Sunday , 19 May 2024
Makala & UchambuziTangulizi

Mungu msamehe Mtolea

Abdallah Mtolea, aliyekuwa Mbunge wa Temeke
Spread the love

NIMELAZIMIKA kujitosa kwenye mjadala unaohusu kujiuzulu wadhifa wa ubunge kwa Abdallah Mtolea, aliyekuwa mbunge wa Chama cha Wananchi (CUF), katika jimbo la Temeke, jijini Dar es Salaam. Anaandika Saed Kubenea … (endelea). 

Mtolea alitangaza kujiuzulu ubunge waliompa wananchi wa Temeke, tarehe 15 Novemba 2018. Ilikuwa katikati ya mjadala wa muswada wa uendeshaji wa taasisi ndogo za kifedha.

Mara baada ya kuitwa na Spika wa Bunge, Job Ndugai, kuchangia muswada huo, Mtolea alisema, anachukua nafasi hiyo kumjulisha spika na umma kuwa ameamua kujiuzulu ubunge.

Muda mfupi baadaye, akaonekana ameongozana na Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Bashiru Ally na kutangaza kujiunga na chama hicho.

Kama walivyofanya wengine waliotoka upinzani na kujiunga na chama tawala, Mtolea alisema, “nimeamua kujiuzulu ubunge, ili kuunga mkono juhudi za Rais John Magufuli katika kuendesha nchi.”

Mtolea anakuwa mbunge wa tatu wa CUF kujiuzulu na wa pili jiji la Dar es Salaam.

Wabunge wengine wa chama hicho waliojiuzulu, ni pamoja na aliyekuwa mbunge wa Kinondoni, Maulid Mtulia na aliyekuwa mbunge wa Liwale, mkoani Lindi, Zuberi Kuchauka.

Nimeamua kumjadili Mtolea kwa sababu nyingi. Miongoni mwao, ni hizi zifuatazo:

Kwanza, alikuwa mmoja kati ya wabunge wa upinzani jijini Dar es Salaam, waliotangazwa kwa mbinde kuwa washindi katika uchaguzi mkuu wa 25 Oktoba 2015.

Msimamizi wa uchaguzi jimboni Temeke, alimtangaza Mtolea kuwa mbunge, baada ya kuona hatari ya damu kumwagika. Alimtangaza kuwa mbunge baada ya baadhi ya akina mama kukesha wakiwa wamebeba vichanga vyao mgongoni ili kulinda “kura zake.”

Alitangazwa baada ya mamia ya vijana na wazee, kusimama kidete kulinda ushindi wake. Alitangazwa baada ya jasho kumwagika na miguu ya wazee kuvimba.

Si hivyo tu: Baada ya njama za kupora ushindi wake kukwama, aliyekuwa mshindani wake, Abas Mtemvu (CCM), alikimbilia mahakamani kupinga ubunge wake.

Hatukumtupa. Tulimshika mkono kwa kuongozana naye mahakamani kila siku ya kesi. Tulichanga sehemu ya tulichokuwa nacho, ili kumsaidia kulipia sehemu ya gharama za mawakili wake. Tuliweka hata magari yetu mafuta ili kubeba baadhi ya wafuasi wake.

Pili, Mtolea alikuwa moja ya nguzo muhimu ya upinzani bungeni. Alikuwa kiungo mahiri kwa vyama vinavyounda jumuiko la Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA).

Ndani ya Bunge, alikuwa naibu kiongozi wa kambi rasmi ya upinzani. Alikuwa pia kiongozi wa wabunge wa CUF.

Tatu, siku moja kabla ya kutangaza “kuunga mkono juhudi,” tulikutana na kuzungumza mengi. Miongoni mwa tuliyojadili, ni mustakabali wa kisiasa wa vyama vyetu na sisi wenyewe.

Hakuna kokote kwenye mazungumzo yetu ambako Mtolea alionyesha hofu ya kutetea ubunge wake. Hakuna alikoonyesha shauku ya kutaka kujiunga na CCM.

Tuliachana naye, majira ya saa tano usiku, katika eneo la Dodoma hoteli akionekana imara na jasiri. Tulikuwa tunatokea kwenye hafla ya uuzaji wa hisa za Benki ya Dar es Salaam Commercial Bank PLC (DCB).

Nikikumbuka jinsi nilivyokesha pale Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kulinda kura za wananchi wa Ubungo, hakika hatua ya Mtolea, imenitia simanzi sana.

