MUSWAADA wa Vyama vya Sisasa uliowasilishwa bungeni na serikali kwenye mkutano uliyopita wa Bunge na ambao umeanza kujadiliwa kwenye ngazi ya Kamati, umebeba vifungu vinavyopingana na Katiba ya Jamhuri ya Muungano. Anaripoti Danson Kaijage, Dodoma … (endelea).
Muswaada unatoa adhabu za kijinai kwenye makosa ya kiutendaji. Ndani ya Muswaada kumewekwa vifungo kwa watu binafsi na taasisi; na kumechongwa adhabu zisizoendana na makosa yaliyoainishwa.
Ndani ya Muswaada kumewekwa vifungu vinavyompa msajili mamlaka ya kufuta chama kwa sababu ya makosa ya kiutendaji; kinyume na Katiba ya Jamhuri. Muswaada unatoa adhabu ya mamilioni ya shilingi kwa watu binafsi; na au taasisi.
Marekebisho yaliyopo ndani ya Muswaada huu, yanatoa mamlaka yasiyo na mipaka kwa msajili; na yanazuia fursa ya ushindani huru kwenye jukwaa la kisiasa.
Katika muswaada huu, bado msajili anabaki kuwa mteule wa rais, ambaye ni mwenyekiti wa chama cha siasa. Lakini papo hapo, anapewa mamlaka juu ya vyama vingine, ikiwemo kusimamisha mtu uwanachama; kufuta usajili wa vyama, kutaka taarifa yoyote kutoka kwenye vyama, na kutaka vyama vibadilishe katiba zao.
Katiba ya Jamhuri (1977), Ibara ya 13 (1), inaeleza kuwa watu wote ni sawa mbele ya sheria, na wanayo haki bila ya ubaguzi wowote, kulindwa na kupata haki sawa mbele ya sheria.
Nayo Ibara ya 20 (1), inaeleza kuwa kila mtu anao uhuru wa kukutana na watu wengine kwa hiari yake na kwa amani; kuchanganyika, kushirikiana na watu wengine, na kwa ajili hiyo kutoa mawazo yake hadharani na kuanzisha na kujiunga na vyama au mashirika yalioanzishwa kwa madhumuni ya kuhifadhi au kuendeleza imani au maslahi yake au maslahi mengineyo.
Katika Ibara ya 107A (1), kumeelezwa kuwa mamlaka yenye kauli ya mwisho ya utoaji haki katika Jamhuri ya Muungano itakuwa ni mahakama.
Muswaada unampa dhamana waziri mwenye dhamana jukumu la kutengeneza kanuni kuhusu masuala ya ndani ya vyama vya siasa bila kujali kuwa waziri ni mwanachama wa chama fulani.
Muswaada unakataza; na au kudhibiti, shughuli halali za vyama vya siasa na uhuru wa kujieleza. Unakataza mashirika yanayotaka kutoa elimu ya uraia na ya kujenga uwezo kwa vyama vya siasa.
Kwenye marekebisho ya sheria ya vyama vya siasa, kumewekwa vifungu vinavyozuia vyama kufanya kazi kama vikundi vya ushawishi – kazi muhimu za vyama vya siasa – na umeainisha makosa kwa chama “kutoa kauli ambazo siyo za kweli.”
Kimsingi, kifungu hiki kinaashiria demokrasia na haki ya msingi ya uhuru wa kujieleza kuwa mgumu. Hii ni kwa sababu, ni vigumu kuainisha upi ni ukweli na upi ni uwongo hasa katika masuala yenye utata hasa inapotokea mvutano wa kimtazamo au kiitikadi.
Vyama vinavyoathirika na maamuzi ya Msajili havina nafasi ya kutosha ya kujitetea. Marekebisho (na sheria kuu) yanampa Msajili mamlaka makubwa sana bila uwajibikaji. Ana mamlaka ya kuvinyima vyama ruzuku, kuvisimamisha, kuvifutia usajili na kuvibana kwenye makosa mbalimbali. Maamuzi ya msajili kwa kiwango kikubwa ni ya mwisho.
Kimsingi, sheria inahusu kudhibiti usajili na utendaji kazi wa vyama vya siasa. Kwa masuala mengine na makosa, wanachama na viongozi wa vyama vya siasa wanapaswa kuheshimu sheria zilizoko.
Marekebisho ya sheria yametumia vifungu na maneno yasiyo na maana ya moja kwa moja ambayo kisheria yanaweza kuwa na maana zaidi ya moja na hivyo kuruhusu maamuzi yasiyo na usawa.
Kwa mujibu wa uchambuzi uliofanywa na mashirika yasiyo kuwa ya kiserikali, kama vile, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Twaweza, Chama cha Wanasheria Tanganyika – Tanganyika Law Society (TLS) – Baraza la Habari Tanzania – Media Council of Tanzania (MCT), Center For Strategic Litigation na Jumuiya ya waandishi wa habari Zanzibar (WAHAMAZA).
Baadhi ya vifungu katika sheria hii, vinampa Msajili mamlaka ya kufanya maamuzi yenye madhara makubwa kwa vyama kwa kufuata kile “anachokiamini” au kwa “kutoridhishwa” na jambo fulani mapitio ya Sheria zilizoko, mikataba na kanuni.
Vifungu vilivyomo ndani ya Muswaada vinaweka masharti ya kutungwa kwa kanuni za sheria ya utawala na adhabu; mkataba wa kimataifa wa haki za kiraia na kisiasa (ICCPR) 1966.
Nafasi ya vyama imebanwa sana na hakuna ufuatiliaji wa kutosha wa kazi zinazofanywa na msajili.
Leave a comment