July 7, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Muswada wa Sheria ya Katiba ‘wachanwa’ Rais Kikwete mtegoni

Wenyeviti wa vyama vya upinzani wakiwa Ikulu na Rais Kikwete
Spread the love

RAIS Jakaya Kikwete amewekwa mtegoni. Ama akubaliane na Bunge au vyama vya siasa katika mchakato wa kuleta Katiba mpya, MwanaHALISI Online linaweza kuripoti.

Tayari vyama vitano vya siasa vilivyoko bungeni  vimekamilisha mapendekezo yanayochanachana baadhi ya vifungu vya sheria ambayo tayari rais amesaini.

“Tusingefika hapa. Ni ukaidi wa Naibu Spika Job Ndugai aliyejenga mazingira ya kufukuza wabunge wa upinzani na kufanya muswada kupitishwa na wabunge wa CCM peke yao,” amelalama mmoja wa wabunge wa chama hicho.

Rais Kikwete alinukuliwa wiki iliyopita alipokutana ikulu na wenyeviti wa vyama vitano akisema, katika kuonyesha dhamira yake ya kupata Katiba mpya, sharti kwanza “upatikane mwafaka kwenye sheria hii.”

“Ndani ya mkutano, mheshimiwa rais alisema hatutaenda kwenye hatua ya pili ya muswada wa kura ya maoni, wala hatutaenda kwenye bunge la katiba, bila kwanza kuelewana kwenye hili la sheria iliyopitishwa,” ameeleza mtoa taarifa.

Wenyeviti aliokutana nao tarehe 15 mwezi huu ni Freeman Mbowe (CHADEMA), Profesa Ibrahim Lipumba (CUF) na James Mbatia (NCCR-Mageuzi).

Wengine waliohudhuria kikao cha ikulu na kuwa kwenye kamati ya vyama ya kuandaa mapendekezo ya marekebisho ya sheria chini ya mwavuli wa Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD), ni pamoja na Makamu Mwenyekiti wa CCM, Philip Mangula na mwakilishi wa UDP.

MwanaHALISI Online limeona mapendekezo ya vyama vya siasa ambayo yanapingana na muswada uliopitishwa na bunge na rais kuusaini tarehe 10 mwezi huu.

Taarifa kutoka ofisi ya bunge, ikulu na vyama vya siasa zimethibitisha kuwa marekebisho ya muswada tayari yamewasilishwa serikalini kupitia TCD.

Marekebisho yanayoletwa na vyama ni pamoja na:

  • Idadi ya wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba kuwa 908 badala ya 604 ambao nusu watatoka Bara na nusu nyingine Zanzibar.
  • Tume ya Mabadiliko ya Katiba itakoma kufanya kazi baada ya Kura ya Maoni na matokeo yake kutangazwa.
  • Wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba watakaokuwa nje ya wabunge wa Bunge la Muungano na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, watateuliwa na makundi na asasi za kiraia kama yanavyobainishwa kwenye sheria.
  • Idadi ya wajumbe wanawake kwenye Bunge Maalum la Katiba wasipungue theluthi moja ya wajumbe walioteuliwa kutoka katika makundi hayo.

Kutolewa kwa mapendekezo hayo kumepokewa kwa tahadhari kubwa miongoni mwa wachambuzi wa masuala ya siasa, sheria na utawala nchini.

Mabere Marando, wakili mashuhuri wa Mahakama Kuu, amesema baadhi ya mapendekezo aliyoyasikia, kama yatakubalika na yakapita kama yalivyo, anaona uwezekano wa kupatikana katiba bora na ambayo Watanzania wanaitaka.

Marando ambaye pia ni mjumbe wa Kamati Kuu ya CHADEMA, amesema mapendekezo hayo yakipita, “tunaweza kuondoa mifarakano hata kama Katiba itaipendelea CCM.”

“Rais, kwa hatua hiyo, ataweza kutimiza “ndoto yake.” Ila bado wasiwasi wangu CCM haitakubali na hivyo itakuwa mgogoro,” anasema.