Aidha, nikikumbuka jinsi wananchi wa Temeke na maeneo mengine ya Dar es Salaam, walivyotuunga mkono katika uchaguzi mkuu uliyopita, kitendo cha Mtolea, kimenitoa machozi.

Nikikumbuka jinsi wananchi walivyochanga sumuni sumuni zao kuhakikisha yeye na sisi wengine tunashinda uchaguzi huo, kujiuzulu kwake, kumenifedhesha na kumenihuzunisha sana.

Hii ni kwa sababu, kinyang’anyiro cha uchaguzi mkuu uliyopita, kilikuwa kigumu mno. Baadhi ya waliotangazwa, siyo walioshinda. Wale walioshinda– hasa kutoka upinza – siyo waliotangazwa.

Karibu katika maeneo mengi ya nchi, uchaguzi ulitawaliwa na hila na vitimbi, kutokana na chama kilichopo Ikulu kuonekana kinaelekea kushindwa.

Binafsi, nilitangazwa kwa mbinde kuwa mshindi wa kiti cha ubunge, dhidi ya aliyekuwa mshindani wangu mkuu, Didas Masaburi (CCM).

Kama ilivyokuwa kwa wengine wengi, ushindi wangu, ulipatikana baada ya wananchi kuweka shinikizo dhidi ya waliotaka kupora haki yao.

Nilitangazwa kabla ya Maulid Mtulia (Kinondoni); Halima James Mdee (Kawe) na John Mnyika (Mnyika).

Nikaona ushindi huo hauwezi kuwa wa maana, iwapo wenzangu hao, ambao wakati huo, tulikuwa tunatokea halmashauri moja ya Kinondoni, hawajatangazwa kushinda.

Nikaamua kutumia rasimali nilizokuwa nazo, hasa baadhi ya vijana wa bodaboda, kuhakikisha wenzangu hawa, wanatangazwa kuwa washindi.

Kweli walitangazwa, ingawa katikati ya mtutu wa bunduki. Walitangazwa katikati ya mabomu ya machozi na mifereji ya damu.

Nimezisikia sababu za Mtolea kujiondoa CUF. Nimesikia utetezi wake. Anadai kuwa haoni nuru huko alikokuwa. Anasema mgogoro ndani ya chama chake, umekidhoofisha sana na hivyo anaona njia pekee ni yeye kuukimbia.

Hakuna hata moja kati ya aliyosema, lenye chembe ya mashiko. Kwa ufahamu wangu, hata kama Mtolea angeamua – baada ya kumaliza ubunge wake mwaka 2020 – kujiunga na vyama vingine rafiki ndani ya UKAWA, bado angeweza kushinda uchaguzi unaokuja.

Badala yake, ameamua kuuza utu wake. Ameamua kuuza heshima ambayo wananchi wa Temeke walimpa. Ameamua kusaliti wananchi.

Ameungana na walioko madarakani, kunyonga haki za wananchi.

Wapo wanaoamini kuwa kujiuzulu kwa Mtolea kumesukumwa na hatua ya Rais Magufuli, kumteuwa aliyekuwa mbunge wa Chadema katika jimbo la Ukonga, Mwita Mwaikabe Waitara, kuwa naibu waziri.

Katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, Waitara alikuwa miongoni mwa wabunge sita wa upinzani jijini Dar es Salaam.

Nihitimishe kwa kusema, Mungu atamlipa kile anachostahili Mtolea.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari MchanganyikoHabari za SiasaTangulizi

Wakili Mwabukusi anusurika kufungiwa, asema hatarudi nyuma

Spread the loveWAKILI Boniface Mwabukusi amesema kuwa hatorudi nyuma kuwatetea Watanzania na...

Habari MchanganyikoHabari za SiasaTangulizi

Lissu akabidhiwa gari lake, aomba msaada wa matengenezo

Spread the loveMakamu Mwenyekiti wa Chadema Bara, Tundu Lissu leo Ijumaa amekabidhiwa...

Habari za SiasaTangulizi

Haya hapa majina walioteuliwa kugombea nafasi mbalimbali CHADEMA

Spread the loveCHAGUZI wa kanda za Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA)...

Habari MchanganyikoHabari za SiasaTangulizi

Uingereza yamwaga bil. 9 kumuunga mkono Samia matumizi nishati

Spread the loveWaziri Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Selemani...

error: Content is protected !!