JIMBO la Musoma Vijijini, mkoani Mara, limeomba Serikali kuhakikisha ujenzi wa Barabara ya Musoma-Makojo-Busekera, unaanza baraka baada ya mwaka mpya wa fedha (2023/24), kuanza. Anaripoti Mwandishi Wetu, Mara … (endelea).
Ombi hilo limetolewa leo tarehe 23 Mei 2023 na Ofisi ya Mbunge wa Musoma Vijijini, Prof. Sospeter Muhongo.
Mbali na ombi la mradi huo kuanza mapema, jimbo hilo limeshauri mkandarasi atakayepewa tenda ya ujenzi huo kuwa na uzoefu.
“Achukuliwe mkandarasi mzoefu na anayejitosheleza kwenye vifaa vya ujenzi. Ujenzi uanze haraka baada ya bajeti ya Serikali kwa 2023/2024, yaani tarehe 1 Julai 2023,” imesema taarifa hiyo.
Aidha, jimbo hilo limemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan, pamoja na Serikali yake kwa kutenga bajeti ya kutosha kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ikiwemo barabara hiyo.
Taarifa hiyo imesema, ujenzi huo umepangwa kufanyika kwa awamu mbili, ambapo fedha za utekelezaji mradi huo zimetengwa katika Bajeti ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kwa mwaka ujao wa fedha.
Taarifa hiyo imesema ujenzi wa awamu ya kwanza wa barabara yenye urefu wa kilomita 40 ulishaanza kwa kilomita tano kuanzia Kijiji Cha Kusenyi-Makojo-Busekera.
Ujenzi wa awamu ya pili inatarajia kuanza Kijiji Cha Kusenyi kuelekea Musoma Mjini.
Leave a comment