May 27, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mchumba wa Maunda Zoro: Tulitarajia kufunga ndoa Julai

Mume wa aliyekuwa Msanii wa Bongo fleva, Maunda Zoro

Spread the love

 

MCHUMBA wa aliyekuwa Msanii wa Bongo fleva, Maunda Zoro ambaye amefariki dunia jana Kigamboni jijini Dar es Salaam, amefunguka kwamba alitarajia kufunga ndoa na mkewe mwezi Julai mwaka huu. Anaripoti Faki Ubwa, Dar es Salaam … (endelea).

Maunda ambaye kwa jina lingine alifahamika kama Hellen baada ya kubadili dini kutoka Uislam kuelekea Ukristu, amefariki dunia jana tarehe 13 Aprili, 2022 baada ya gari yake kuacha njia na kuligonga lori la mchanga.

Akizungumza na waandishi wa habari kwa masharti ya kutotajwa majina yake, Mumewe Maunda amesema walishamaliza hatua zote za maandalizi ya ndoa lakini miezi mitatu nyuma walipata pigo.

“Nilifiwa na kaka yangu…kama sio msiba huo tungekuwa tumeshafunga ndoa, sasa tulipanga ifanyike mwezi saba au wa nane,” amesema.

Amesema yeye na Maunda wamezaa watoto watatu ambapo mtoto wa kwanza ana miaka 12 anaitwa Rishard, wa pili ana miaka sita anaitwa Zack na watatu ana miaka 4 anaitwa Angella.

Amesema jana usiku alipigiwa simu na kuelezwa kuwa imeonekana gari inayofanana na ya mzazi mwenziye imepata ajali lakini mtoa taarifa hakuwa na uhakika juu ya taarifa za gari hiyo.

“Niliamua kumpigia simu Mkuu wa Trafki Kigamboni ambaye alifanya mawasiliano na kunithibitishia kwa namba ya gari iliyopata ajali ni ya mke wangu mtarajiwa,“ amesema.

 

Maunda Zorro

Amesema kuwa mpaka ‘Breakdown’ inafika eneo la tukio Maunda alikuwa hai na kwamba alikuwa hawezi kutoka kutokana na kubanwa na gari.

Amesema mpaka anaondolewa kwenye gari yake alikuwa tayari amefariki dunia.

Aidha, kaka wa marehemu, Banana Zorro familia hiyo ilikuwa kwenye hatua za mwisho za maandalizi ya ndoa ya Maunda Zorro.

Banana amesema taarifa za kifo cha Maunda zilimshtua na alipata taarifa hizo muda wa saa 4 usiku kwamba dada yake amepata ajali hatua chache kuelekea nyumbani kwake.

“Maunda amepata ajali alipokuwa akirejea nyumbani kwake Toangoma. Kutoka eneo alikopata ajali na nyumbani kwake ni kama dakika tano tu kwa mwendo wa gari” amesema Banana.

Aidha, Banana ametoa ratiba ya msiba huo kwamba waombelezaji wanakutana nyumbani kwa baba yao Mzee Zahir Ali Zorro.

Amesema kwamba Maunda atahifadhiwa kwenye nyumba yake ya milele siku ya Jumamosi huku Toangoma.

Wakati Mzee Zahir Zorro Baba mzazi wa Maunda amesema amepata pigo kubwa kumpoteza mtoto wake na kwamba alipata ishara mbaya kwa muda wa wiki nzima.

“Maunda hana kawaida ya kupita siku bila kuongea nami mara mbili au tatu. Huwa ninaongea naye mpaka saa nane za usiku lakini wiki hii hatujazungumza kabisa,” Amesema Mzee Zahir huku akibubujikwa na machozi.

error: Content is protected !!