July 26, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Mutungi asaka suluhu UKUTA vs Serikali

Spread the love

JAJI Francis Mutungi, msajili wa vyama vya siasa nchini, ameonesha hofu yake iwapo hakutakuwepo muafaka kati ya serikali na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kinachosisitiza kuanzisha maandamano na mikutano nchini nzima, anaandika Charles William.

Kumekuwepo na mvutano kati ya Serikali na Chadema kuhusu kuanza kwa maandamano pia mikutano inayotarajia kuanza kufanyika Septemba Mosi mwaka huu, chini ya operesheni inayojulikana kama Umoja wa Kupinga Udikteta Tanzania (UKUTA).

Mutungi ambaye 28 Julai mwaka huu, alijitokeza na kulaani mpango wa kuitishwa kwa maandamano na mikutano ya hadhara, akihofu kuwa inaweza kusababisha uvunjifu wa amani, amejitokeza tena leo na kusema bado jitihada na mazungumzo ili kuepusha maandamano hayo yanaendelea.

“Nawasihi wadau wote wenye mipango ya mikutano na maandamano wasubiri kwanza; tukae, tuzungumze na kukubaliana. Naamini hatuwezi kushindwa kupata suluhu ya suala hili.”

Jaji Mutungi amevitaka vyombo vya habari, kusaidia kupunguza hofu kwa wananchi kwani mazungumzo baina ya makundi mbalimbali na Chadema yanayendelea ili kuhakikisha suluhu inapatikana kabla ya Septemba mosi, mwaka huu.

“Makundi mbalimbali yanaendelea kujitahidi kujaribu kuendelea kutafuta muafaka wa suala hili, nayapongeza makundi hayo na kwa kauli yangu nataka kusema bado hatujaishiwa njia za ufumbuzi wa mvutano huu,” amesema.

Jaji Mutungi ametangaza kuwa, baraza la vyama vya siasa linalojumuisha vyama vyote vya siasa hapa nchini, litakaa katika kikao maalum kuanzia 29 hadi 30 Agosti mwaka huu katika kikao ambacho kitaalika wadau wengine muhimu ili kutafuta suluhu ya suala hilo.

“Kikao hicho cha baraza la vyama vya siasa hapa nchini, kitatoka na maazimio na iwapo wajumbe wataafikiana, wataomba kwenda kuonana na Rais John Magufuli ili kulitafutia ufumbuzi suala la mikutano ya kisiasa na maandamano,” amesema Mutungi.

Kuhusu mvutano unaoendelea ndani ya Chama cha Wananchi (CUF), Jaji Mutungi amesema, “Suala hilo limenifikia lakini si vyema kulizungumzia kwa sasa. Huu siyo muda muafaka, muda muafaka utakapofika nitalizungumzia.”

error: Content is protected !!