Saturday , 2 December 2023
Home Gazeti Habari za Siasa Musiba sasa ahamia kwa marais wastaafu
Habari za SiasaTangulizi

Musiba sasa ahamia kwa marais wastaafu

Cyprian Musiba
Spread the love

CYPRIAN Musiba, mwanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), aliyejipambanua kuwa mtetezi mkuu wa Rais John Magufuli, amewatuhumu watangulizi wa rais huyo wa sasa, kuwa baadhi yao “waliigeuza Ikulu kuwa danguro la kutafutia utajiri.” Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Alhamisi wiki hii, Musiba alisema, “ukimuondoa Mwalimu Julius Nyerere (rais wa kwanza wa Tanzania), wengine wote walioshika nafasi hiyo, “ni wezi watupu.”

“Marais wote wastaafu na wake zao, ukimuondoa Mwalimu Nyerere, walitumia Ikulu kujitajirisha,” amesema Musiba na kusisitiza, “siwashambulii wala kuwasingizia, kama ambavyo baadhi ya watu wanavyosema. Huo ndio ukweli.”

Amesema, viongozi hao waliitumia Ikulu kikamilifu kujitajirisha binafsi. Anasema, hata wenzao wao, walianzisha makampuni na taasisi kadhaa kwa lengo la kukusanya mabilioni ya shingi, ili kukidhi mahitaji yao na familia zao.

Waliowahi kuwa marais wa Tanzania na ambao wanatuhumiwa na Musiba kugeuza Ikulu kuwa pango la walanguzi, ni pamoja na Alli Hassani Mwinyi, aliyeongoza taifa hilo kati ya mwaka 1984 na 1995; Benjamin William Mkapa (1995 hadi 20015) na Jakaya Mrisho Kikwete (2005 hadi 2015).

Kuibuka kwa Musiba kutuhumu marais hao wastaafu na wenza wao, kumekuja wiki moja tangu makatibu wakuu wawili wa zamani wa chama hicho tawala, Kanali Abdulrahman Kinana na Luteni Yusuf Makamba, kulalamika kuchafuliwa.

Katika andishi lao la kurasa tatu kwa umma, Kinana na Makamba wamesema, “pasipo kuwasilishwa ushahidi wowote, Musiba amekuwa akituhumu kila mmoja kuwa anapanga njama za kutaka kumhujumu Rais Magufuli.”

Wanaonya kuwa hatua ya viongozi wakuu wa chama hicho walioko sasa, kunyamazia kauli na matendo ya Musiba, kunaweza kusababisha kutokea kwa mifarakano, jambo ambalo linaweza kukimega chama hicho.

Aidha, kuibuka kwa Musiba kumekuja katika kipindi ambacho viongozi hao wawili – Kinana na Makamba – wamenukuliwa wakisema, tayari wamewasilisha malalamiko yao juu ya jambo hilo kwa katibu wa viongozi wakuu wastaafu, Pius Msekwa na mwenyekiti wake, Rais mstaafu Mwinyi.

Vilevile, kuibuka kwa Musiba kutuhumu Mwinyi, Mkapa na Kikwete, kumekuja katika kipindi ambacho kumeripotiwa kuwapo audio zinazowanukuu viongozi hao, wakimtuhumu Rais Magufuli, kushindwa kuongoza chama na serikali.

Mbali na tuhuma za kushindwa kuongoza serikali, baadhi ya viongozi hao wamesikika wakidai kuwa hatua ya viongozi wakuu wa nchi, kunyamazia ama kubariki kauli za Musiba, kwaweza kuhatarisha Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Musiba amekuwa akiwatuhumu viongozi hao na wengine wandamizi, wakiwamo viongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), kupanga njama za kumhujumu Rais Magufuli.

Kauli hiyo ya Musiba, ndiyo ambayo Kinana na Makamba wanasema, “inalenga kugombanisha viongozi wa SMZ na wale wa Tanganyika, jambo ambalo linaweza kusababisha kuvunjika kwa Muungano.”

Tuhuma za Musiba dhidi ya viongozi wakuu wastaafu zimekuja siku tano baada ya Rais Magufuli, kumuengua kwenye wazifa wa uwaziri, January Makamba; mtoto wa Yusuf Makamba.

Katika mkutano wake wa juzi Alhamisi na waandishi wa habari, Musiba ameendelea kusisitiza kuwa wake wa marais hao wastaafu na wao wenyewe, wamefanya vitendo vingi viovu vilivyodhoofisha uchumi wa taifa.

Kutajwa kwa marais wastaafu na wenza wao, kumetafsiriwa na wachambuzi wa kisiasa, kuwa kumenogesha mjadala kuwa chini ya Musiba, hakuna aliyepo salama.

Katika kipindi cha uongozi cha Rais Benjamin Mkapa, Mama Anna Mkapa alikuwa anaendesha na kusimamia Mfuko wa Fursa Sawa kwa Wote (EOTF). Mpaka anaondoka madarakani, Desemba 2005, hajaeleza ni akina nani walichangia fedha mfuko huo na jinsi zilivyotumika. Mama Anna Mkapa ndiye mwenyekiti wa taasisi hiyo.

Mfuko wa Mama Mkapa, ulianzishwa mara baaada ya Mkapa kuingia madarakani, Novemba 1995. Kwa muda wote ambao Mkapa alikuwa ikulu, mfuko huu ulikuwa unaendeshea shughuli zake katika majengo ya Ikulu.

