November 30, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Muswada Bima ya Afya kwa wote wakwama bungeni

Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Bernard Konga

Spread the love

 

MUSWADA wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote, umeshindwa kusomwa kwa mara ya pili bungeni jijini Dodoma, kutokana na mhimili huo na Serikali kujadiliana kuhusu hoja kadhaa zilizoibuliwa na wabunge pamoja na wadau mbalimbali dhidi yake. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Kauli hiyo imetolewa leo Ijumaa, tarehe 11 Novemba 2022, bungeni jijini Dodoma na Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson.

Spika Tulia amesema, muswada huo ulipaswa kuwasilishwa bungeni leo na Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu, kwa ajili ya mjadala na kutunga sheria lakini umeshindwa kutokana na sababu hiyo.

“Nadhani mtakuwa mmeona kwenye orodha ya shughuli za Bunge kwamba leo tungeanza na hati za kuwasilisha mezani. Katika hati za kuwasilisha ipo iliyopaswa kuwasilishwa na Waziri wa Afya akifuatiwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii. Haitawasilishwa leo sababu Bunge pamoja na Serikali tunaendelea na mashauriano juu ya mambo ambayo hatujaafikiana vizuri,” amesema Spika Tulia.

“Tunaendelea na mashauriano katika hoja kadhaa ambazo zimeibuliwa na wabunge na wadau mbalimbali waliojitokeza mbele ya kamati na nyingine Serikali inaendelea kulitazama namna bora ya kuwahudumia wananchi kwenye eneo hili la bima ya afya,”

Baada ya muswada huo kusomwa kwa mara ya kwanza Bungeni jijini Dodoma, Septemba 2022, wadau mbalimbali walitoa ushauri kwa Serikali wakiitaka iusitishe kwa madai kwamba kuna masuala kadhaa yanapaswa yarekebishwe ili ipatikane sheria itakayowaweza wananchi kunufaika na bima ya afya kwa wote.

Miongoni mwa masuala yaliyoibuliwa ambayo yametajwa kuwa changamoto, ni kipengele kinachoelekeza ufutwaji wa mfuko wa afya ya jamii, hatua itakayopelekea wananchi wenye kipato kidogo kuingia katika skimu ya bima ya afya inayorithi vifurishi vya mifuko ya hifadhi ya jamii ambavyo ni vya gharama kubwa.

Suala lingine ni muswada huo kuweka vigezo vya kupata leseni, pasi ya kusafiria, kitambulisho cha NIDA, lazima uwe na kadi ya bima ya fya, kitendo kilichoelezwa na wadau kuwa kitanyima wananchi uhuru na haki yao ya kupata huduma hizo.

error: Content is protected !!