Mhadhiri mstaafu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Azaveli Lwaitama, huku akisifia hatua iliyopigwa, ametahadharisha kuwa bado anaona Rais Kikwete anakabiliwa na mtihani kupitia baadhi ya mawaziri wake, akiwataja waziri wa Sheria na Katiba, Mathias Chikawe na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri (Uratibu na Bunge), William Lukuvi.

“Mimi naona hili ni jambo zuri. Kama mapendekezo haya yataingia kwenye majedwali yale na kukubaliwa na chama cha CCM, hapo muafaka utapatikana… upatikane nje ya Bunge ili wasije wabunge wa CCM wakafika bungeni na mapendekezo yakapelekwa mpaka kufikia hatua ya kusema ‘sasa tupige kura.’ Hapa tutakuwa tumerudisha mgogoro maana inafahamika hili bunge ni la wabunge wengi wa CCM,” alisema.

Dk. Lwaitama pia aligusia ukimya wa mawaziri wa Rais Kikwete ambao wamekuwa wakimyumbisha, akisema rais anahitaji waziri wa sheria atakayemfanyia kazi nzuri ya kulipeleka mbele suala hili la kupatikana katiba wanayoitaka Watanzania.

“Haya mapendekezo yatakuwa na maana kama tutakuwa na waziri wa sheria atakayemshauri vizuri rais. Hii hali ya kushuhudia mawaziri wanaoona mambo yako kama kawaida, haitakiwi kwa sasa. Mawaziri wale wako kimya. Hatukuwasikia. Sasa hawa wajiuzulu kwanza.

“Lazima rais aombwe kuweka sawa watu wake, mawaziri wake pamoja na wabunge wa chama chake. Hatutaki mgogoro mapendekezo yakishaingia bungeni,” alisema Dk. Lwaitama.

Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba, Deus Kibamba amesema kwa marekebisho aliyosomewa, kama ndivyo yalivyo, ni “mwanzo mzuri. Hapa itakuwa hatua ya kunasua pale palipokwama.”

“Kama hivi unavyonisomea ndivyo yalivyo mapendekezo ya kurekebisha muswada unaohusu Katiba, inatia moyo. Lakini naogopa kuyapa sifa nyingi kwa sababu bado sina hakika kama hakutakuja mwanya wa kuchakachua.

“Kama rais hatateua tena wajumbe wale wa nje ya wabunge na wajumbe wa baraza la wawakilishi, ni sawa lakini je, watatokana na utaratibu gani. Kuna swali hapa halijajibika, makundi yanatajwa kwenye sheria?” anahoji.

Hata Kibamba anatilia shaka kitendo cha mawaziri Chikawe na Lukuvi. “Huyu Chikawe juzi tu, siku mbili zilizopita ameulizwa na vyombo vya habari kama kuna marekebisho yatapelekwa bungeni kupitishwa, akajibu kwa kuuliza, “Kwani kuna mpango tena hapa wa kufanyia marekebisho muswada uliopitishwa kwa utaratibu halali wa bunge?”

Amekosoa mtiririko wa dhana ya uwajibikaji wa pamoja upande wa serikali; akisema kuwa anaona utiifu kwa dhana hiyo unalegalega kwa Tanzania.

Kibamba alisema lipo eneo ambalo hana hakika kama limeguswa katika marekebisho yaliyofikiwa. Suala la wanasiasa kujipa mamlaka ya kuwa wengi ndani ya Bunge Maalum la Katiba kama vile suala la kupatikana kwa katiba ni suala la wanasiasa zaidi.

“Hapa najua wanasiasa hawapaangalii kwa sababu ni maslahi yanayowapendeza; lakini wamejiweka wengi kwenye Bunge la Katiba. Mimi naona hakukuwa na sababu. Badala yake wangeachiwa wananchi wakachagua wajumbe hawa,” alisema.

Kwa mujibu wa sheria ya sasa, Zanzibar itakuwa  na wajumbe 214. Kati yao, 78 ni wabunge wa Bunge la Muungano; 81 wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na 55 kutoka asasi za kiraia.

Kwenye mapendezo mapya ambayo yametajwa kuzingatia “haja ya uwakilishi sawa kwa washirika wa Muungano,” idadi ya wajumbe watakaoteuliwa kutoka Zanzibar itaongezeka hadi kufikia wajumbe 279.

error: Content is protected !!