Taarifa zinasema, hata gharama za bili ya maji, umeme, simu na mishahara ya wafanyakazi vililipwa na serikali. Misaada na michango iliyotolewa na wafadhili, mingi ilitolewa kwa kuwa mwenyekiti wake ni mke wa rais; mfuko ulionekana kama vile ni wa umma.

Akiongea kwa njia ya kumuingiza Mkapa katika dhahama, Musiba anasema, “tumuache Rais Magufuli afanye kazi. Hawa wengine wote walikuwa majizi. Watanzania wamepata rais ambaye hajawahi kutokea baada ya Mwalimu Nyerere.”

Anna Mkapa, anatajwa kuwa amejilimbikizia mali nyingi zenye thamani kubwa. Anatajwa kuwa yeye na mumewe, ndio wamilik wa mali nyingi za thamani.

Nao wake wa rais Mwinyi, Mama Sitti na Bi Hadija, walituhumiwa kugeuza Ikulu, kuwa pango la walanguzi. Katika kipindi cha utawala wa Rais Mwinyi, ndipo wafanyabiashara kadhaa “waliingia Ikulu, bila kubisha hodi.”

Kuna wakati Mwalimu Nyerere aliwahi kumtuhumu rais Mwinyi, kuwa anaendesha nchi kwa kufuata ushauri wa wake zake.

Naye Salma Kikwete, mke wa rais Jakaya Kikwete, kama ilivyokuwa kwa Mama Anna Mkapa, alianzisha taasisi binafsi iitwayo, “Wanawake na Maendeleo (WAMA). Taasisi hii ilianzishwa mara baada ya Kikwete kuingia madarakani.

Taasisi ya Mama Salma, nayo ilikusanya mamilioni ya shilingi na dola za Marekani; mpaka wanaondoka Ikulu, Novemba 2015, hakuna aliyeleza fedha walizokusanya kupitia taasisi hiyo zimetumikaje, huku kinachoitwa, “maendeleo kwa wanawake wa Tanzania,” kikiwa hakionekani.

Luteni Yusuf Makamba, amekuwa katibu mkuu wa chama hicho kati ya mwaka 2007 hadi 2011. Alichukua nafasi hiyo kutokea kwa Philip Mangula.

Naye Kinana alipokea wadhifa huo wa ukatibu mkuu kutokea kwa Wilson Mukama. Aliongoza CCM kutoka mwaka 2012 hadi 2018. Kinana amepata kuhudumu pia kama Spika wa Bunge la Afrika Mashariki.

Mukama alihudumu kwenye nafasi ya ukatibu mkuu wa CCM, kati ya mwaka 2011-2012. Kabla ya kuwa katibu mkuu wa CCM, Mukama amepata kuhudumu kama katibu mkuu kwenye wizara ya afya.

“Tumetafakari kwa kina kabla ya kuamua kutoa taarifa hii kwa umma kuhusiana na uzushi alioutoa Cyprian Musiba dhidi yetu katika nyakati mbili tofauti,” inasema sehemu ya barua ya Kinana na Makamba.

Tafsiri inayopatikana hapa ni kwamba kisiasa viongozi hawa wawili hawakutaka suala hilo liishie kwenye vikao vya ndani ya chama.

Kanal Kinana na Luteni Makamba wameonyesha kufahamu kinachoendelea na nani anamtuma mwanaharakati huyo kuwatuhumu. Hilo linathibitishwa na aya ya pili ya barua yao inayoeleza, “huyu anayetuhumu anatekeleza maagizo kama kipaza sauti.”

Barua inasema, “yeye anatumwa kutekeleza maagizo na kutumika kama kipaza sauti tu.” Sentensi hii peke inadhihirisha kuwa viongozi hawa wastaafu wana mengi mioyoni mwao ama wamechoshwa kukaa nayo pamoja na kuendelea kuvumilia kuchafuliwa na kuvunjiwa heshima kama walivyosema.

“Kwamba yupo mtu au kundi la watu ambao linamtumia mwanaharakati huyo kuwatuhumu viongozi wastaafu. Mantiki inatuelekeza kuwa Kinana na Makamba wanazo taarifa juu ya ‘mtu’ aliyeko nyuma ya harakati za zinazorushwa kwao, hivyo badala ya kuzitamka mwenyewe ameamua kutumia wakala.”

Barua ya Kinana na Makamba na kauli za Musiba, zimeibua makundi mawili – linalotetea makatibu hao wa Kikwete dhidi ya kundi jipya la kiongozi wa sasa wa nchi na CCM.

Makundi hayo mawili yamekuwa na kazi ya kulinda urithi mzuri wa viongozi wastaafu, huku lingine likiwa na wajibu wa kulinda maslahi ya mwenyekiti wa sasa wa CCM.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari MchanganyikoTangulizi

Mwalimu jela miaka mitatu kwa rushwa

Spread the loveMAHAKAMA ya Hakimu Mfawidhi, wilaya ya Igunga, mkoani Tabora imemhukumu...

Habari za Siasa

Rais Samia kuzindua programu ya nishati safi ya kupikia kwa wanawake Afrika

Spread the loveRais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuzindua programu ya...

Habari za Siasa

AG aiagiza kamati ya maadili kuwashughulikia mawakili wanaokiuka maadili

Spread the loveMWANASHERIA Mkuu wa Serikali (AG), Dk. Eliezer Feleshi, ameagiza Kamati...

Habari za Siasa

Jaji avunja ukimya sakata la Mpoki kusimamishwa uwakili

Spread the loveJAJI Mkuu wa Tanzania, Prof. Ibrahim Juma, amekitaka Chama cha...

error: Content is protected !!