ya Chadema, Ibara ya 5.4.1 na kwamba kwa uamuzi huo, jimbo hilo litakuwa wazi kuanzia sasa.

Pamoja na kujivua uanachama wa Chadema, Mkundi ameomba kujiunga na Chama Cha Mapinduzi (CCM), anachodai kuwa kimedhihirisha kwa vitendo na itikadi yake ya utu, udugu, mshikamano, haki na umoja.

Mkundi anakuwa mbunge wa tano wa chama hicho kuondoka tangu kumalizika kwa uchaguzi mkuu wa rais, wabunge na madiwani wa 25 Oktoba mwaka 2015.

Wabunge wengine wa Chadema waliondoka na kutimkia CCM mpaka sasa, ni Mwita Mwaikabe Waitara (Ukonga), Dk. Godwin Ole Mollel (Siha), Julius Kalanga (Monduli) na James Millya (Simanjiro).

Tofauti na wenzake waliotangulia, Mkundi ameeleza sababu tofauti za kuondoka kwake. Anawatuhumu viongozi wake wa juu kuwa walimtelekeza katika kipindi hicho kigumu cha msiba.

“Ni kweli, siyo Mbowe (Freeman Mbowe), mwenyekiti wa chama hicho taifa, Dk. Vicenti Mashinji, katibu mkuu, manaibu makatibu wakuu, wajumbe wa Kamati Kuu (CC), wabunge na hata viongozi wa mabaraza ya chama, waliokwenda Ukerewe kumfariji mwenzetu,” ameeleza mmoja wa viongozi wajuu wa chama hicho.

Anasema, “kutokana na hali hiyo na kwa kuzingatia kuwa CCM walikuwa wanamkodolea macho Mkundi, hicho kilichotokea, binafsi nilikitarajia.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

BiasharaHabari za Siasa

Mavunde aagiza Perseus kuharakisha fidia Sengerema

Spread the loveWaziri wa Madini, Anthony Mavunde ameipongeza Kampuni ya Perseus kwa...

Habari za Siasa

Kigogo Chadema awanyooshea vidole vigogo serikalini kuhusu ripoti ya CAG

Spread the love  MWANACHAMA wa Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Boniface Jacob, amedai...

Habari za Siasa

Wabunge waikalia kooni TAKUKURU Bungeni

Spread the love  BAADHI ya wabunge wamelia na changamoto za utendaji wa...

Habari za SiasaTangulizi

Mpina ataka Waziri Majaliwa ajiuzulu, akosoa teuzi za mawaziri

Spread the love  MBUNGE wa Kisesa, Luhaga Mpina, amemtaka Waziri Mkuu, Kassim...

error: Content is protected !!