May 26, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Muswada sheria uvunaji viungo vya binadamu kutua bungeni

Dk. Godwin Mollel, Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto

Spread the love

 

SERIKALI ya Tanzania imesema, inaandaa muswada wa sheria ya uvunaji, utunzaji na upandikizaji wa viungo vya binadamu. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Taarifa hiyo imetolewa leo Jumatano tarehe 28 Aprili 2021, na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Godwin Mollel, wakati akijibu swali la Mbunge Viti Maalumu, Rose Tweve, bungeni jijini Dodoma.

Dk. Mollel amesema, muswada wa sheria hiyo, itakayoongoza taratibu za uvunaji, utunzaji na upandikizaji viungo vya binadamu hasa figo na moyo, utawasilishwa bungeni katika vikao vya mhimili huo, vitavyoanza mwezi Septemba mwaka huu.

Naibu Waziri huyo wa afya amesema, kwa sasa wizara hiyo iko katika hatua za ukusanyaji maoni ya wadau kuhusu muswada huo.

“Tuko kwenye hatua ya kukusanya maoni ya wadau, kwenye bunge la mwezi wa sita tutaleta muswada kwa ajili ya kufanya hivyo,” amesema Dk. Mollel.

Awali, Tweve alisema kumekuwa na ongezeko kubwa la magonjwa yasiyo ya kuambikizwa hasa moyo na figo, na kuhoji Serikali ina mkakati gani wa kuanzisha utaratibu maalum wa kuvuna viungo hivyo kwa ajili ya kusaidia Watanzania wenye uhitaji wa viungo hivyo.

Ambapo Dk. Mollel alijibu akisema, kwa sasa shughuli ya upandikizaji viuongo hivyo inafanyika nchini kwa kutumia miongozo ya kimataifa inayosimamia uvunaji na upandikizaji wa viungo vya binadamu.

“Kwa kuwa huduma zimeshaanza kutolewa, kwa sasa nchi inatumia miongozo ya kimataifa inayosimamia uvunaji na upandikizaji wa viungo,” amesema Dk. Mollel.

Dk. Mollel amesema huduma hizo zinatolewa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili na Hospitali ya Benjamin Mkapa, na kwamba tangu Novemba 2017 hadi sasa, hospitali hizo zimepandikiza figo 80.

“Hadi sasa Hospitali ya Taifa Muhimbili imepandikiza Figo 62 na Hospitali ya Benjamin Mkapa imepandikiza Figo 18. Aidha, kwa upande wa upandikizaji wa moyo, Serikali inaendelea kujenga uwezo wa ndani wa kutoa huduma hiyo,” amesema Dk. Mollel.

error: Content is protected !!