January 23, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Muswada Benki ya Posta wapita

Mwigulu Nchemba

Spread the love

KWA pamoja bunge limeridhia Muswada wa Sheria ya Benki ya Posta Tanzania (TPB) kwa mwaka 2015 uliolenga kufuta sheria iliyosajili benki hiyo ili sasa isajiliwe chini ya Sheria ya Makampuni. Anaandika Dany Tibason … (endelea).

Muswada huo umepitishwa leo huku wabunge hao wakionekana kuunga mkono bila kuwepo kwa msuguano kutoka pande zote.

Akisoma muswada huo kwa mara ya pili bungeni, Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba amesema, kwa zaidi ya miongo miwili tangu kuanzishwa kwa benki hiyo, kumekuwa na mafanikio makubwa akitolea mfano amana za wateja, idadi ya matawi kutoka tawi moja hadi 51, ofisi za mawakala wa benki 400 kwa mwaka 2014 na aina za huduma kutoka mbili mwaka 1992 hadi 22 mwaka 2014.

Mwiguli amesema, muswada huo unalenga kuiwezesha TPB kukidhi matakwa ya sheria ya mabenki na taasisi za fedha na kanuni zake hivyo benki hiyo kuwa endelevu na kuondokana na utegemezi wa ruzuku kutoka serikalini.

Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Uchumi, Viwanda na Biashara, Dunstan Kitandula amesema, muswada huo umepelekwa bungeni wakati muafaka kwa lengo la kutumia mabadiliko hayo kujitanua zaidi kibiashara.

Kitandula amesema, ni jambo la kusikitisha kuona Sheria ya Mabenki na Taasisi za Fedha ya Mwaka 2006 kuwepo kwa miaka 10 sasa bado serikali ilikataa kutekeleza matakwa hayo ya kisheria hivyo benki hiyo kuendeshwa kinyume cha matakwa ya kisheria.

Amesema, kamati yao inaendelea kuishauri serikali kuwa na sheria mahsusi itakayoshughulikia uendeshaji na usimamizi wa MFIs, Saccos na Vicoba nchini kutokana na ukweli kuwa, bado kuna udhaifu katika usajili, uendeshaji na usimamizi wa shughuli za kifedha.

Kitandula amesema, kamati inasikitishwa na kutotimizwa kwa ahadi ya serikali iliyotolewa bungeni ya kuwa na Sheria ya Microfinance mara tu baada ya kukamilika uandikwaji upya kwa sera za Asasi za Kifedha hapa nchini.

Akiwasilisha maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Mbunge wa Mkanyageni Habib Mnyaa amepongeza ufanisi wa TPB na kuitaka kutumia mabadiliko hayo ya kisheria kuchochoa kukuza uchumi kwa wananchi hasa wanyonge.

Mnyaa ameitaka serikali kuwekeza kwa asilimia 100 kwenye benki hiyo na kuachana na tabia ya kutafuta wawekezaji kutoka nje kwa kuwa madhara yake yameonekana katika Benki ya Biashara ya Taifa (NBC 1997).

“Mheshimiwa mwenyekiti pia tunapenda kutoa changamoto kwa watendaji wakuu wa benki zetu hapa nchini kujitanua hadi nje ya nchi kama mabenki ya nchi nyingine yanavyokuja nchini kuwekeza, tulitarajia NMB kwa sababu inamilikiwa na Waholanzi ingeenda kuwekeza huko kwao,” amesema.

Akichangia Muswada huo Mbunge wa Ngara (CCM), Deogratius Ntukamazina amesema, iwapo TBP itapata mtaji mzuri ni dhahiri kuwa itasaidi wananchi wanyonge kwani haina masharti magumu.

Ntukamazina amesema, benki hiyo inahitajika kufungua matawi vijijini ili iweze kuwakopesha wajasiriamali ambao wamejiunga na Vokoba kote nchini.

Mbunge wa Longido, Michael Laizer (CCM) amesema, ni vema kuwepo kwa uwazi katika mchakato mzima wa utendaji wa benki hiyo hasa katika kipindi hiki ambacho inaingia katika mabadiliko ya utoaji huduma kisheria.

Mbunge wa Manyoni Mashariki, Kapteni John Chiligati (CCM) ameitaka TPB kukaa na menejimenti ya Mpango wa Kurasimisha Mali za Wanyonge Tanzania (Mkurabita) ili kukubaliana kuongeza wateja.

error: Content is protected !!